Mafuriko yaikumba Mtwara, 1,800 wakosa makazi

Jeshi la zimamoto na uokoaji Mkoa wa Mtwara likisaidia kuokoa wananchi wa Kijiji cha Kivava waliokumbwa na mafuriko baada ya mto Ruvuma kujaa maji. Picha na Florence Sanawa

Muktasari:

  • Zaidi ya watu, 1,800 wameathiriwa na mafuriko mkoani Mtwara baada ya mvua kubwa kunyesha katika wilaya za Mtwara na Nelwala jana.

Mtwara. Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Mtwara, Elizabeth Mpondele amesema kuna zaidi ya watu 1,800 wanaohofiwa kuatihriwa na mafuriko ya mto Ruvuma katika Wilaya za Mtwara na Newala.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa leo Aprili 5, Mpondele amesema kati ya watu hao, zaidi ya 1,400 wameokolewa katika wilaya ya Mtwara kijiji cha Kivava, huku wilayani Newala wakiokolewa watu 300.

“Ni kweli yametokea mafuriko makubwa watu wameingiliwa na maji nyumba nyingi zimebomoka watu wamekosa makazi.

“Kuna kaya 528 katika vijiji na vitongoji vya Kivukoni na Sokoni hivyo na wote wamehamishiwa shule ya msingi Kivava hapo kwa ajili ya kuangalia usalama wao na mali zao,” amesema.

Alkizungumzia janga hilo, Mkuu wa Wilaya ya Newala Alhaji Rajab Kundya amesema kuwa zaidi ya wakazi 314 waliokuwa wakiishi katika makazi ya muda huku wakilima katika eneo hilo ndio walioathiriwa.

“Kwa sasa tulikuwa tunafanya uokoaji katika hili eneo ambalo awali lilishapigwa marufuku na serikali kuishi kwa kuwa ni bondeni,” amesema.

Amesema katika eneo hilo la kisiwa cha Shangani zaidi ya wakazi 159 nao wameathiriwa.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mkunya, Salma Karani amesema kuwa zaidi ya wakazi 200 wa kata yake wameathirika na mafuriko hayo ambayo yamesomba vyakula na mifugo.

“Katika kata yangu kuna zaidi ya watu 200 wameathirika na maji hayo yaani kijiji cha Lihapa, sehemu kubwa kimefunikwa na maji, tumepoteza mifugo, mahindi, mpunga, ufuta na korosho vilivyokuwa karibu na kuvunwa,” amesema.

Naye Diwani wa Kata ya Mchori 1 Wilayani Newala, Said Chakame amesema kuwa maji yamekuwa mengi na wananchi bado wanaendelea kuokolewa.

“Wananchi wengi wanaishi mashambani hata kwenye kitongoji cha karibu kimefunikwa na maji. Wananchi wamekusanyika katika eneo la mlima ili wajihifadhi,” amesema Chakame.