Prime
Macho na masikio kwa Tume ya Uchunguzi Matukio Oktoba 29
Dar es Salaam. Wakati leo Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani ya Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 ikitarajia kuwasilisha taarifa yake ya uchunguzi, macho na masikio ya wadau yameelekezwa kwa Tume hiyo kujua kilichobainika.
Ripoti hiyo, inatarajiwa kutoa majibu ya maswali ya wananchi yatakayotoa mwanga juu ya matukio yote yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi, inatarajiwa kukabidhiwa rasmi kwa Rais Samia Suluhu Hassan, leo au siku yoyote baada ya kutimiza muda wa siku 132 ilizopewa na mamlaka yake ya uteuzi.
Novemba 14, 2025, wakati akifungua kikao cha 13 cha Bunge la Tanzania, Rais Samia alitangaza nia ya kuunda tume hiyo na baadaye, Novemba 18, 2025 aliitangaza rasmi Tume hiyo iliyopewa jukumu la kuchunguza chanzo na athari za vurugu zilizotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Katika kipindi hicho, baadhi ya watu walipoteza maisha wengine kupata ulemavu pamoja na mali za umma na binafsi kuharibika kufuatia maandamano ya vijana yaliyozua vurugu.
“Serikali imechukua hatua ya kuunda Tume ya kwenda kuchunguza ili tujue kiini cha tatizo na taarifa itakayotolewa na Tume hiyo itatuongoza katika mazungumzo ya kuleta amani na maelewano nchini,” alisema Rais Samia.
Rais Samia alisema ripoti ya Tume hiyo itawezesha kuanza kwa maridhiano pamoja na mchakato wa kupata Katiba mpya.
Mamia ya vijana walikamatwa na kufunguliwa kesi za uhaini Mahakama mbalimbali nchini. Hata hivyo, Rais Samia alitangaza msamaha kwa baadhi yao akieleza kuwa walifuata mkumbo na walifutiwa kesi na kurudi uraiani huku wengine wakiendelea na kesi zao.
Tume hiyo aliyopewa miezi mitatu kufanya kazi, ilikuwa na wajumbe tisa wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Jaji Mkuu mstaafu, Othman Chande, huku wajumbe wengine wakiwa ni Jaji Mkuu mstaafu, Profesa Ibrahim Juma, Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue.
Wengine ni, Balozi Radhia Msuya na Luteni Jenerali Paul Meela ambaye ni Mwanadiplomasia na Balozi mstaafu.
Pia wamo, Said Mwema (Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu), Balozi David Kapya (Mwanadiplomasia na Balozi mstaafu) na Dk Stergomena Tax, aliyewahi kuwa Waziri wa Ulinzi, na pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Aidha, Novemba 20, 2025, Rais Samia alizindua tume hiyo akiipa majukumu kuangalia maeneo saba ikiwemo kuchunguza chanzo cha kadhia na sababu halisi zilizoibua vurugu, kutathmini madai ya vijana walioingia barabarani na kubaini walikuwa wanadai haki gani, kuchambua matamshi ya vyama vya upinzani, ikiwemo kauli za uchochezi zinazodaiwa kutolewa kabla ya uchaguzi.
Pia, kuangalia uhusiano kati ya vyama vya siasa na Tume Huru ya Uchaguzi, kuchunguza mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) ya ndani na nje katika matukio ya Oktoba 29, 2025, kutathmini kama kulikuwa na njia mbadala zaidi ya maandamano, uvunjifu wa amani, na vitendo vya uchomaji, ili kushughulikia changamoto kati ya tume, vyama vya siasa, na Serikali pamoja na kuangalia hatua zilizochukuliwa na vyombo vya dola kukabiliana na vurugu, na kama zilikuwa sahihi au zilikithiri.
Tume hiyo ilianza majukumu huku vyama vikuu vya upinzani vikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ACT Wazalendo na baadhi ya wadau vilipinga uteuzi wa tume hiyo wakiibua utata katika uteuzi wake na aina ya wajumbe walioteuliwa. Hao inaelezwa hawakuenda kutoa maoni yao.
Katika utata mwingine dhidi ya Tume hiyo, Novemba 27, 2025 shauri la madai mchanganyiko kupinga uhalali wa Tume hiyo lilifunguliwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo, Dar es Salaam na mwanaharakati Rose Mwakitwange na mawakili wa Mahakama Kuu na Mahakama za chini, Edward Heche na Deogratius Mahinyila.
Katika shauri hilo ambalo Desemba 18, 2025 Mahakama Kuu ilihalalisha Tume hiyo kupingwa mahakamani, Machi 13, 2026, Mahakama Kuu ilitupilia mbali shauri hilo, ikieleza Rais Samia alitumia mamlaka aliyonayo kisheria chini ya Kifungu cha 3 cha Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32, na kwamba hakuvunja mamlaka yake ya kisheria kuiteua.
Tume ilivyofanya kazi
Katika kujibu tuhuma na hofu hiyo ya jamii, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mkuu mstaafu, Chande akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam baada ya Tume hiyo kuanza kazi zake alisisitiza utendaji wa Tume hiyo utapimwa kitaifa na kimataifa, hivyo imejikita kuangalia Watanzania wanataka nini katika uchunguzi wake.
Ilizunguka mikoani na kukutana na wadau mbalimbali mahususi wakiwamo waathirika na vyombo vya habari viliruhusiwa kuingia na kuripoti kile kilichokuwa kikielezwa.
Hata hivyo, Januari 24, 2026, Tume hiyo ikiwa Wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam, ilitangaza kutoruhusu waandishi wa habari kuingia ukumbi wakati ushahidi unapotolewa, Jaji Mkuu mstaafu Profesa Ibrahim Juma, akieleza uamuzi huo ulilenga kulinda faragha ya mashahidi, hatua iliyoibua mjadala miongoni mwa wananchi wakihofia juu ya usiri ndani ya tume hiyo.
Baada ya muda wa siku 90 kutimia Februari 20, 2026, Rais Samia aliiongezea muda wa siku 42 ikipewa nafasi zaidi hadi leo Ijumaa Aprili 3, 2026 ili kuipa nafasi ya kukamilisha uchunguzi wake kikamilifu.
Juzi Jumatano, Aprili 1, 2026, Ikulu ya Dar es Salaam, Rais Samia alikutana na waliokuwa wagombea urais 16 katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 kujadili kuhusu namna ya kuimarisha maridhiano ya kisiasa, demokrasia ya vyama, amani na mshikamano wa kitaifa.
Taarifa ya kikao hicho, imetolewa na kutiwa saini na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Shaaban Kissu ilieleza wanasiasa hao, walitumia nafasi hiyo kuwasilisha maoni yao kuhusu namna ya kuimarisha maridhiano ya kisiasa, demokrasia ya vyama, amani na mshikamano wa kitaifa baada ya uchaguzi mkuu.
Pia, wametoa maoni kuhusu namna ya kuimarisha ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo na kudumisha tunu za umoja wa kitaifa.
Mashaka na matumaini
Wadau wamezungumzia kinachosubiriwa kutoka katia kile kilichobainika kwenye uchunguzi uliofanywa na Tume hiyo wakiwa na hisia mgawanyiko juu ya namna ripoti hiyo itakavyobeba ukweli na kujibu wasiwasi uliopo kwenye jamii.
Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam, (UDSM), Dk Richard Mbunda, anasema kutokana na hali iliyopo katika jamii tangu mwanzo wa tukio hilo na kuundwa kwa Tume hiyo, kinachosubiriwa ni namna taarifa ya Tume hiyo itakavyojibu maswali yaliyopo katika jamii.
“Kinachosubiriwa hapa ni ikiwa ripoti hiyo itakwenda kuthibitisha wasiwasi uliopo kwa baadhi ya wadau au kufuta hofu hizo. Hii ni kutokana na wasiwasi ulioibuliwa juu ya aina ya wajumbe walioteuliwa na namna Tume ilivyofanya kazi ikianza kwa kuwasikiliza wadau waziwazi mbele ya vyombo vya habari na baadaye kuvizuia vyombo hivyo,” anasema.
Anafafanua kuwa hali hiyo ilifanya baadhi ya watu kuingiwa wasiwasi wa kufichwa kwa baadhi ya taarifa za ukweli. Kusikilizwa kwa mashuhuda mbele ya vyombo vya habari kuliwapa nafasi wananchi kusikia taarifa walizokuwa wanazifahamu jambo ambalo lingewaongezea imani ya kujua ukweli.
“Kikubwa hapa ni namna ripoti pia itakavyowasilishwa, kama itatolewa kwa uwazi mbele ya Rais isomwe watu wajue kilichoibuliwa au kama itawasilishwa kimyakimya kwa Rais halafu yeye ndiye aamue kusema yaliyomo au la, hayo ndiyo mambo yatakayofanya jamii iwe upande gani katika kuiamini ripoti hiyo,” anaongeza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Anna Henga anabainisha Tume hiyo inasubiriwa kuwasilisha matokeo ya uchunguzi wake kwa mashaka akibainisha ripoti hiyo inahofiwa kuathiriwa na uhuru wa Tume hiyo, hivyo kushindwa kutoa majibu halisi kwa kuwa baadhi ya watuhumiwa wa matatizo yaliyotokea wanaweza kuwa sehemu ya wenye mamlaka ambao wana masilahi sawa na walioteuliwa kuongoza uchunguzi huo.
“Tunaisubiri ripoti hiyo kwa mashaka tukihofia inaweza kutoa majibu ya kung’ata na kupuliza, lakini kwa kuwa mambo mengi yamesimama kwa kisingizio cha kukamilika kwa uchunguzi huo ikitoka itawezesha hatua nyingine muhimu za kitaifa kuendelea,” anasema.
Kwa upande wa waliokuwa wagombea wa urais katika uchaguzi huo, Doyo Hassan Doyo, aliyegombea urais kupitia Chama cha NLD anasema wao wanatarajia kusikia ukweli wa kilichotokea ili kuondoa hisia iliyopo kwenye jamii.
“Kwa mtazamo wangu kwa niaba ya wagombea tulioshiriki uchaguzi huo, tunategemea ripoti ya Tume itaweka wazi kile kilichotokea kijulikane, kama ambavyo wadau wamekuwa wakihitaji chombo huru cha kuchunguza yaliyojiri, basi matarajio yetu kwa Tume ni kuona inafichua ukweli wa kilichotokea katika uchaguzi huo,” anasema.
Mmoja wa viongozi waandamizi serikalini aliyeomba hifadhi ya jina lake anasema: “Hii ripoti ni kama mwiba, kwa sababu bila kusema ukweli haitaaminika na wala maridhiano hayawezi kuwepo na wajumbe wenyewe watakuwa wamejishushia heshima.”
“Tuliambiwa na Jaji Chande tuiamini na tusubiri ripoti, muda umefika, wakiichakachua wananchi wanajua kilichotokea, wapo walioona mashuhuda wakitoa ushahidi wao, sasa wakituletea yasiyoeleweka wanampa wakati mgumu tu mama,” anasema.