Maandamano Chadema yaweka rekodi, Mbowe atoa msimamo

Viongozi waandamizi wa Chadema Taifa wakiongozwa na mwenyekiti wao, Freeman Mbowe leo wameongoza wafuasi wa chama hicho katika maandamano ya kupinga miswada ya sheria za uchaguzi iliyowasilishwa bungeni, yaliofanyika jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga na Said Khamis

Muktasari:

  • Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimefanya maandamano makubwa ya amani. Maandamano hayo yameibua mijadala maeneo mbalimbali huku wachambuzi wa kisiasa, diplomasia wakiyazungumza kwa mitizamo tofauti.

Dar es Salaam. Maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) yametikisa Jiji la Dar es Salaam baada ya viongozi, wanachama, wafuasi na wananchi wengine kujumuika pamoja kwenye maandamano hayo.

Maandamano hayo yaliyoishia katika ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) jijini Dar es Salaam yalianza rasmi majira ya saa 5 asubuhi, lakini makada na wafuasi wa chama hicho walianza kujitokeza katika maeneo ya Mbezi Luis, Buguruni na Kariakoo kuanzia saa 12 asubuhi.

Januari 13, 2024 Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangaza maandamano hayo yaliyopangwa na kamati kuu ya chama hicho, akisema lengo ni kupinga miswada ya sheria za uchaguzi iliyowasilishwa bungeni na kutaka Serikali itengeneze mpango wa dharura wa kukabiliana na kupanda gharama za maisha kwa Watanzania.

🔴#LIVE: Mbowe, Lissu waongoza maandamano Chadema

Miswada ya uchaguzi inayopingwa ni ule wa sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani,  Sheria ya Tume ya Uchaguzi Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa yote ya mwaka 2023, ambayo Chadema inasema haikuzingatia maoni ya wananchi.


Kilomita 35 za maandamano

Maandamano hayo marefu kuwahi kufanyika nchini, yalikuwa ya njia mbili, moja ikiongozwa  na Mwenyekiti Freeman Mbowe kuanzia Buguruni kupitia Barabara ya Uhuru hadi Kariakoo na kisha Barabara ya Morogoro hadi Shekilango.

Njia ya pili iliongozwa na Tundu Lissu, makamu mwenyekiti wa Chadema-Bara, kuanzia Mbezi Luis hadi Shekilango walipoungana na wenzao kisha wote kwenda ofisi za Umoja wa Mataifa, jijini Dar es Salaam.

Walioandamana njia ya Buguruni – Kariakoo – Shekilango – PSSSF Tower zilipo ofisi za UN, walitembea umbali wa kilomita 16.1 huku wenzao walioandamana njia ya Mbezi – Kimara – Shekilango – PSSSF Tower wakiandamana umbali wa kilomita 18.5.

Maandamano hayo yalikuwa ya amani huku yakisindikizwa na Jeshi la Polisi kuanzia mwanzo wa safari hadi mwisho na kuweka rekodi ya maandamano makubwa ya kupinga jambo kusindikwa kwa amani.

Njiani, wafuasi wa chama hicho walikuwa wakiimba nyimbo za hamasa huku wakiendelea kusonga mbele.

Wapo waandamanaji waliotumia pikipiki, bajaji na magari yaliyopambwa na bendera za chama hicho. Matalani Lissu alikuwa akipanda gari lenye uwazi juu na wakati mwingine akishuka na kutembea. Mbowe alitembea kwa miguu mwanzo-mwisho.

Kuna wakati umati wa waandamanaji ulisababisha msongamano mitaani na kusimamisha shughuli kwa muda kuruhusu upite.

Moja ya matukio ni la Mbowe alipofika Mtaa wa Msimbazi Polisi alipokutana na Kamanda wa Polisi kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, akapigia saluti kama ya kijeshi, kisha wakasalimia na kuzungumza kwa sekunde kadhaa.

Wachambuzi wa siasa wanaeleza maandamano hayo yamefanikiwa kwa kuangalia mwitikio mkubwa wa wananchi walioshiriki na hivyo kushauri madai ya chama hicho yafanyiwe kazi na Serikali.

Kamanda Muliro, mshangao maandamano Chadema

Hali ilivyokuwa

Wengi waliojitokeza walikuwa wamebeba mabango, bendera na kuimba nyimbo mbalimbali zilizokuwa zinapigwa kupitia magari maalumu ya hamasa ya wazi.

Miongoni mwa mabango yalikuwa yameandikwa: “Ugumu wa maisha Tanzania ni mpango wa CCM, sio mpango wa Mungu, “Kurudi nyuma mwiko mpaka tupate Katiba mpya”, “Miaka 62 maisha hayabadiliki, tunataka Katiba mpya.”

Pia, mengine yaliandikwa, “Ahadi nyingi za CCM ni za uongo”, “Serikali iondoe miswada bungeni”, “Gharama za maisha zipo juu, maoni ya wananchi yaheshimiwe”.

Lipo pia lililosomeka “Uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 usimamiwe na Tume Huru ya Uchaguzi.”


Wanawake wavaa viroba

Baadhi ya wanawake wameibuka kwenye maandamano ya amani ya Chama cha Demokrasia ya Maendeleo(Chadema) wakiwa wamevaa viroba (magunia) vyenye ujumbe tofauti.

Katika Kituo cha Daladala cha Mbezi, baadhi ya wanawake waliibuka kwenye maandamano ya wakiwa wamevaa viroba (magunia) vyenye ujumbe tofauti.

Wanawake hao wanaofanya biashara ya kuokota chupa za plastiki, wamesema wamebuni vazi hilo wakilenga kufikisha ujumbe kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.

“Tumevaa hivi kwa kuwa kitu rahisi kukipata kwa sasa ni kiroba, maisha yamekuwa juu na familia nyingi zinateseka, tukiwamo sisi,” amesema mmoja wa wanawake hao.

Hata hivyo, wanawake hao kwa nyakati tofauti, wamesema wao sio wanachama wala wafuasi wa Chadema, lakini wanashiriki maandamano hayo kama wananchi wa kawaida kutokana na kuvutiwa na ajenda za Chadema kwenye maandamano hayo.


Chalamila aibukia Mbezi

Mapema leo Januari 24, 2024 asubuhi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amekutana na wafuasi Chadema wanaojiandaa kuandamana na kuwapa salamu za kubariki maandamano hayo akidai ni za Rais Samia.

Chalamila alikuwa anaongoza shughuli za usafi katika eneo la Mbezi Luis, ambako pia maandamano yameanzia.

Chalamaila ambaye awali alitangaza jana Jumanne na leo Jumatano kuwa siku ya askari wa vyombo vya dola kufanya usafi, amewataka wafuasi na wanachama wa Chadema waendelee kuandamana na kufikisha ujumbe wao.

Pia, amesema wakati Chadema wakiendekea na maandamano, yeye na watu wake (ambao si askari) wameendelea na usafi huku akisisitiza kuwa Rais Samia ameyabariki maandamano hayo na kuwa kila mmoja anapaswa kulinda amani.

“Nawapa salamu za Rais, ninyi endeleeni kuandamana na sisi tunaendelea na usafi,” amesema Chalamila huku akishangiliwa na wafuasi na wanachama wa chama hicho waliokuwa wakiimba, kucheza na kupiga makofi huku baadhi ya nyimbo zikimtaja Rais Samia na nyingine “sukari bei juu”.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila akiwa amebeba taka wakati wa kushiriki usafi katika eneo la Mbezi Malamba Mawili leo Jumatano Januari 24, 2024 

Mbowe na wanawe

Mbowe ametumia maandamano hayo kujibu kwa vitendo kauli za wakosoaji wake waliotaka viongozi watangulize familia zao kwenye maandamano.

Mwanasiasa huyo leo ameambatana na watoto wake watatu ambao walipozungumza wote walikuwa na ujumbe unaofanana kwamba “wanawapenda Watanzania” huku Mbowe akitoa ujumbe kwamba maandamano hayo hayatakoma na yatasambaa nchi nzima.

“Tunataka miswada iondolewe bungeni na tupate mwafaka wa kitaifa ili miswada hiyo itakaporejeshwa bungeni itibu matatizo yaliyosababisha uvunjifu mkubwa wa haki mwaka 2020 na chaguzi zote za marudio zilizowahi kufanyika,” amesema Mbowe.

Mbali na kuambatana na watoto wake, Mbowe aliambatana na viongozi wengine wa Chadema waliotoka mikoa ya Mbeya na Kilimanjaro kwa ajili ya kushiriki maandamano hayo huku wakieleza kwamba wanasubiri maelekezo ya kufanya maandamano katika mikoa yao.

Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema amesema ameambatana na watu kadhaa akiwemo mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Grace Kiwelu, wajumbe wa kamati ya utendaji ya mkoa huo na wilaya zake.

Alisema kwa takwimu za awali waliosafiri usiku ambao tayari walikuwa wamewasili Dar es Salaam alfajiri ya jana ni zaidi ya watu 60.

Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Mbeya, Joseph Mwasote alisema wamejumuika pamoja ili kufikisha ujumbe waliokusudia kwa watawala.

Mwasote alisema jambo hilo ni la Watanzania wote, hivyo wameamua kushiriki na wenzao wa Dar es Salaam na wakirejea Mbeya watapanga ratiba ya lini watafanya maandamano.


Walivyofika ofisi za UN

Saa 9:30 alasiri, viongozi wakuu wa Chadema wakiambatana na wanachama wao, walifika kwenye Ofisi za UN zilizopo Barabara ya Sam Nujoma. Viongozi waliingia katika ofisi hizo zilizopo hapa nchini kuwasilisha ujumbe wenye mapendekezo ya chama hicho.

Walioingia ndani huku wafuasi wengine wakibakia nje ya ofisi hizo na mabango yao, ni Mwenyekiti Mbowe, Makamu wake Bara, Lissu, Katibu Mkuu, John Mnyika na Kaimu Mwenyekiti Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Sharifa Ally Suleiman.

Katika ofisi hizo, waliingia kwa kusindikizwa na Muliro.

Nje ya ofisi, makada wa Chadema na viongozi wengine walioshiriki maandamano hayo wakiwemo wajumbe wa kamati kuu, Godbless Lema, John Heche na Mchungaji Peter Msigwa waliendelea kuimba nyimbo mbalimbali.

Mbowe, Kigaila, Lema watinga Buguruni maandamano Chadema

Demokrasia imekua

Wakizungumzia maandamano hayo, wadau wa demokrasia nchini wamesema ni ishara ya kukua kwa demokrasia nchini na ujumbe uliokusudiwa na Chadema umefika.

Mwanasheria mkongwe, Dk Hellen Kijo Bisimba amesema maandamano hayo yamekuwa na mafanikio kwa sababu walilenga kuionyesha dunia kuhusu malalamiko waliyonayo kupitia maandamano.

“Wamefanya tathmini yao baada ya kupeleka malalamiko yao serikalini hawakufanikiwa, bungeni nako ndiyo hivyo na hata wangepeleka kwa Rais naye ni mwenyekiti wa CCM.

“Umoja wa Mataifa ni sehemu nzuri kupeleka malalamiko kwa sababu Tanzania ni mwanachama,” amesema Bisimba.

Alipoulizwa kuhusu nguvu ya Umoja wa Mataifa kuibana Tanzania kutekeleza madai ya Chadema, Dk Bisimba alisema, “ni kweli hawana fimbo ya kuichapa Tanzania, lakini wanaweza kurudisha mazungumzo ya pande mbili mwafaka upatikane.”

“Kikubwa ni kwamba Chadema wamejitokeza na wameeleza dukuduku lao na dunia nzima imeona.”

Dk Bisimba aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ameongeza kuwa maandamano hayo yamefanikiwa kwa sababu Rais aliyeko madarakani ameruhusu, tofauti na awamu iliyopita.

“Pamoja na kwamba haitakiwi kila jambo liamuliwe na mtu mmoja, lakini kama Rais asingetaka waandamane, wasingeandamana kwa hiyo tunampongeza,” alisema.

Kwa upande wake, Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), John Seka, licha ya kusema yamefanikiwa na kukusanya watu wengi, amesema muhimu ni ujumbe uliokusudiwa kupokelewa na kufanyiwa kazi.

“Nafikiri ni mapema mno kusema kuwa maandamano yamefanikiwa, kabla ujumbe huo haujapokelewa na kufanyiwa kazi.

“Lakini kwa mwitikio umekuwa mkubwa na hata Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ameunga mkono, Polisi wameonekana wakiyalinda na vyombo vya habari vya ndani na nje vimeonyesha dunia, oganaizesheni imekuwa nzuri,” alisema.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia Dar es Salaam, Denis Konga amesema Chadema imefanikiwa kufikisha ujumbe wake kwenye chombo huru kinachoweza kuiambia Serikali.

“Mashirika ya kimataifa yana uwezo wa kuisema Serikali, kwa hiyo Chadema wakifikisha huko, nadhani kwa kuunganisha lile Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu la mwaka 1948, watakuwa wamefanya kitu,” amesema.

Ameongeza, “Kuruhusiwa tu kuandamana ni kuonyesha kuwa tumekuw=a kidemokrasia, mimi binafsi sikutarajia na hasa niliposikia kwamba wanajeshi watafanya usafi, kile kilikuwa ni kitisho.”

Amesema hata kama Umoja wa Mataifa hautafanyie kazi malalamiko yao, lakini ujumbe umefika na itajulikana kuna sehemu ya Watanzania wana mawazo tofauti na ya Serikali.

“Kama maandamano yasingefanyika, kungekuwa na ujumbe kwamba Watanzania wanakubaliana na hali iliyopo, lakini kwa kuandamana hata wangekuwa wachache na kufikisha ujumbe ni jambo kubwa na tupongeze ukuaji wa demokrasia yetu,” amesema.

Akizungumzia maandamano hayo, mwanahabari na kada wa Chadema, Ansbert Ngurumo amesema chama hicho kimedhihirisha ukubwa wake katika organazesheni na uhamasishaji.

"Mtaji wa kwanza ni wanachama. Kama huna wanachama huwezi kuandaa maandamano na Mbowe amedhihirisha umwamba wake.

“Ameunganisha jumuiya ya kimataifa na Chadema, Serikali ikashtukia haina chaguo lililo salama kuliko kutuma polisi wayalinde maandamano," amesema Ngurumo anayeishi nchini Finland.

Chadema Kilimanjaro wanogesha maandamano Dar, Katibu wa mkoa, Basil Lema afunguka kila kitu

Kwa upande mwingine, Katibu wa Itikadi Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda akiwa ziarani mkoani Arusha amesema zama za kuzuia maandamano ya wapinzani zimepita, wanaachwa waandamane lakini hawatapa kura za wananchi.

Makonda ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wananchi wa Makuyuni wilayani Monduli mkoa wa Arusha, akielekea Manyara, akisisitiza kuwa CCM imejikita kutatua kero za wananchi.

“Walitegemea leo wakiandamana wale kaka zangu kina Mbowe (Freeman) na Lissu (Tundu) kuwa tutawapelekea polisi wa kuwapiga mabomu, nawaambia kaka zangu staili zimebadilika, awamu hii tutawapa kila wanachotaka, lakini wananchi hawatawapa kura,” amesema Makonda.

Amesema Rais Samia ni mwanamama shupavu na jasiri aliyetoa kila aina ya picha katika uongozi wake katika kuhakikisha anajenga demokrasia inayotoa haki bila kuwabagua watu.


Imeandikwa na Victor Tullo, Imani Makongoro, Juma Issihaka, Nasra Abdallah, Pamela Chilongola, George Helahela, Elias Msuya na Baraka Loshilaa.