Mahakama yatoa maagizo kesi ya 'vigogo wa MSD'
Watumishi wa Bohari ya Dawa (MSD) na Halmashauri wakiwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Maktaba
Muktasari:
- Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 37 yakiwemo ya wizi wa dawa na vifaatiba wakiwa watumishi, kuisababishia hasara MSD, kuongoza genge la uhalifu na kutakatisha fedha, matukio wanayodaiwa kuyatenda kati ya Julai 1, 2021 na Juni 30, 2025 katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Songwe, Dodoma na Singida.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa Jamhuri katika kesi ya wizi wa dawa na vifaa tiba inayowakabili watumishi sita wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD), kukamilisha upelelezi kwa wakati ili kesi hiyo iweze kuendelea na hatua nyingine.
Washtakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 7833 ya mwaka 2026 ni Mhasibu Mwandamizi, Suddi Abas (34), mkazi wa Kibamba Shule.
Wengine ambao wote ni wafamasia ni Petro Mdegela (42), mkazi wa Manga Veta; Rashid Hassan (34), mkazi wa Isyesye.
Vilevile yupo Edward Tengulaga (40), mkazi wa Manga Veta; Mfamasia wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba, mkoani Songwe, Jackson Mahagi (39) na Wema Mohamed (39) ambaye ni mfamasia wa Wilaya ya Singida na mkazi wa Mandewa.
Washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 37 yakiwemo ya wizi wa dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya Sh5.537 bilioni na kuisababishia MSD hasara ya Sh14.6 bilioni.
Maelekezo hayo yametolewa leo Jumatatu, Juni 22, 2026 na Hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube, wakati kesi hiyo ilipotajwa.
Hakimu Makube amefikia hatua hiyo muda mfupi baada ya upande wa utetezi kuhoji ni lini upelelezi wa kesi hiyo utakamilika.
Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Thawab Issa alieleza Mahakama kuwa upelelezi haujakamilika na kwamba wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Issa baada ya kutoa taarifa hiyo, mawakili wa utetezi Saburi Yakub na Isaya Mwanri, walidai tarehe iliyopita Jamhuri ilieleza Mahakama hiyo kuwa upelelezi upo katika hatua za mwisho kukamilika, hivyo waliomba kujua ni lini utakamilika.
"Kikao kilichopita Jamhuri ilieleza Mahakama kuwa upelelezi upo katika hatua za mwisho kukamilika, lakini leo wametueleza bado haujakamilika," alidai Yakub.
"Mheshimiwa Hakimu, washtakiwa hawa ni watumishi wa umma, walikamatwa tangu mwaka jana, hivyo kama upelelezi haujakamilika waachiwe kwa dhamana kwa sababu ni watuhumiwa wanaojulikana na ni watumishi, hivyo wanaweza kupatikana muda wowote wakihitajika," alidai.
Hakimu Makube baada ya kusikiliza hoja za pande zote, alikubaliana na ombi la upande wa utetezi na kuelekeza upande wa Jamhuri kukamilisha upelelezi kwa wakati ili kesi hiyo iweze kuendelea na hatua nyingine.
"Wakili wa Serikali, jitahidi ufikishe taarifa hii kwa viongozi wako, hatutaki kubeba lawama ambazo si zetu," alisema Hakimu Makube na kuahirisha kesi hiyo hadi Julai 6, 2026 kwa ajili ya kutajwa.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Aprili 13, 2026 na kusomewa mashtaka yanayowakabili.
Kati ya mashtaka 37 yanayowakabili washtakiwa hao, mashtaka 31 ni ya kutakatisha fedha; matatu ni ya wizi wakiwa watumishi; mawili ni kuisababishia mamlaka hasara na moja ni kuongoza genge la uhalifu.
Miongoni mwa mashtaka hayo ni la kuongoza genge, linalowakabili washtakiwa wote ambapo wanadaiwa kati ya Julai Mosi, 2021 na Juni 30, 2025 katika maeneo tofauti ya mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Songwe, Dodoma, Singida na maeneo mengine ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa makusudi waliongoza genge la uhalifu kwa kutenda kosa la wizi wakiwa watumishi.
Shtaka la pili ni wizi wakiwa watumishi, linalomkabili Abas, Mdegela, Hassan na Tengulaga, ambapo wanadaiwa kati ya Julai Mosi, 2021 na Juni 30, 2025 katika maeneo tofauti ya mikoa ya Dar es Salaam na Mbeya, wakiwa watumishi kwa vyeo vyao, kuiba dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya Sh2.695 bilioni, mali ya MSD, iliyofika mikononi mwao wakiwa waajiriwa.
Shtaka la tatu ni wizi linalowakabili Abas, Mdegela, Hassan na Mahagi. Katika siku na maeneo hayo, washtakiwa wanadaiwa kuiba Sh2.592 bilioni, mali ya MSD iliyofika mikononi mwao wakiwa waajiriwa.
Mashtaka mengine ni wizi, kuisababishia hasara mamlaka hiyo na kutakatisha fedha.