Mabadiliko katika tamaduni za Kinyakyusa

Wednesday January 05 2022
wanyakyusa pc
By William Shao

Katika toleo lililopita tuliona utamaduni wa kabila la Kinyakyusa ulivyo katika kuwalea watoto wao na kuwaandaa kuwa watu wazima baadaye maishani mwao.

Katika utaratibu huo, watoto wa kiume wenye umri wa miaka 12 na hata 13 walikuwa wakipelekwa jandoni. Lakini kutokana na hali za maisha na mchanganyiko wa tamaduni za makabila mbalimbali, utaratibu huo umebadilika kutokana na sababu kadhaa. Sababu kubwa zaidi ni watoto kumaliza shule za awali wakiwa na umri wa kati ya miaka 12 na 16.

Leo tutajaribu kuangazia heshima ya wanawake katika kabila la Wanyakyusa. Kabla ya ujio wa wakoloni Tanzania, mwanamke alikuwa na hadhi yake katika jamii ya Wanyakyusa kama ambavyo wanaume nao walikuwa na hadhi yao.

Katika jamii za Kinyakyusa, wanawake walithaminiwa sana kwa sababu mbalimbali, lakini moja kubwa ni kwa vile wao ndiyo waliziunganisha koo mbalimbali za Wanyakyusa na ndio wao waliongeza mali ya familia kwa kuleta mahari nyingi wakati wa kuolewa na pia kuzisaidia familia zao huko walikotoka hata baada ya kuolewa.

Hata hivyo, mahari haikuwa na maana ya kumnunua mwanamke kama mali. Wengi ambao siku hizi wanasoma habari zinazohusu mahari kwa Wanyakyusa wanachukulia kwamba mahari ilikuwa ni kubadilisha mali na mwanadamu kana kwamba ni kumnunua. Lakini utaratibu huo wa mahari ulitumika kujenga uhusiano kati ya famila za pande zote mbili za waliooana.

Kwa utamaduni wa Wanyakyusa, mwanamke aliyeolewa alikuwa na thamani kubwa kuliko mwanamke aliyefikia umri wa kuolewa lakini hajaolewa. Ziko nyimbo kadhaa zilizowasifia wanawake walioolewa.

Advertisement

Katika jamii nyingi za Tanzania mwanamke au mwanamume akifikia hatua ya kuitwa mtu mzima, huwa anapewa mafundisho ya namna ya kuishi kama mume na kuishi kama mke ili kuhimiza mila na desturi za jamii hiyo.

Ili mtoto katika jamii ya Kinyakyusa aonekane amekua, alipaswa kupitia mafunzo ya kijamii katika jamii hiyo. Mwanamume alikwenda jandoni na mwanamke alikwenda unyagoni. Jando na unyago ilikuwa ni sehemu nzuri na bora ya kufundishia vijana kuingia katika hatua nyingine ya kimaisha.Mabadiliko

Hata hivyo, mambo yote hayo yamebadilika na badala yake yamekuja mambo kama “bag party” kwa wanaume na unyago ni kama umechukuliwa na kile kinachoitwa “kitchen party” ambavyo vinadaiwa kama vinawafundisha vijana wanapokuwa wanajiandaa kufunga ndoa. Haya mambo mapya ni tofauti na jando na unyago ambavyo viliwaandaa vijana hata kama hafungi ndoa wakati huo.

Hata muda uliokuwa unatumika kuwafundishia vijana hawa ulikuwa ni muda mrefu na katika eneo lililojitenga, wakati hizi za sasa zinawafundisha ukumbini kwenye watu wengi.

Ulipoanza kuingia utamaduni mpya, jando na unyago vilianza kukosolewa na kuonekana kama ni chanzo kikubwa cha matatizo katika jamii kama magonjwa ya zinaa na mimba za utotoni.

Katika makabila mengi ya Kiafrika katika jamii za awali, waliamini kuwa ndoa za wake wengi (mitala) lilikuwa ni jambo la kawaida kabisa, hususan kwenye kabila la Wanyakyusa.

Jambo hilo lilisukumwa na sababu nyingi, na mojawapo ya hizo ni haja ya mwanamume kupata watoto iwapo itatokea mmoja wa wake wa mwanamume huyo ndiye kikwazo kikubwa katika upatikanaji wa watoto.

Lakini sababu nyingine ni mahitaji yake ya kuridhisha tamaa za kimwili ili kuepuka makatazo ya kitamaduni kama vile kutofanya ngono mwanamke anapokuwa ananyonyesha. Sababu nyingine ambayo si dhahiri ni kwa mwanamke wa awali kuwa mzee, mgonjwa au kutovutia. Hata hivyo, sababu iliyozungumzwa zaidi ni kwamba kuoa wake wengi ilikuwa ni sifa kwa mwanamume.

Kutokana na baadhi au sababu zote zilizotajwa hapo juu, suala la mitala katika jamii za awali lilionekana la maana sana kwa sababu mwanamume mwenye mitala alionekana kuwa ni mwenye uwezo na akili kiasi kwamba mtu yeyote anaweza kwenda kupata ushauri wa masuala ya ndoa kutoka kwake.

Katika mfumo wa ndoa za mitala, mwanamume aliyetaka kuoa mwanamke mwingine alilazimika kuchangia asilimia 80 ya gharama zote za mahari.

Katika tasnifu yake alipochunguza mabadiliko ya tondozi za Wanyakyusa katika awamu za kihistoria kwa ajili ya kutimiza masharti ya kutunukiwa shahada ya uzamivu ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Rose Ssekile anaandika hivi:

“Wanaume na wanawake walipimwa kwa kigezo cha bidii katika ufanyakazi ili aweze kumudu maisha vizuri. Katika jamii asilia ya Kinyakyusa wazazi waliwajibika kumtafutia mtoto wao mke kwa sababu mke ndiyo msingi mkubwa wa familia. Mwanamke alithaminiwa kwa uwezo wake wa kuzaa, ugumba ulikuwa ni laana katika jamii.”

Baadhi ya watafiti waliofuatilia historia ya mila na tamaduni za Mwafrika wameandika kuwa katika jamii ya Kiafrika mwanamke aliheshimiwa tu kama amezaa watoto. Mwanamke asiyezaa, au asiye na watoto, huonekana hajakamilika.

Kwa upande mwingine, mwanamume alithaminiwa kutokana na uwezo wake wa kuwa na watoto wengi. Kwa upande wa watoto katika mila na desturi za Kinyakyusa, kila mtoto ana thamani yake katika jamii ya Wanyakyusa.

Kila mmoja alikuwa akimtegemea mwingine kwa namna fulani. Watoto wa kike walithaminiwa sana kwa sababu mahari iliyokuwa inatolewa kwa ajili yake ingeweza kutumiwa pia kutolea mahari kwenda kwenye familia ambayo mtoto wa kiume atakwenda kuoa.

Mwelekeo wa jamii ya Kinyakyusa kuhusu ndoa, kama zilivyo jamii nyingine nyingi za Kiafrika, umekumbwa na mabadiliko makubwa kwa sababu awali kijana alitakiwa kuoa katika jamii au kabila la Kinyakyusa na hata wakati mwingine kwenye koo zilizopo katika maeneo yao.

Kijana alikuwa anatafutiwa mchumba na wazazi wake, jambo ambalo kwa sasa halipo, na kama lipo, ni kwa uchache sana, na isitoshe, ndoa zimevuka mipaka kiasi kwamba mtu anaweza kuoa kabila tofauti na kabila lake, na wengi wamekuwa wakioana bila hata kujuana kwa undani.

Itaendelea kesho kumalizia simulizi kuhusu Wanyakyusa

Advertisement