Mabilioni yamwagwa kumaliza shida ya maji Same
Muktasari:
- Wizara ya Maji itatumia Sh247 milioni kumaliza tatizo la maji katika kata ya Kihurio Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.
Same. Wizara ya Maji itatumia Sh247 milioni kumaliza tatizo la maji katika kata ya Kihurio Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Julai 7, 2021 na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso wakati akisikiliza kero za wananchi wa jimbo la Same Mashariki.
"Dhamana niliyopewa na Serikali yangu ya kusimamia wizara hii ya maji kuhakikisha tunatatua changamoto ya maji kwenye maeneo ya wananchi ili na nyinyi wananchi wa Kihurio mpate maji safi na salama.”
"Kero zenu nimezisikia, tutatoa fedha hizi Sh247 milioni na tutazileta mapema, niombe fedha hizi zikija wahandisi wa mradi huu mhakikishe mnafanya kazi usiku na mchana ili mkamilishe mradi huu na nitarudi hapa kujiridhisha kuwa mradi huu umekamilika ili wananchi hawa waweze kuondokana na changamoto hii ya maji," amesema Aweso
Huku akiwa makini amesema, “nataka niwatie moyo wananchi wa Kihurio bajeti ambayo tumeipitisha wizara yangu ni Sh680 bilioni na tukaongezewa Sh207 bilioni ili kutatua changamoto ya maji nchini, fedha hizi sio za kuchezea mmeteseka vya kutosha kwa muda mrefu na nataka changamoto hii ya maji iishe.”
Mbunge wa jimbo hilo, Anna Kilango amesema kwa muda mrefu kata hiyo inakabiliwa na changamoto ya maji na kuishukuru Serikali kwa kutenga zaidi ya Sh1.2 bilioni kwa ajili ya kumaliza changamoto ya maji Wilaya ya Same.
"Jimbo hili lina changamoto ya maji kwa muda mrefu, namshukuru waziri kufika hapa Kihurio kusikiliza kero za wananchi , naishukuru Serikali kwa kuhakikisha Same inatengewa bajeti nzuri kumaliza changamoto ya maji," amesema Kilango.