Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Madereva daladala Arusha wagoma, abiria wapanda toyo

Muktasari:

 Wakazi wa Jiji la Arusha wakiwamo wanafunzi waliofungua shule leo wamepitia msoto wa hali ya juu kutokana na kukosa usafiri.


Arusha. Wakazi wa Jiji la Arusha wakiwamo wanafunzi waliofungua shule leo Jumatatu Julai 3, 2023 wamepitia msoto wa hali ya juu kutokana na kukosa usafiri.

Adha ya usafiri imesababishwa na mgomo wa daladala unaoendelea katika barabara zote za Jiji la Arusha na Arumeru kushinikiza kuondolewa kwa bajaji katika ruti zao.

Akizungumzia hali hiyo miongoni mwa abiria, Amina Hassan amesema mgomo huo umeanza leo asubuhi umesababisha mateso makubwa kwa wakazi wa Jiji la Arusha pamoja na wanafunzi wanaotumia usafiri huo kuwahi makazini na shuleni.

"Tunaomba Serikali itafute suluhu ya jambo hili kwani tunaoteseka ni wananchi na hili jambo la daladala kugoma imekuwa siyo mara moja," amesema.

Ramadhani Ally aliiomba serikali kusikilizwa madai ya daladala na kutatua changamoto hiyo.

"Shida hawa daladala wanataka wao wenyewe ndio wafanye kazi ya usafirishaji wakati hii ni biashara huria, inafaa kila mtu acheze kwenye nafasi yake kupata kipato.

“Hivyo tunaomba Serikali isikilize madai yao kama yana maana watatuliwe lakini kama ni haya ya ubinafsi wenzao wasifanye kazi basi  wanaohamasisha mgomo wafutiwe leseni," amesema.

Akizungumzia mgomo huo, Mwenyekiti wa Chama cha Wasafirishaji Mkoa wa Arusha na Kilimanjaro, Locken Adolf amesema kuwa utitiri wa bajaji umeathiri biashara ya daladala hivyo wanaiomba serikali kuzipunguza.

"Ukubwa sa eneo la Arusha, hazitakiwi kuzidi zaidi ya 100 lakini sasa zimekuwa nyingi na zimekuwa kero sana na zimeteka ruti zote za daladala. Pia zinafanya biashara ya kupakia abiria kama wanavyofanya wenzao jambo ambalo siyo makubaliano wakati zinaingia mjini," amesema.

Amesema kuwa katika ufuatiliaji wamebaini bajaji nyingi ndani ya Jiji la Arusha hazina leseni lakini zinaruhusiwa kufanya kazi tofauti na daladala ambazo zimekuwa zikipigwa faini kila hatua.

"Tunataka kujua anayesimamia hizi bajaji ni nani na ana sauti gani kwenye mamlaka za serikali zinazosimamia usafirishaji, kwa kuwa wao wanafanya kazi kinyume na sheria, taratibu na makubaliano lakini hawafanywi chochote wanazidi kupeta tu," amesema.

Akizungumzia adha hiyo Ofisa Mfawidhi wa  Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), Mkoa wa Arusha, Amani Mwakalebela amesema kuwa wamesikia mgomo huo na wanaendelea na taratibu za kushughulika na madai ya madereva hao wa daladala.

"Sisi tumesikia madai yao na tunaendelea kuyafanyia kazi hivyo niwaombe warudi barabarani kuendelea kutoa huduma na tutawapa majibu ya suluhu ya changamoto yao," amesema.

Katika hilo Mwakalebela amekiri ongezeko la bajaji ndani ya Jiji la Arusha hasa ruti za Sombetini-Ngusero, pia njia ya Majengo, pamoja na ile ya Uswahilini -Dampo ambapo wameanza kuhukua hatua.

"Kweli kuna ongezeko la bajaji ambapo katika 350 zilizosajiliwa na zoezi kufungwa lakini kwa haraka haraka kuna zaidi ya bajaji 2,000 ambazo zinafanya kazi na kugeuka kero, hivyo tulichoamua ni kuomba oda ya mahakama kuzipiga mnada bajaji ambazo tutazikamata hazina usajili wala leseni na uzuri tulishafunga mwaka jana," amesema Mwakalebela.