Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maisha, kifo cha Kamanda Abwao vyavuta hisia

Muktasari:

  • Kamanda, Richard Abwao alifariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam alikokuwa akiendelea na matibabu

Morogoro. Ilikuwa kama ndoto pale taarifa za majonzi zilipoifikia familia ya George Abwao, Juni 20, 2026, baada ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Richard Abwao, kufariki dunia.

Abwao, aliyefariki dunia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam alipokuwa akiendelea na matibabu, alikuwa kamanda wa polisi mwenye uzoefu wa miaka 27 kazini.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Juni 22, 2026, mdogo wake Manley Abwao amesema familia imepoteza mtu aliyekuwa mhimili.

"Pengo la kaka ni kubwa sana kwa familia. Alikuwa mzazi, mlezi na mshauri wetu. Ndiye aliyetuunganisha na kuhakikisha familia, inabaki pamoja, kuondoka kwake ni pigo ambalo si rahisi kuliziba," amesema.

Mama mzazi wa aliyekuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) na kamanda wa polisi mkoa wa Tabora, Richard George Abwao, Mary Abwao akiaga mwili wa mtoto wake aliyefariki dunia Juni 20 mwaka huu katika hospitali ya Muhimbili Dar es Salaam wakati wa tukio la kuaga nyumbani kwake marehemu Mji Mwema kata ya Tungi Manispaa ya Morogoro. Picha na Juma Mtanda.

Manley amesema hata alipojiunga na Jeshi la Polisi mwaka 1998, kaka yake alikuwa mwalimu na kielelezo katika utumishi.

"Alinifundisha mambo mengi kuhusu maisha na kazi. Alikuwa mtu wa watu, aliyependa umoja, aliyethamini undugu na aliyekuwa tayari kusaidia kila aliyemhitaji," amesema.

Safari ya Abwao ilianza Juni 23, 1975 katika Kijiji cha Kawawa, Wilaya ya Iringa. Alisoma elimu ya msingi katika Shule ya Bungo mkoani Morogoro kabla ya kujiunga na Shule ya Sekondari Kigurunyembe alikohitimu kidato cha sita mwaka 1996.

Baada ya kumaliza masomo yake, alijiunga na Jeshi la Polisi Tanzania mwaka 1998. Akiwa kazini, aliendelea kujiongezea ujuzi kwa kusoma Stashahada ya Juu katika Usimamizi wa Vyama vya Ushirika katika Chuo cha Ushirika Moshi na baadaye akasoma Stashahada ya Uzamili katika Usimamizi wa Biashara, Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).

Pamoja na mafunzo mbalimbali ya taaluma na uongozi, elimu ilimjengea msingi uliomwezesha kupanda ngazi za utumishi hadi kufikia Cheo cha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi mwaka 2024.

Mke wa aliyekuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) na kamanda wa polisi mkoa wa Tabora, Richard George Abwao, Anna Job akiaga mwili wa mume wake aliyefariki dunia Juni 20 mwaka huu katika hospitali ya Muhimbili Dar es Salaam wakati wa tukio la kuaga nyumbani kwake marehemu Mji Mwema kata ya Tungi Manispaa ya Morogoro. Picha na Juma Mtanda

Katika kipindi cha utumishi, Abwao aliwahi kuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Nyamwaga, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kishapu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu kabla ya kuhamishiwa Tabora mwaka 2021, alikohudumu hadi mauti yalipomkuta.

Ndani ya muda wake wa utumishi, ameacha historia, majonzi na kumbukumbu nyingi huku baadhi ya marafiki wakimtambua si kama polisi tu, bali mwanasoka mahiri, nahodha wa timu ya shule, aliyevaa jezi namba saba.

Akizungumzia maisha yake ya soka Kigurunyembe, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Mtatiro Kitinkwi aliyesoma naye, amesema alikuwa mchezaji tegemeo na mwenye kipaji kikubwa cha kuhamasisha wenzake.

"Alikuwa nahodha wa timu ya shule na alicheza vizuri sana, alikuwa mwenye ushawishi mkubwa kwa wenzake ndani na nje ya uwanja," amesema.

Baadhi ya askari wa jeshi la polisi wakitoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) na kamanda wa polisi mkoa wa Tabora, Richard George Abwao aliyefariki dunia Juni 20 mwaka huu katika hospitali ya Muhimbili Dar es Salaam wakati wa tukio la kuaga nyumbani kwake marehemu Mji Mwema kata ya Tungi Manispaa ya Morogoro. Picha na Juma Mtanda.

Katika timu hiyo walikuwamo pia wanafunzi ambao baadaye walikuja kuwa viongozi na watu maarufu katika nyanja mbalimbali, akiwamo Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, wanamuziki Joseph Haule maarufu Profesa Jay, Seleman Msindi maarufu Afande Sele, Ashton Balaigwa, Samuel Msuya na Mwenyekiti wa Morogoro Press Club, Nickson Mkilanya.

"Kama vipaji vya wakati ule vingekutana na mazingira ya sasa, wengi wangecheza soka la kulipwa katika vilabu vikubwa, lakini kila mmoja alichagua njia yake ya kulitumikia Taifa katika sekta tofauti," amesema Kitinkwi.

Rafiki yake wa karibu tangu walipokuwa wanafunzi Sekondari Kigurunyembe, Ramadhan Libenanga amesema Abwao alibaki kuwa yuleyule aliyemfahamu akiwa kijana wa shule.

"Richard alikuwa rafiki wa kweli. Kila alipokuwa akija Morogoro likizo au matembezi alinipigia simu. Tulikutana na kuzungumza kama zamani. Ukituona pamoja usingeamini alikuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa," amesema.

Waombolezaji wakiwa katika msiba wa aliyekuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Richard George Abwao aliyefariki dunia Juni 20 mwaka huu katika hospitali ya Muhimbili Dar es Salaam wakati wa tukio la kuaga nyumbani kwake marehemu Mji Mwema kata ya Tungi Manispaa ya Morogoro. Picha na Juma Mtanda.

Amesema hata alipokuwa akisafiri kwenda Tabora, Abwao alikuwa akimpokea kwa ukarimu na urafiki uleule alioujenga tangu ujana wao.

"Madaraka hayakumbadilisha. Alibaki mwenye upendo, mkarimu na aliyependa kuona marafiki na ndugu wanaendelea kushikamana. Tumeondokewa na rafiki wa kweli na pengo lake halitazibika kirahisi," amesema.

Londo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, ambaye pia alisoma naye Kigurunyembe amesema kifo cha Abwao si hasara kwa familia yake pekee, bali pia kwa Serikali na Jeshi la Polisi.

"Nilimfahamu tangu tukiwa wanafunzi, baadaye tukakutana tena akiwa katika utumishi wa Jeshi la Polisi. Alikuwa mtu mwenye mapenzi kwa wenzake, mnyenyekevu na aliyependwa na wengi. Ameacha pengo kubwa ambalo halitakuwa rahisi kuzibika," amesema.

Baada ya mwili wake kuagwa nyumbani kwake Mjimwema, Manispaa ya Morogoro leo Jumatatu Juni 22, 2026, umesafirishwa kupelekwa Shirati mkoani Mara kwa ajili ya mazimo yatakayofanyika Ijumaa Juni 26, 2026.