Madaktari watakiwa kuchunguza wagonjwa maeneo nyeti wakiwa na wasimamizi wao

Muktasari:

  • Ili kuepusha madaktari na wahudumu wa afya kuwanyanyasa kijinsia wagonjwa, wametakiwa kuwahusisha wasimamizi wa wagonjwa wanapokuwa wakifanya uchunguzi katika sehemu zao nyeti.

Dodoma. Ili kuepusha madaktari na wahudumu wa afya kuwanyanyasa kijinsia wagonjwa, wametakiwa kuwahusisha wasimamizi wa wagonjwa wanapokuwa wakifanya uchunguzi katika sehemu zao nyeti.

Hayo yamesemwa leo Novemba 25 na Msajili wa Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT), David Muzava wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kanuni za maadili na utendaji wa kitaalamu kwa Madaktari kwa lengo la kuelimisha umma leo Novemba 25 jijini hapa.

Muzava amesema kutokana na madaktari kufanya uchunguzi katika sehemu nyeti wakiwa peke yao kwenye sehemu za faragha kumewafanya kuingia kwenye kashfa hizo.

“Mwanataaluma ana wajibu wa kuwa na mwana taaluma mwingine ambaye atakuwepo kipindi yeye anafanya uchunguzi kwenye maeneo nyeti ya ngonjwa ili kuepuka sintofahamu inayoweza kujitokeza.

“Kukiuka kwa takwa hili kumesababisha kuwepo kwa mashauri yanayohusisha unyanyasaji wa kijinsia kinyume na maadili ya kiutendaji, kwa kuwa mtu anafanya uchunguzi kwenye maeneo nyeti na hakuna mtu mwingine pale kusimamia eneo hilo,” amesema.

Amesema Kanuni hiyo inaweka wajibu kwa mtaalamu kuwa na usiri wa taarifa za mgonjwa katika matibabu yanayohusisha pia kugusa mwili wa mgonjwa na katika kufanya hilo inamtaka kupata ridhaa kutoka kwa mteja husika.

Aidha amesema madaktari wana wajibu wa kutenda wema na ubinaadamu kwa wagonjwa wao ikiwa ni wajibu unaotakiwa kutoka kwa mwanataaluma kutenda kwa manufaa ya wengine.


Amesema wataalamu wana wajibu wa kutenda kazi ambayo matokeo yake hayatodhuru mteja wake kwa kufata ushauri wa kitaalamu ikiwa atakutana na tatizo ambalo hana utaalamu nalo.

“Kumekuwa na mifano ambayo sio ya kuigwa ya wanataaluma ambao wanaendelea kutoa huduma kwa mgonjwa hata kwa matatizo ambayo yeye hana utaalamu nayo na kufanya mgonjwa kupata matibabu ya chini ya kiwango,” amesema.

Amesema mgonjwa ana haki ya kupewa majibu ya ugonjwa wake ili awe na chaguo la kimatibabu yatakayomsaidia kukubali au kukataa matibabu anayotakiwa kufanyiwa kwa kuangalia njia chanya itakayomfaa bila kukiuka taratibu za maadili ya kiutendaji.

Pia amesema wanataaluma wana haki ya kutoa huduma ya haki sawa, na utendaji ufaao kwa kile anachostahili kufanya mwanataaluma husika bila kujali jinsia, kabila na dini ya wagonjwa pamoja na kutoa gharama sahihi za matibabu.