Mafuriko Mtwara yaua mmoja, kadhaa wahama makazi

Muktasari:

Mtu mmoja amefariki dunia baada ya kusombwa na maji kufuatia mvua kubwa zilizonyesha kwa siku mbili katika Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Mtwara. Mtu mmoja amefariki dunia baada ya kusombwa na maji kufuatia mvua kubwa zilizonyesha kwa siku mbili katika Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Watu wengine zaidi wamelazimika kuyahama makazi yao kwenda maeneo yaliyotengwa na uongozi wa mkoa kujihifadhi kutokana na maeneo mengi kukumbwa na mafuriko.

Maeneo ya Manispaa ya Mtwara, ambayo yamezingirwa na maji ni pamoja na Chuo cha Ualimu Mtwara, Nabwanda, Likonde, Magomeni, Chuno na Kiangu huku barabara za mji huo zikiwa hazipitiki kutokana na mvua hizo.

Hali hiyo ilisababisha Serikali kutenga shule za sekondari za Mikindani, Chuno, Shangani, Rahaleo, Majengo, Bandari, Naliendele, Mangamba na Umoja na shule za msingi za Majengo, Tandika, Rahaleo, Kambarage na Lilungu kwa ajili ya kuhidhi waathirika.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mtwara, Christina Sunga aliiambia Mwananchi jana alisema hadi jana walikuwa na taarifa ya kifo cha mtu mmoja kilichotokana na maafa hayo.

Hata hivyo, uongozi wa mkoa wa Mtwara mbali na taarifa ya kifo cha mtu mmoja, ulisema bado unakusanya takwimu kujua walioathirika na mafuriko hayo.

Sungu alimtaja aliyepoteza maisha kuwa ni Ismail Maruchile, ambaye inasemekana alikuwa fundi wa televisheni mjini Mtwara.

Kamanda huyo alieleza mtu huyo alikuwa anaendesha pikipiki katika maeneo ya Mkanaredi ambako alisombwa na maji.

“Aliingia kwenye karavati baada ya pikipiki kuacha njia na alipopatikana alikuwa ameshafariki dunia,” alieleza Sunga.

Aliongeza kuwa maeneo ya Kiyangu, Chuno, Chuo cha Ualimu Mtwara maji yalikuwa yamejaa hadi kwenye usawa wa madirisha ya nyumba na kusababisha hasara kubwa kwa watu.

Alisema hadi jana madhara yalikuwa makubwa na wananchi hawana amani katika makazi yao na wamalazimika kukaa nje kutokana na hofu.

“Watu wahame maeneo yaliyojaa maji waendekwenye maeneo yenye miinuko, nyumba nyingi zimejaa maji hali si shwari, inaelekea mitaro imezidiwa maji yanaingia kwenye makazi ya watu kwa sasa barabara zote si salama, hazipitiki kabisa tena na maji yanapita kwa kasi hivyo madereva wawe makini,” alisema Sunga.

Wananchi wazungumza

Mkazi wa Kiangu, Peter Marwa alisema amehama makazi yake akiondoka na nguo alizovaa pekee kutokana nyumba kuzingirwa na maji huku barabara zikifunikwa na maji mengi.

Alisema baada ya kuamka na kukuta maji yakiwa ndani na yamelowesha vitu vyote -- nguo, vyakula na vitu vingine, hatua aliyochukua ni kuondoka.

Mwajuma Athuman, mkazi wa Magomeni alisema baada ya kuona maji yakianza kuingia ndani alibebea watoto na kuanza kuwatoa na kuwapeleka kwa jirani ambapo palikuwa na nafuu.

“Nilikimbiza watoto wangu ili niwanusuru na janga hili, niliona ma yanaingia ndani ikabidi nitoke nje kuchungulia nikakuta ni mengi sana nje, niliporudi nilikuta yameongezeka na vitu vyote -- vyakula, nguo, makochi, kabati, televisheni na godoro vilikuwa katikati ya maji na kutokana na kasi yake nililazimika kuondoka haraka,” alieleza.

Kwa upande wake, alisema jana kuwa baadhi ya barabara zimefungwa huku zikitafutwa njia za kuokoa watu waliozingirwa na maji na kushindwa kutoka ndani ya nyumba zao.

Walioshindwa kutoka ndani kutokana na kuzingirwa na maji tunatafuta utaratibu wa kuwatoa hasa katika maeneo ya Kiyangu, Matopeni na Magomeni,” alisema Kyobya.