Magufuli, maaskofu wanadi amani, umoja
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa akisalimiana na waumini baada ya Ibada ya Sikukuu ya Pasaka iliyofanyika katika Kanisa la Azania Front jijini, Dar es Salaam jana. Picha na Anthony Siame
Muktasari:
- Rais Magufuli aliyesali katika Kanisa la Mtakatifu Joseph, Jimbo Kuu la Dar es Salaam jana, aliwatakia heri ya Pasaka waumini akitoa wito kwa Watanzania kuendelea kuishi kwa amani na upendo, huku wakishiriki ipasavyo katika ujenzi wa Taifa.
Dar/Mikoani. Wakati viongozi wa dini wakikemea roho za chuki na visasi katika mahubiri ya mkesha na ibada za Pasaka, Rais John Magufuli ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuishi kwa amani na upendo.
Rais Magufuli aliyesali katika Kanisa la Mtakatifu Joseph, Jimbo Kuu la Dar es Salaam jana, aliwatakia heri ya Pasaka waumini akitoa wito kwa Watanzania kuendelea kuishi kwa amani na upendo, huku wakishiriki ipasavyo katika ujenzi wa Taifa.
Alitoa wito huo baada ya Paroko Msaidizi wa Parokia ya Mtakatifu Joseph, Padri Venance Tegete aliyeongoza misa hiyo kumkaribisha kutoa salamu.
“Kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo ukafufue matendo yetu, tuendelee kuijenga amani yetu, upendo wetu na tujenge maendeleo ya Watanzania wote, kwani Kristo alifundisha upendo miongoni mwetu,” alisema Rais Magufuli katika taarifa ya Ikulu iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana.
Katika mahubiri
Akihubiri katika Kanisa la Azania Front jijini Dar es Salaam, Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani ya Kanisa la Kiinjili ya Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa aliwaasa Watanzania kuondoa roho za chuki na visasi, badala yake waishi kwa amani kwa sababu wameumbwa kwa mfano wa Mungu.
Alisema Watanzania wanapaswa kufungua masikio na kusikia agizo la Mungu ili kulinda amani, “Dunia ina mambo mengi, dunia ina kelele nyingi, fungua masikio na usikilize Mungu anakuambia nini na Roho Mtakatifu akikuambia nenda ukashuhudie atakuongoza kufuata yale uliyoyasikia yapate kutendeka katika maisha yako.”
Dk Malasusa alisema binadamu hapaswi kuishi kwa huzuni na manung’uniko wala kukata tamaa katika maisha.
“Kuna watu wamezaliwa kuwapelekea wenzao hofu lakini sisi Wakristo tumezaliwa na kuagizwa kuwaletea watu matumaini na kuhubiri amani,” alisema Dk Malasusa.
Alisema wasije kutokea watu wakavuruga amani kwa kuwa itakuwa ni vigumu kuirejesha na kuwataka Wakristo kusimamia maandiko katika kuhubiri amani badala ya kusikiliza maneno kutoka sehemu tofauti.
“Ndiyo maana tunafuatwa na kuambiwa tuhubiri amani kwa sababu wanaamini dini zina nguvu katika kuhubiri amani na ni rahisi waumini kuyasikiliza kama ilivyo kwa maandiko,” alisema.
Katika misa takatifu ya Pasaka iliyofanyika kwenye Kanisa la Mtakatifu Petro, Oysterbay jijini Dar es Salaam Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa aliwataka waumini kuishi maisha ya kutolipa ubaya kwa ubaya kwa wanaowatendea uovu, bali kulipa ubaya kwa wema.
“Haijalishi umeumizwa na nini kutoka kwa watu wanaokuzunguka, usilipe ubaya huo kwa ubaya, bali lipa ubaya kwa wema nawe utakuwa na amani,” alisema na kuongeza kuwa ulimwengu umejaa mambo mengi yanayoumiza.
“Unaweza kutendewa ubaya mwingi kama vile kupigwa, kuonewa, kudhalilishwa na hata kuuawa. Ukifanyiwa ubaya kwa sababu ya wema wako, kuwa na amani na mshukuru Mungu, lakini kama unafanyiwa ubaya kwa sababu ya dhambi uliyotenda basi tubu na Mungu atakusamehe na utakuwa na maisha ya amani.”
Askofu Nzigilwa alisema Mkristo aliyeiva ni yule mwenye uwezo wa kushinda ubaya kwa kufanya yaliyo mema na ndiyo maisha wanayopaswa kuishi.
Pia alitoka kauli hiyo juzi katika mkesha wa Pasaka kwenye Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph akisema hakuna sababu ya kulipiza kisasi. Alisema kinachotakiwa ni kumshirikisha Mungu kwa vita unayokutana nayo dhidi ya adui.
“Ujumbe wa Pasaka ni kushinda mabaya kwa kutenda yaliyo mema, hupaswi kulipiza kisasi, mshirikishe Kristo. Huwezi kufanya kila kitu mwenyewe, namsifu sana Musa kila alipokwama kule Jangwani alikwenda kumuuliza Mungu, sasa hapa nifanyeje,” alisema Askofu Nzigilwa.
Kauli hiyo pia ilitolewa na Askofu Mteule wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Isaac Amani aliyewataka waumini na Taifa kwa jumla kuachana na maisha ya chuki na mafarakano.
Akizungumza katika Kanisa la Kristo Mfalme Moshi, alisema kuna hali ya kusikitisha kwa baadhi ya waumini kuendeleza chuki na kukataa kushirikiana kwa mambo yenye kuleta maendeleo katika jamii.
Pia, alisema upo umuhimu wa waumini kufurahia na kuheshimu rasilimali za nchi.
“Tufurahie na tulinde rasilimali za nchi ambazo Mungu ametujalia,” alisema Askofu Amani.
Katika adhimisho la misa ya Pasaka kwenye Parokia ya Mtakatifu Maurus Kurasini, Padri Maselino Mukari aliwataka waumini kuwa waadilifu na kuachana na mambo yasiyompendeza Mungu ili kuishi maisha ya furaha, amani na upendo. Alisema bila hayo, kuna uwezekano wa kuwapo uvunjifu wa amani.
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo aliwaasa waumini kufufuka na Yesu Kristo kwa kuzingatia mateso na mafunzo aliyoyatoa.
Akihubiri katika Misa ya Sikukuu ya Pasaka iliyofanyika kwenye Kanisa la Mtakatifu Joseph, Kardinali Pengo alisema ni wajibu wa kila mmoja kusimamia imani yake.
“Hata kama umeteswa, umeumizwa kiasi gani, Bwana Yesu Kristo alisimamia imani yake, nasi tusimamie imani yetu na kuidumisha,” alisema.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sosthenes alisisitiza amani, kupendana na kuachana vitendo viovu, vikiwamo rushwa, ufisadi na mambo yanayomkandamiza binadamu.
Alisema hayo katika ibada iliyofanyika katika Kanisa la Anglikana Mtaa wa Mtakatifu Theresia lililopo Kata ya Vijibweni wilayani Kigamboni.
Askofu Sosthenes aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa kanisa jipya linalojengwa eneo hilo.
Imeandikwa na Aurea Simtowe, Jackline Masinde, Kelvin Matandiko, Pamela Chilongola, Ibrahim Yamola, Bakari Kiango, Emmanuel Mtengwa (Dar); Ipyana Samson na Godfrey Kahango (Mbeya) na Janeth Joseph (Moshi).