Madereva wasitisha mgomo, mabasi ya mikoani yaanza kazi

Mbowe akizungumza na madereva mara baada ya kuwasili katika kituo cha mabasi cha Ubongo leo jijini Dar es Salaam. 

Muktasari:

Mgomo huo ulioanza jana umesababisha usumbufu mkubwa kwa raia sehemu nyingi nchini Tanzania ambao walikuwa wamejiandaa kusafiri kuelekea katika mikoa mingine jana na leo kwa ajili ya shughuli zao mbalimbali zikiwemo za kibiashara na kijamii.

Online Team, Mwananchi

Hatimaye madereva wa mabasi na malori wameamua kusitisha mgomo leo baada ya Serikali kuwahakikishia kuwa inaandaa utaratibu mzuri wa kujibu na kushughulikia matatizo yao.

Mgomo huo ulioanza jana umesababisha usumbufu mkubwa kwa raia sehemu nyingi nchini Tanzania ambao walikuwa wamejiandaa kusafiri kuelekea katika mikoa mingine jana na leo kwa ajili ya shughuli zao mbalimbali zikiwemo za kibiashara na kijamii.

Taarifa zilizotufikia ni kwamba Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda akiwa na viongozi wengine wa Serikali walifika katika kituo cha mabasi yaendao mikoani cha ubungo na kuzungumza na madereva hao wakiwataka wasitishe mgomo wao na kuanza kazi kwani mambo yao Serikali inayafanyia kazi na hivi karibuni watajibiwa.

Kufuatia hali hiyo maderva hao walikubaliana na ombi hilo la Serikali baada ya kutokea kwa Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Freeman Mbowe ambaye naye aliwasihi waache mgomo huo kwani Serikali itafanyia kazi maombi yao.

Ungana nasi baadaye kwa ajili ya tarifa zaidi.

xxxxxxx

Nchi yasimama: Madereva mabasi, malori wagoma sehemu kubwa ya Tanzania

Dar/mikoani. Nchi imesimama. Hii ndiyo sentensi inayofaa kuelezea tukio la jana la mgomo wa madereva nchini kote ambao kwa mara ya kwanza ulisababisha mabasi yote kutoka Dar es Salaam kwenda mikoani na nchi jirani kushindwa kuondoka.

Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo (UBT), kushindwa kutoa huduma kwa sababu yoyote ile.

Tangu asubuhi hadi jioni, hakuna basi hata moja lililotoka wala kuingia katika kituo hicho hadi abiria walipoanza kukata tamaa na baadhi yao kuondoka na wengine kuanza kushinikiza kurejeshewa nauli.

Mgomo huo ambao ni mwendelezo wa ule uliofanyika Aprili 9, mwaka huu ulipewa uzito na madereva hao baada ya ahadi walizopewa na Serikali kutofanyiwa kazi kama ilivyoahidiwa na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka.

Tofauti na wa awali, safari hii mpaka inatimu saa 11.00 jioni hakuna kiongozi yeyote aliyejitokeza katika kituo hicho kusikiliza kilio cha madereva hao.

Hata hivyo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameunda kamati ya iliyotangazwa na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta ya kusimamia usafiri barabarani itakayowakutanisha wadau wote ili kutatua matatizo katika sekta hiyo kila yanapotokea.

Polisi wachemsha Dar

Tangu saa 2.30 asubuhi, polisi walijaribu kuyasindikiza mabasi waliyodhani madereva wake wako tayari kuondoka Ubungo lakini walishindwa baada ya kutoungwa mkono.

Mkuu wa Trafiki Ubungo, Inspekta Yussuf Kamotta akiwa na Inspekta Solomon Nkindwa ambaye pia ni mkaguzi wa magari, waliingia katika basi la Kampuni ya Master City na kuliondoa kituoni hapo wakiwa na mmiliki wa kampuni hiyo, Abdallah Mohammed huku wakimtafuta dereva bila mafanikio na kulazimika kulitafutia sehemu salama ya kuliegesha baada ya madereva kulizingira.

Kitendo cha askari hao kilisababisha kuzomewa kwa Inspekta Nkindwa wakisema mkaguzi huyo arudi shule akasome... “Solomoooon… rudi shuuuule… gia nane… zimekushinda,” walisikika madereva hao wakiimba huku wakikimbia mchakamchaka kurudi zilipo ofisi zao.

Kutokana na vurugu zilizotokea nje ya kituo hicho, polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya watu waliokuwa katika makundi.

Nje ya UBT, magari sita ya polisi yaliegeshwa katika makutano ya barabara za Sam Nujoma, Nelson Mandela na Morogoro wakati mengine yakielekea Mwenge na Buguruni kwenda kukabiliana na tishio lolote ambalo lingeweza kutokea.

Saa 5.30 askari wa Kikosi cha Mbwa waliwasili kuongeza nguvu na kuvutia macho ya wengi kutokana na jinsi walivyokuwa na pilikapilika bila ya kuwapo kwa mhalifu yeyote anayetafutwa.

Sikukuu ya madereva

Tofauti na migomo mingine, huu haukuwa na vurugu zozote wala sintofahamu kwani kila mtu aliyekuwa UBT alionekana akiwa katika sehemu yake akiendelea na hamsini zake. Abiria walikuwa katika mabasi husika huku mawakala na makarani wakiendelea kukatisha tiketi za safari na kupanga mizigo ya abiria.

Huku wakiendelea na mazungumzo yao katika vikundi katika kituo hicho, madereva hao walisikia wakisema hapakuwa na mgomo, bali sikukuu yao.

“Madereva ndiyo watu walisahaulika. Hatuna utambulisho wowote mahali popote katika nchi hii. Hivyo leo tumeamua iwe sikukuu yetu wala hatugomi ila ni kama wanavyofanya wafanyakazi wengine katika sikukuu zao,” alisema.

Wamiliki watofautiana

Pamoja na kusitishwa kwa huduma za usafiri, wamiliki wa mabasi hawakuwa na kauli moja. Wapo waliounga mkono na kutowaruhusu madereva wao kuanza safari na wengine waliotaka huduma ziendelee kama kawaida.

Mmiliki wa mabasi ya Master City alisema alitoa ruhusa kwa askari kuliondoa gari lake kituoni hapo ili kuonyesha kuwa alikuwa haungi mkono mgomo uliokuwa unaendelea.

“Abiria wajue kuwa wamiliki hatuutambui huu mgomo na tunatamani kuona wateja wetu wanapewa huduma waliyoilipia. Hali hii ina madhara mengi kwetu na abiria pia kwani wana mipango yao,” alisema Mohammed.

Mmiliki wa mabasi ya Kirumo, Enea Mrutu alisema kinachotokea ni woga baina ya wamiliki na madereva kwani mgomo huo unafanywa na watu wachache ambao wanawalazimisha wengine.

Baadhi ya madereva walisema mgomo huo unatambulika na wamepata maelekezo kutoka kwa mabosi wao wasiondoe mabasi mpaka hali itakapokuwa shwari ili kuepusha hasara zinazoepukika.

Abiria walianzisha

Baada ya kuchoshwa na kukaa ndani ya mabasi, ilipotimu saa 9.30 alasiri abiria walianza kukusanyika kilipo Kituo cha Polisi na kuomba maelekezo ya nini cha kufanya baada ya dalili zote kuonyesha kuwa hakutokuwa na safari.

Baada ya kuambiwa kuwa hapakuwa na msemaji, walianza zomeazomea dhidi ya maofisa wa polisi waliokuwapo huku baadhi wakilalamikia malazi na kupanda kwa bei za vyakula.

Wakati hayo yakitokea ndani ya kituo, baadhi ya wahuni walitoka nje ya kituo hicho na kutaka kufunga barabara lakini polisi walirusha mabomu ya machozi kuwatawanya.

Tamko la madereva

Katibu wa Umoja wa Vyama vya Madereva Tanzania, Rashid Saleh aliwataka radhi Watanzania na abiria waliokwama kutokana na mgomo huo na kubainisha kuwa huduma zitaendelea mara tu Waziri Mkuu Pinda atakaposikiliza madai yao.

“Najua watu wengi wanaathirika lakini hatuna namna. Tunataka waziri mkuu aje atoe suluhisho la madai yetu. Hatutaki tena majadiliano kwani yalishafanywa na mawaziri wake… kwa sasa tunahitaji utekelezaji hivyo tunaendelea kumsubiri hata kama atakuja baada ya siku tatu,” alisema Saleh.

Tanga

Tangu saa 11.00 alfajiri, madereva waliingiza magari yao stendi na ilipofika saa 12 muda wa kuanza kuondoka abiria walipatwa na bumbuwazi baada ya kuona hayaondoki.

Maofisa wa Sumatra na polisi waliwabembeleza madereva kuondosha magari bila mafanikio na kuzusha tafrani.

Madereva hao waliokuwa katika mzozo na maofisa polisi na Sumatra, walisema wasingeondoa magari hadi watakapopata ruksa ya viongozi wao makao makuu.

“Sisi hapa hatuondoshi magari, madai yetu ni ya msingi, alisema dereva wa basi la Simba Mtoto, Hussein Zubeir.

Wakala wa mabasi ya Mtei, Albert Clement alisema Serikali inawajibika kusikiliza madai ya madereva vinginevyo mgomo huo unaweza kusambaa.

Arusha

Mjini Arusha mgomo huo, ulianza kwa kusuasua. Baadhi ya magari yaliondoka baada ya kushauriana na maofisa wa polisi waliokuwa kituoni hapo.

Baadhi ya mabasi ya kutoka Arusha kwenda Bukoba, Mwanza, Kahama, Singida na Dar es Salaam yaliondoka saa 1.30 asubuhi badala ya muda wa kawaida wa saa 12.00 na 12.30 kutokana na mgomo huo, lakini kwa kusindikizwa na magari ya polisi kutokana na hofu ya kushambuliwa kwa mawe.

Hiyo ilikuwa baada ya polisi na Chama cha Wamiliki wa Magari ya Abiria Arusha na Kilimanjaro(Akiboa) kukutana na madereva hao na kuwashawishi kuendelea na kazi.

Hata hivyo, baadhi ya magari yaliishia Moshi na kuzuiwa na mengine mkoani Singida.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Libaratus Sabas alisema baada ya kikao hicho: “Ndugu zangu tumekuwa na makubaliano mwendelee na kazi wakati hoja zenu zinafanyiwa kazi ili kutoathiri wageni wetu hasa watalii. Arusha ni jiji la kimataifa hivyo tusilitie doa.”

Katibu wa Akiboa, Locken Adolf aliitaka Serikali kumaliza mgogoro huo hasa suala la kusoma madereva kila baada ya miaka mitatu.

Pwani

Mamia ya abiria katika Kituo cha Mailimoja, Kibaha walishindwa kusafiri baada ya kutoonekana kwa basi hata moja kituoni hapo kutoka maeneo mbalimbali.

Mbali na abiria wa mikoani, adha hiyo pia iliwakumba wasafiri wa daladala kwani wengi walilazimika kutumia pikipiki na magari madogo ya mizigo maarufu kirikuu kufika kwenye shughuli zao.

Abiria hao walipata pigo jingine ilipotimu saa nane mchana baada ya mvua kunyesha na kutokana na wingi wao, idadi kubwa walikosa sehemu za kujikinga kutokana na eneo hilo kutokuwa na vibanda vya kupumzikia.

“Nimelowana na nina hofu hata vitu vyangu kwenye begi vimelowa,” alisema msafiri aliyekuwa kituoni hapo, Vivian Piuza.

Abiria waliokuwa na safari za karibu walilazimika kupanda kirikuu na Noah kwa kulipa kati ya Sh1,000 hadi Sh1,500 badala ya Sh300 na 400 wakati wale waliokuwa wakienda Ubungo walitakiwa kulipa Sh3,000 badala ya Sh1,000 na Sh1,200.

Ruvuma

Abiria jana walijikuta wakichapa usingizi ndani ya basi na wengine wakizunguka katika Kituo cha Mabasi Malamala baada ya kushindwa kusafiri kutokana na mgomo huo.

Mbeya

Abiria waliokata tiketi kwa safari za kwenda nje ya Mkoa wa Mbeya kwa mabasi waliwatupia lawama wamiliki wakisema waliwaibia fedha zao kwa kuwakatia tiketi wakati wakijua kuna mgomo.

“Huu ni wizi kabisa, haiwezekani mmiliki asijue kwamba dereva wake ana mpango wa kugoma halafu mawakala wao wanakata tiketi badala ya kutuambia ukweli kuwa hakuna usafiri,” alisema abiria Sophia Alfredy aliyekuwa anakwenda Dodoma.

Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Abiria Mbeya, Stanford Mwambojela aliwashauri abiria kuwashtaki wenye mabasi yaliyochukua fedha zao wakati walijua mgomo huo.

Mgomo huo uliwaathiri wagonjwa kwenye Hospitali za Rufaa Mbeya, Meta na hata ya mkoa baada ya ndugu wengi kushindwa kwenda kupeleka chai asubuhi.

Akizungumza kwa simu, mmiliki wa mabasi ya Ndenjela, Allan Mwaigaga alisema hawana habari ya mgomo huo kwa vile hakuna mahali popote yalipofanyika mazungumzo baina yao na madereva hao.

Mwaigaga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya, alisema suala hilo lina mambo mengi yaliyojificha, hivyo Serikali ichunguze kwa kina.

Dodoma

Polisi mkoani hapa walilazimika kuyasindikiza mabasi ambayo madereva wake hawakushiriki mgomo ili kuepuka kufanyiwa fujo njiani.

Mabasi yaliyosindikizwa ni yale yanayomilikiwa na Kampuni ya Shabiby ambayo yaliendelea na ratiba zake kama kawaida.

“Mimi nilikuja hapa asubuhi nikawauliza madereva si mna mkataba na kampuni? Wakanijibu ndiyo, nikawaambia ingieni kwenye gari zenu anzeni safari,” alisema mmiliki wa mabasi hayo, Ahmed Shabiby.

Shabiby ambaye pia ni Mbunge wa Gairo (CCM), alisema hofu kubwa ya madereva wake ni fujo zinazoweza kufanywa njiani kwa kisingizio cha usaliti. Hata hivyo, basi lililokuwa likielekea Mbeya, lilikwama Iringa.

Kutokana na hali hiyo aliomba ulinzi wa polisi wa kusindikiza mabasi hayo hadi nje ya mji kutokana na baadhi ya watu katika maeneo ya Chang’ombe, Njiapanda ya Area D na Nkuhungu waliokuwa wanasimamisha mabasi, daladala, bajaji, teksi na pikipiki wakiwalazimisha kushusha abiria.

“Nilipakia abiria pale Emaus nakuja mjini, nilipofika Njiapanda ya Area D nikasimamishwa na mtu ninayemfahamu ambaye alinihoji iwapo mtu niliyempakia ni abiria au la,” alisema na kuongeza dereva bodaboda Said Juma. “Yule abiria akasema huyu ni mdogo wangu. Mwanzoni sikuelewa lakini baada ya kutuachia pale ndipo abiria akaniambia kuwa ni sababu ya mgomo.”

Abiria waliokuwa wamekata tiketi kwa ajili ya safari ya kwenda maeneo mbalimbali licha ya mgomo huo walionekana wakiwa wameketi ndani ya mabasi wakiwa wamekata tamaa.

Moshi

Mgomo huo uligeuka neema kwa madereva bodaboda na bajaji mjini Moshi baada ya kuutumia kuongeza gharama za usafiri.

Nauli za bodaboda zilipanda kutoka Sh1,000 hadi 3,000 kwa maeneo ya Moshi Mjini na kwenda wilaya jirani ya Hai usafiri huo ulifikia Sh25,000 hadi 30,000, eneo ambalo kwa basi ni Sh1,000.

Wagonjwa walilazimika kutumia usafiri wa teksi ambao nauli yake ilipanda hadi Sh10,000 kutoka Sh5,000.

Katika Kituo cha Mabasi Moshi Mjini, mabasi yote hayakuruhusiwa kutoka na hata yale yaliyotokea Arusha yalipofika, yalizuiwa kuondoka.

Iringa

Abiria waliokuwa wakisafiri kwenda nje ya mkoa hususan Dar es Salaam walikwama kwenye Kituo cha Mabasi Iringa. Mbali ya hao, hata mabasi yaliyokuwa yakipitia Mjini Iringa kuelekea maeneo mengine ya nchi walikwama.

Basi la Shabiby kutoka Dodoma kwenda Mbeya lilishindwa kuendelea na safari baada ya dereva wake kuziwa na kundi la watu waliokuwa wakishabikia mgomo huo.

Kondakta wa gari hilo, Ray Magaila alisema: “Tumetoka Dodoma saa 12.00 lakini tulipofika hapa dereva wangu amevamiwa na kubebwa juujuu na kundi la watu, wamemuumiza kidogo na hadi sasa sijajua amejificha wapi.”

Mmoja wa abiria aliyeathiriwa na mgomo huo, Luciana Mpulule aliyekuwa akielekea Dar es Salaam kwa matibabu alisema: “Nimesafiri kwa shida kutoka Magulilwa (nje ya Mji wa Iringa) hadi hapa ... kwa kweli Serikali inastahili kulaumiwa.”

Kutokana na adha hiyo, Ofisa Mfawidhi wa Sumatra Mkoa wa Iringa Baltazar Patel alisema madereva wa mkoa huo walikuwa tayari kuendelea na safari lakini walishindwa kufanya hivyo kutokana na shinikizo la wenzao waliopo Dar es Salaam.

Imeandikwa na Julius Mathias, Hussein Issa, Salim Mohammed, Filbert Rweyemamu na Mussa Juma, Julieth Ngarabali, Sanjito Msafiri, Joyce Joliga, Godfrey Kahango, Albert Msole, Brand Nelson, Sharon Sauwa, Geofrey Nyang’oro na Rehema Matowo.