Madai ya mateso yaibua kesi ndogo
Washtakiwa wa kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini kutoka Mererani Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Erasto Msuya wakielekea katika chumba cha Mahakama Kuu Kanda ya Moshi chini ya ulinzi wa askari kanzu jana. Picha na Dionis Nyato
Muktasari:
Hoja hiyo iliibuliwa na wakili John Lundu anayemtetea mshtakiwa baada ya shahidi wa 10 wa upande wa mashtaka, Sajini Atway Omar alipoiomba mahakama ipokee maelezo hayo kama kielelezo.
Moshi. Hoja ya mshtakiwa wa saba katika kesi ya mauaji ya bilionea Erasto Msuya, Ally Majeshi kuwa alitoa maelezo ya kukiri kosa baada ya kuteswa na polisi, jana iliibua kesi ndogo ndani ya kesi.
Hoja hiyo iliibuliwa na wakili John Lundu anayemtetea mshtakiwa baada ya shahidi wa 10 wa upande wa mashtaka, Sajini Atway Omar alipoiomba mahakama ipokee maelezo hayo kama kielelezo.
Katika hoja yake, wakili Lundu alisema mteja wake amemweleza baada ya kukamatwa na kupelekwa mahabusu, alikaa ndani kwa dakika 10 tu kisha kutolewa.
“Baada ya kutolewa mahabusu kilichoendelea ni mateso na kupigwa ambayo yalichukuwa muda mrefu. Alipotolewa alipelekwa chumba cha mateso na hakujua kilichoendelea,” alidai.
Aliendelea kuwa mteja wake alipigwa ili kukiri kushiriki mauaji ya bilionea Msuya ilhali hajui chochote na kwamba, maelezo ya kukiri yaliandaliwa na polisi lakini yeye hakuhiari kuyatoa.
Kutokana na hoja hiyo, wakili mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavula alidai linapojitokeza suala la kama maelezo yalitolewa kwa hiari au la, mahakama lazima iende kwenye kesi ndani ya kesi.
Jaji Salma Maghimbi alikubaliana na msimamo huo wa kisheria na kuahirisha kesi hiyo kwa dakika 10 kila upande ujiandae, ili kupima kama mshtakiwa aliteswa au la.
Baada ya muda huo, upande wa mashtaka ulimwita Sajini Atway kutoa ushahidi wake akiongozwa na wakili wa Serikali, Kassim Nassir.
Mahojiano hayo yalianza kwa Wakili Nassir kutaka kujua shahidi alikuwa wapi Oktoba 5, 2013 na kujibiwa kuwa alikuwa Kigoma kwa kazi ya kumkamata Ally Majeshi anayetuhumiwa kwa mauaji ya Erasto Msuya na kwamba alikuwa na Samwel, ambaye ni shahidi wa tisa, na mpelelezi anayeitwa Seleman.
Alisema siku hiyo waliamka saa 10:00 alfajiri na kuelekea stendi, wakiwa wamevalia kiraia na kutumia gari aina ya Toyota Land Cruiser na walipofika walianza kumsaka kumtafuta mshtakiwa Ally Majeshi, ambaye hakuwa akimfahamu kabla.
Wakili Nassir: Mkiwa hapo nini kilitokea?
Shahidi: Afande Samwel alimuona Ally Majeshi kwa sababu kulishaanza kupambazuka.
Wakili Nassir: Alimuona akiwa umbali gani?
Shahidi: Kama mita 20 na ili kuthibitisha ni yeye, afande Samwel alitoa simu yake na kumpigia.
Wakili Nassir: Ikawaje baada ya afande Samwel kumpigia?
Shahidi: Mshtakiwa alitoa simu yake na kuipokea lakini afande Samwel akaikata baada ya kuthibitisha ni yeye.
Wakili Nassir: Baada ya kuthibitisha ni yeye, afande Samwel alitoa maelekezo gani?
Shahidi: Tulishuka kwenda kuwakamata.
Wakili Nassir: Ebu tueleze mlivyowakamata.
Shahidi: Afande Samwel alikuwa mbele aliwahi kumkamata Ally Majeshi na mimi nikamkamata kijana mwingine aliyekuwa naye.
Wakili Nassir: Ebu tueleze mlivyowakamata.
Shahidi: Kwanza alitaharuki na afande Samwel akajitambulisha na kumweleza dhima nzima ya kumkamata.
Wakili Nassir: Unasema alimweleza dhima nzima ya kumkamata, ni kitu gani alimweleza?
Shahidi: Alimwambia anahusika na mauaji ya Erasto Msuya na akakubali, ndiyo. Akamwambia nataka twende wote kituoni.
Shahidi huyo alisema watu waliokuwa stendi walitaharuki, lakini Koplo Samweli aliwaeleza kuwa wamemkamata kwa sababu ya mauaji na baadaye wakapanda gari kwenda Kituo cha Polisi Kigoma ambako mtuhumiwa aliwekwa mahabusu na Samwel akaenda kwa mkuu wa upelelezi wa mkoa.
Alisema mtuhumiwa alikuwa katika hali nzuri wakati akiingia mahabusu na ilichukua dakika 30 kabla ya Koplo Samweli kurudi na kumuagiza aandike maelezo ya mtuhumiwa ambayo alichukulia kwenye chumba alichoomba kituoni hapo.
Wakili Nassir: Hicho chumba ulichoonyeshwa kulikuwa na mtu?
Shahidi: Hapana.
Wakili Nassir: Baada ya kukabidhiwa chumba ulifanyaje?
Shahidi: Nilimuomba incharge anitolee mshtakiwa mahabusu.
Wakili Nassir: Ikawaje?
Shahidi: Mshtakiwa alitolewa nikaenda naye hadi chumba cha mahojiano.
Wakili Nassir: Wakati anatolewa mahabusu alikuwa katika hali gani?
Shahidi: Alikuwa katika hali nzuri na alikuwa akitembea mwenyewe.
Wakili Nassir: Wewe ulijitambulisha kwake?
Shahidi: Nilijitambulisha kuwa ni koplo Atway (wakati huo) nataka kuchukua maelezo kuhusiana na mauaji ya Erasto Msuya.
Wakili Nassir: Ikawaje baada ya kujitambulisha.
Shahidi: Alikubali kuwa atatoa maelezo na nikamsomea onyo.
Wakili Nassir: Ulimpa onyo gani?
Shahidi: Nilimweleza kuwa maelezo yake yanaweza kutumika mahakamani kama ushahidi.
Wakili Nassir: Ulimpa haki gani?
Shahidi: Nilimweleza anaweza kuwa na ndugu, jamaa au wakili wa kumshuhudia maelezo yake, lakini akasema atatoa maelezo mwenyewe.
Wakili Nassir: Baada ya kumaliza mahojiano nini kiliendelea?
Shahidi: Aliandika uthibitisho wake kwa mwandiko wake na akasaini.
Wakili Nassir: Umesema ulimwandika mshtakiwa maelezo ya onyo. Ukiyaona leo utayakumbuka?
Shahidi: Ndiyo, nitayakumbuka.
Wakili Nassir akampa karatasi na kutaka aseme ni kitu gani na kujibiwa kuwa ni maelezo ya onyo ya Mussa Ally Majeshi, ambayo alisema anataka ayatumie kama kielelezo na yakapokelewa na Jaji Maghimbi.
Baada ya wakili Nassir kumaliza kumuongoza shahidi huyo kutoa ushahidi, mawakili wa utetezi Hudson Ndusyepo, Majura Magafu, Emmanuel Safari na Lundu walianza kumuhoji uzoefu wake na kuwajibu kuwa alihitimu Chuo cha Polisi Moshi mwaka 2000.
Wakili Magafu alitaka kujua kama kulikuwa na ulazima wa kuandikia maelezo ya mshtakiwa mkoani Kigoma, na akajibiwa kuwa ilikuwa ni maelekezo ya Koplo Samwel.
Wakili Magafu: Je, una statement (maelezo) inayoonyesha uliyaandikia maelezo ya mshtakiwa Kigoma?
Shahidi: Hapana.
Wakili Magafu: Mshtakiwa namba saba alikueleza ni mkazi wa wapi?
Shahidi: Anaishi Babati mtaa wa Magugu.
Wakili Magafu: Ni haki zipi ulimpa mshtakiwa na ni kwa mujibu wa kanuni zipi?
Shahidi: Nilijitambulisha kwake na nikamweleza kama angependa mtu mwingine asikie akitoa maelezo.
Wakili Magafu: Uliwahi kumuuliza kama Kigoma anao ndugu?
Shahidi: Sikumuuliza.
Wakili Magafu: Ulimuuliza Kigoma anaye wakili?
Shahidi: Ndiyo, alisema hana.
Wakili Magafu: Ulitegemea nani ashuhudie akitoa maelezo ikiwa yeye ni mgeni Kigoma?
Shahidi: Alinijibu sina ndugu.
Wakili Magafu: Ulitegemea angempata wapi?
Shahidi: Alisema atatoa yeye mwenyewe kwa sababu hana wasiwasi.
Wakili Magafu: Uliwahi kumuuliza kuhusu huyo aliyekuwa akiongozana naye kuwa ni nani?
Shahidi: Sikumuuliza.
Wakili Magafu: Huyo aliyekuwa akiongozana na Ally Majeshi mlimpeleka wapi?
Shahidi: Tuliwaweka wote lockup (mahabusu).
Wakili Magafu: Nikisema mshtakiwa namba saba hakuwahi kuandika maelezo bali alilazimishwa kusaini tu,kweli siyo kweli?
Shahidi: Siyo kweli.
Wakili Magafu: Nikisema mshtakiwa namba saba alitwambia mawakili wake kuwa alichelewa kuunganishwa na wenzake kwa sababu alikuwa anaumwa baada ya kuteswa sana. Kweli, siyo kweli?
Shahidi: Siyo kweli.
Baadaye Wakili Safari alitaka kujua kama shahidi aliieleza mahakama kuwa mshtakiwa alikamatwa stendi na jibu likawa ndio, lakini akahoji kama ilikuwa usiku kwa kuwa waliwasha taa, lakini shahidi akasema ni kutokana na ukungu.
Shahidi huyo pia alisema hawakuandika maelezo ya mtu yeyote aliyekuwa stendi na baadaye Wakili Safari akampa karatasi kutaka aangalie sehemu ya juu kama pameandikwa.
Shahidi: Hapajaandikwa.
Wakili Safari: Mtu anaweza akasaini kitu ambacho hakijui?
Shahidi: Hapana, Majeshi alisaini kitu alichokifanya.
Wakili Safari: Mtu ambaye hajapigwa na kuteswa anaweza akasaini kukubali kusaini kosa ambalo hajafanya?
Shahidi: Alikiri amehusika na tukio la mauaji ya Erasto Msuya, ndiyo maana akasaini.
Wakili Safari: Kwenye maelezo hapo juu uliandika?
Shahidi: Sikuyaandika, hayapo.
Wakili Safari: Kilichomfanya asaini kitu ambacho hakipo ni nini kama siyo kupigwa?
Shahidi: Ni baada ya kumwambia.
Wakili Safari: Huyo mwingine ulimwandikia maelezo?
Shahidi: Hapana.
Wakili Lundu: Nani aliwaambia kuwa Ally anaishi Stendi?
Shahidi: Tulipata maelekezo kwa afande Samwel.
Wakili Lundu: Ulimuuliza mshtakiwa kama anajua kusoma na kuandika?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili Lundu: Kwa nini hukumpa mshtakiwa aandike maelezo yake mwenyewe?
Shahidi: Hili ni onyo.
Wakili Lundu: Kwa nini uliandika wewe na anayetakiwa kujibu hiyo sehemu ni Ally?
Shahidi: Aliponitajia mimi niliandika.
Wakili Lundu: Mshtakiwa alitueleza kuwa mlimtesa kwa kumpiga na chuma huku mmemfunga pingu mikononi.
Shahidi: Hilo mimi sijui.
Wakili Lundu: Rejesta ya kuwaweka lockup (mahabusu) ipo wapi?
Shahidi: Ipo Kigoma.
Kesi hiyo inawakabili washitakiwa saba ambao ni Sharifu Mohamed, Shaibu Jumanne au Mredii, Musa Mangu, Jalila Zuberi, Karim Kihundwa, Sadick Mohamed au Msudani au Mnubi na Ally Mussa.
Habari hii imeandikwa na Daniel Mjema, Charles Lyimo na Janeth Joseph