Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mahakama yaelezwa kontena dawa za kulevya lilivyoingizwa Tanzania

Washtakiwa wanadaiwa kuingiza shehena ya dawa za kulevya aina ya  Mitragyna Speciosa zenye uzito wa kilo 11,596, wakiwa chini ya ulinzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne

Muktasari:

  • Shaweji ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya kuingiza na kusambaza mbolea ya NRM Agro Limited na wenzake wanadaiwa kuingiza shehena hiyo ya dawa za kulevya aina ya Mitragyna Speciosa zenye uzito wa kilo 11,596, tukio wanalodaiwa kutenda Julai Mosi, 2025 katika Bandari Kavu ya Said Salim Bakhresa (SSB ICD) iliyopo Sokota, Wilaya ya Temeke.

Dar es Salaam. Mashahidi 42 na vielelezo 88 vinatarajiwa kutolewa mahakamani katika kesi ya kusafirisha na kuingiza nchini sampuli za dawa za kulevya aina ya Mitragyna Speciosa zenye uzito wa kilo 11,596, inayowakabili washtakiwa 10 wakiwemo raia wa Sri Lanka na kampuni za uingizaji na usambazaji wa mbolea.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nitike Mwaisaka akishirikiana na Erick Mabagala, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Alhamisi Juni 4, 2026 wakati wakiwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo washtakiwa hao, yaani Committal Proceeding.

Washtakiwa hao ni Riziki Shaweji, ambaye ni Mkurugenzi na Rais wa Kampuni ya uingizaji na usambazaji wa mbolea ya NRM Group Company Limited na mkazi wa Masaki.

Wengine ni Andrew Nyembe (34), wakala wa forodha; Mariam Ngatila (40), ambaye ni mke wa Shaweji; na Ramadhani Said (57), mfanyabiashara na mkazi wa Kifuru.

Wengine ni dereva Godwin Mafikiri (40), mkazi wa Oysterbay, na wafanyabiashara wawili raia wa Sri Lanka, Jagath Wellalage (46) na Santhush Hewage (25).

Washtakiwa wengine ni kampuni tatu zinazoingiza na kusambaza mbolea nchini ambazo ni NRM Agro Limited, NRM Group Company Limited na ASP Holdings Tanzania Limited.

Washtakiwa wanadaiwa kuingiza shehena ya dawa za kulevya aina ya  Mitragyna Speciosa zenye uzito wa kilo 11,596, wakiwa chini ya ulinzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne

Kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 19066 ya mwaka 2025 yenye shtaka moja la kusafirisha na kuingiza nchini sampuli za dawa za kulevya aina ya Mitragyna Speciosa zenye uzito wa kilo 11,596 kutoka nchini Sri Lanka.

Dawa hizo zina madhara sawa na dawa za kulevya aina ya heroini, kokaini na methamphetamine na moja kati ya madhara kwa watumiaji wa dawa hizo ni kupoteza kumbukumbu.

Hata hivyo, mashahidi hao wanatarajia kutoa ushahidi wao katika Mahakama Kuu pindi kesi hiyo ya kusafirisha dawa za kulevya itakapopangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa.

Washtakiwa hao wamesomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili hiyo.

Alidai vielelezo 88 ni vya nyaraka na halisi ikiwemo hati ya ukamataji mali, ripoti kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, kiasi cha dawa kilichokamatwa katika kontena pamoja na mali nyingine.

Mwaisaka baada ya kueleza hayo aliwasomea upya shtaka lao na kisha kuwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo.

Kabla ya kusomewa maelezo yao na ya mashahidi, Mahakama ilieleza kuwa amepatikana mkalimani aitwaye Hiran Sumaneweera, ambaye atatafsiri maelezo hayo kutoka lugha ya Kiingereza kwenda lugha inayotumika nchini Sri Lanka, kutokana na washtakiwa wawili katika kesi hiyo kutokujua Kiswahili na Kiingereza.

Namna walivyoingiza dawa hizo nchini

Akiwasomea maelezo ya shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, Wakili Mwaisaka aliieleza Mahakama hiyo jinsi mshtakiwa Shaweji alivyoingiza nchini dawa hizo zenye uzito wa kilo 11,596 zikiwa katika kontena lenye urefu wa futi 20.

Alidai ndani ya kontena hilo kulikutwa mifuko 450 ya salfeti yenye maandishi yaliyoandikwa mbolea.

Alidai dawa hizo ziliingizwa nchini Tanzania Juni 2025 zikitokea nchini Sri Lanka kupitia Bandari ya Dar es Salaam na kisha kupelekwa katika Bandari Kavu ya Said Salim Bakhresa (SSB ICD) iliyopo eneo la Sokota, Wilaya ya Temeke.

Akisoma maelezo ya shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, Salehe Ilala ambaye ni ofisa kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), alidai kuwa Juni 17, 2025 jioni alipata taarifa kutoka kwa msiri kuhusu kuwepo kwa kontena katika yadi ya Bandari Kavu ya SSB iliyopo Sokota, Wilaya ya Temeke, linalozaniwa kuwa limebeba dawa za kulevya.

Alidai mtoa taarifa huyo (msiri) alimueleza Salehe kuwa kuna kontena lingine ambalo linatarajia kuingia nchini Juni 21, 2025 ambalo lenyewe litaenda kuhifadhiwa katika yadi ya bandari kavu eneo jingine.

Salehe baada ya kupata taarifa hiyo alitoa maelekezo kontena hilo lisitolewe hadi atakapojitokeza mhusika.

"Julai 1, 2025, Salehe alipata taarifa kuwa mhusika wa kontena hilo la futi 20 amefika katika Bandari Kavu ya Said Salim Bakhresa na hivyo aliandaa timu yake na kwenda eneo hilo na kuonana na uongozi wa bandari hiyo," alidai Wakili Mwaisaka wakati akisoma maelezo ya shahidi huyo.

Alidai ofisa huyo kutoka DCEA alipofika alikutana na uongozi wa SSB ICD na kujitambulisha kwake.

Hata hivyo, ofisa wa SSB ICD, Said Abdallah Hemed, aliwaeleza timu hiyo kuwa kuna kijana aitwaye Andrew Nyembe ambaye ametumwa na Kampuni ya NRM Group Company Limited inayomilikiwa na mshtakiwa Shaweji kutoa kontena hilo.

Alidai walimueleza Nyembe ampigie mmiliki huyo ili afike eneo hilo wafanye upekuzi, hata hivyo walisubiri kwa muda wa saa nne bila mafanikio na hivyo kufungua na kuanza upekuzi.

"Ndani ya kontena hilo ilikutwa mifuko 450 ya salfeti ambayo ndani yake kulikuwa na unga wa rangi ya kahawia unaozaniwa kuwa ni dawa za kulevya na mifuko hiyo kwa nje ilikuwa imeandikwa mbolea," alidai wakili.

Pia walikamata simu ya Nyembe na kumuweka chini ya ulinzi na baada ya kumaliza upekuzi waliondoka eneo hilo kurejea ofisi za DCEA zilizopo jijini hapa.

Julai 2, 2025, Salehe alipata taarifa kuwa Shaweji ataenda katika yadi ya SSB ICD kumuulizia mteja wake (Nyembe), hivyo alimtoa mahabusu Nyembe na kwenda naye katika yadi hiyo ili kumsubiri Shaweji.

"Baada ya muda, Shaweji alifika katika yadi hiyo akiwa na mwanasheria wake na kuelekea katika ofisi hiyo na ndipo Nyembe alipowaeleza maofisa wa DCEA kuwa amemuona bosi wake akishuka katika gari na kisha kupanda ngazi kuelekea ofisi za SSB ICD," alidai.

Alidai Salehe aliwasiliana na timu yake iliyokuwa eneo hilo na kumuweka chini ya ulinzi.

Alidai katika mahojiano ya awali, Shaweji aliwaeleza maofisa wa DCEA kuwa ameletewa mzigo kutoka Sri Lanka.

Shaweji alipotoa maelezo hayo, timu ya DCEA ilienda katika ofisi za NRM zilizopo katika jengo la Viva Tower na kufanya upekuzi na kisha kumalizia upekuzi wao nyumbani kwa mtuhumiwa huyo eneo la Masaki.

Katika upekuzi huo nyumbani kwa Shaweji walikuta kompyuta tano zikiwemo iPad, simu tatu, nakala za NRM, kadi tatu za Benki ya CRDB zenye majina ya watoto wake, hati mbili za kusafiria zenye jina la Shaweji na mke wake Mariam Shabani, pamoja na kitako cha bunduki aina ya Pump Action.

Baada ya upekuzi huo walimueleza mke wa Shaweji (Mariam), ambaye ni mtuhumiwa namba tatu katika kesi hii, aripoti ofisi za DCEA siku inayofuata.

Juni 4, 2025 Shaweji alichukuliwa maelezo ya onyo na kwamba alikiri kuwa kampuni yake ya NRM Group Company Limited iliingiza kontena lenye dawa za kulevya.

Pia alikiri kuwa wakati anafanyiwa upekuzi katika ofisi yake alimwambia mke wake ahamishie gari yake aina ya Range Rover na iPad, azipeleke kwa shemeji yake Juma Shebele eneo la Kiwalani, jambo ambalo mke wake alitekeleza.

"Baada ya taarifa hizo, timu hiyo ilienda hadi Kiwalani kwa shemeji yake Shaweji na kulikuta gari hilo likiwa limeegeshwa ndani ya uzio wa nyumba ya Shebele na kisha kufanya upekuzi na kulichukua pamoja na iPad na kurudi ofisi za DCEA," alidai.

Shahidi wa pili katika kesi hiyo, Augustino Mwakibete, yeye ni ofisa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambaye anafanya kazi katika yadi ya SSB ICD.

Washtakiwa wanadaiwa kuingiza shehena ya dawa za kulevya aina ya  Mitragyna Speciosa zenye uzito wa kilo 11,596, wakiwa chini ya ulinzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne

Katika maelezo yake, Mwakibete alidai Juni 17, 2025 akiwa katika Bandari Kavu ya SSB ICD, alipokea kontena hilo na kisha kuliongezea ulinzi kwa kufunga kamba maalumu ili lisiweze kufunguliwa.

Baada ya kulipokea, aliwajulisha maofisa wa DCEA na walimueleza kuwa asilipewe mtu yeyote mpaka watakapofika wenyewe.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 9, 2026 itakapoendelea kwa washtakiwa kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo kutokana na mshtakiwa mmoja (Hewage) kuugua.

Tayari Jamhuri imeshasoma maelezo ya mashahidi 11 wa upande wa Jamhuri na wamebaki 31.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa Julai Mosi, 2025 katika Bandari Kavu ya Said Salim Bakhresa (SSB ICD) iliyopo eneo la Sokota, Wilaya ya Temeke, kwa pamoja waliingiza sampuli zenye uhusiano na dawa za kulevya aina ya Mitragyna Speciosa zenye uzito wa kilo 11,596 sawa na tani 11.5.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuingiza dawa hizo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinyume cha sheria.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa Mahakamani hapo Agosti 5, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi.