Mafuriko Morogoro yalivyomuua mwenye ulemavu
Morogoro. Mvua kubwa iliyonyesha katika Manispaa ya Morogoro kwa zaidi ya saa moja imeacha simanzi kwa mkazi wa Mtaa wa Kihonda B, Amina Nkwambi (67) aliyempoteza mjukuu wake, Omary Yahaya (20) aliyefariki dunia katika mafuriko.
Mvua hiyo iliyonyesha Januari 25, 2024 ilisababisha uhalibifu wa miundombinu ya barabara na makazi, huku watu sita wakiripotiwa kufariki dunia kwa kusombwa na maji.
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji liliokoa watu zaidi ya 240 waliozingirwa na maji katika kaya 157.
Akisimulia tukio hilo leo Januari 28, 2024, Amina amesema siku ya tukio saa tano asubuhi mvua ilinyesha na maji yaliingia eneo la choo na ndani ya nyumba, wakati wanatafakari nini cha kufanya, ukuta wa sebule ulianguka na maji kuingia kwa kasi.
“Ilikuwa ni kitendo cha dakika chache maji kuingia ndani ya nyumba, yakiongezeka kwa kasi. Naisha na mjukuu wangu, Omary ambaye ni mlemavu wa viungo na takribani maisha yake yote amekuwa akikaa kwenye kitimwendo. Tulitafuta njia ya kujinasua kutoka ndani tulikwama,” amesema.
Amesema alimwita mtoto wake, Victoria Mkude ili ampatie nguo ya kumbeba Omary ambaye walikwama kutoka naye kwa kuwa hawakuweza kutoa ‘loki’ kwenye kitimwendo kutokana na wingi wa maji.
Amina amesema kiti hicho kina meza iliyokuwa ikimsaidia kukaa, hivyo kutokana na wingi wa maji, mjukuu wake alikunywa maji hayo zaidi ya mara mbili au tatu na kusababisha kifo chake.
Baada ya kugundua Omary amefariki dunia, amesema kazi kubwa ilikuwa kuhakikisha mwili wake hausombwi na maji.
Amesema akiwa na wanawe-- Amina Nkwambi na Victoria Mkude walishikilia mlango. “Maji yalifika usawa wa mdomo wangu wakati huo tukiwa tumesimama na mwili ukiwa umezama kwenye maji kwenye kibaraza cha nyumba yetu, tulikaa eneo lile kwa zaidi ya saa tatu, baadaye tulipata msaada kutoka kwa vijana waliofika kwa kamba na ngazi. Walitupandisha juu ya bati,” amesema.
Amina amesema Victoria alibaki eneo lenye mwili na kuwaeleza vijana hao ambao waliufunga kamba na kuupandisha juu ya bati ambako walikaa kwa saa moja mpaka maji yalipopungua takribani saa 10 jioni, ndipo watu walipokusanyika na kushusha mwili juu ya bati.
Mkazi wa Mtaa wa Kilombero, Kata ya Kihonda, Philipina Nyaki (64) amesema mvua imesababisha kuku 350 aliokuwa akifuga kusombwa na maji pamoja na kuharibu vyakula, huku vyombo vya ndani vikopotea.
“Nilikuwa nafuga kuku katika mabanda mawili, banda moja lilikuwa na kuku 200 na lingine 150, ni mmoja tu aliyepona kwa kunusurika kusombwa na maji nafikiri alirukia juu ya dirisha. Maji yalibomoa ukuta, vyumba vya uwani na vyombo viliondoka na maji. Nimepata hasara kubwa,” amesema na kuongeza ipo haja ya Serikali kuangalia chanzo cha mafuriko hayo ambayo kila mvua kubwa inaponyesha madhara huwa makubwa.
Katika mtaa huo, Juma Maganga amesema vyumba vitano vimebomoka na kwamba maji yalisomba baiskeli, magodoro na kuharibu vyakula na samani za ndani.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kilombero, Kata ya Kihonda, Asheri Ndahani (67) amesema katika mtaa huo kaya 11 zimeathiriwa zaidi kati ya kaya 54 zilizopo.
Mkazi wa Kihonda, Rukia Omary (55), amesema analazimika kujisaidia haja ndogo katika ndoo kutokana na choo alichokuwa akitumia kubomolewa na mafuriko.
“Usiku nalazimika kujisaidia kwenye ndoo kwa sababu jengo la choo changu limebomoka, sina choo. Mchana najisaidia kwa majirani. Maji yamebeba magodoro, vyombo vimeondoka pamoja na kuharibu mali mbalimbali,” amesema.
Mwenyekiti wa Serikali ya Ntaa wa Kihonda B, Hamis Mselem amesema mafuriko yameathiri kaya 180.
“Mafuriko haya yamesababisha kifo cha kijana, Omary Yahaya na kijana huyu alikuwa mlemavu wa viungo na chanzo cha umauti wake ni hayo maji. Kaya 180 zimeathiriwa, lakini kaya mbili hazina mahala pa kuishi, kwani nyumba zao zimebomoka kabisa na wamepoteza kila kitu ndani,” amesema.
Mkazi wa Kihonda B, Shafii Kimanga, amesema ameishi mtaa huo tangu mwaka 1995, maji ya mvua yalikuwa yakipita machache ambayo hayakuwa na madhara kwa wananchi.