Mabala: Sheria ikifuatwa shule nyingi zitafungwa

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mwandishi wa vitabu, Richard Mabala amesema karibu nusu ya shule za Serikali zinaweza kufungwa endapo mfumo wa elimu utafuata sheria

Dar es Salaam. Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mwandishi wa vitabu, Richard Mabala amesema karibia nusu ya shule za Serikali zitafungwa ikiwa sheria ya utoaji wa elimu ya wizara ya elimu itafuatwa ipasavyo.

Kwamba pamoja na jitihada za hivi karibuni za Serikali kuboresha miundombinu ikiwamo kujenga madarasa, kujenga shule mpya jambo ambalo alipongeza lakini alihoji kuwa shule hizo zina sifa za kuwa shule?

Ameyasema hayo leo wakati akichokoza mada katika kongamano la Sekta ya elimu lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru.

Mabala amesema Sheria ya wizara ya elimu inabainisha kuwa darasa moja halipaswi kuwa na wanafunzi zaidi ya 40 hadi 45 lakini kwa shule za serikali ni tofauti.

“Wakaguzi wanasisitiza hilo na kwenda shule binafsi, je wanakagua shule zao wenyewe na kuhakikisha wanafuata sheria zao, chakula kinapaswa kuwepo, idadi ya vitabu na kila kitu kimetajwa,”

 “Ukifuata hizi sheria utafunga nusu ya shule kwa sababu hazina sifa ya kuwa shule kulingana na sera ya wizara ya elimu yenyewe,” amesema.

 Amesema pia ufikiaji wa elimu hutegemeana na elimu inatolewaje huku akibainisha kuwa kama mtu analazimika kujifunza masomo yote katika lugha ambayo huielewi basi hapati elimu.

Amesema mwaka 1982 wakati shule za sekondari ni chache, watu walichujwa sana kwenda sekondari, waingereza walifanya utafiti na kubaini kuwa asilimia 10 pekee ya watu wa kidato cha nne ndiyo walikuwa wamevuka kiingereza cha kidato cha kwanza.

“Kama ni hivyo watafanyaje mitihani,shirika langu tulifanya utafiti mwaka 2012 kwa shule 16  za sekondari tuliwapa kiingereza kama Juma is a boy, Juma likes playing football, Juma plays football on Saturday, When does Juma play football, robo tu waliweza kujibu hili swali,”

“Kama asilimia 75 walishindwa kujibu hili swali watawezaje kusoma historia, ufikiaji wa elimu hutegemea lugha ya kujifunzia,” amesema Mabala