Majaji, mahakimu wanolewa misingi ya haki za binadamu Zanzibar

Muktasari:

  • Majaji na Mahakimu viziwani Zanzibar wamepewa mafunzo kuongeza uelewa kuhusu masuala ya kulinda na kutetea haki za binadamu hususani wanaposhughulikia kesi zinazohusu ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto.

Unguja. Majaji na Mahakimu viziwani Zanzibar wamepewa mafunzo kuongeza uelewa kuhusu masuala ya kulinda na kutetea haki za binadamu hususani wanaposhughulikia kesi zinazohusu ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto.

Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Mtandao wa Utetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), yanatajwa kuongeza uelewa na kuleta ufanisi katika kada hiyo inayosimamia utoaji wa haki na kutafsiri sheria.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo leo Jumamosi Novemba 27, 2021 Mratibu wa THRDC, Onesmo Ole Ngurumwa amesema mahakama ni sehemu ya utetezi na ulinzi wa haki za binadamu hivyo ni muhimu kuwa na kozi mbalimbali za kukumbushana kuhusu masuala hayo.

“Kwa kazi za majaji na mahakimu moja kwa moja ni watetezi wa haki za binadamu kwahiyo ni muhimu tukawa na utaratibu wa kukutana na kuangalia namna bora ya kuliendeleza hili kwasababu kuna mabadiliko mengi ya sheria yanafanyika kila mara,” amesema na kuongeza;

“Kwahiyo mafunzo haya ya siku mbili yanalenga kuwanoa na kuwakumbusha misingi mbalimbali ya haki za binadamu na maamuzi wanayoyafanya.”

Amesema njia pekee ya kutatua matatizo ya kijamii kwa kistaarabu na haki ni kwenda mahakamani maan ndicho chombo kinachotajwa na sheria kutenda haki hivyo ikishindwa kufanya hivyo inaweza kuongeza matatizo.

Naye Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Zanzibar, Salma Ali Hassan amesema suala la mitondoo katika magereza bado linatia aibu hivyo linatakiwa kushughulikiwa maana ni ukiukwaji wa haki za binadamu

“Pamoja na mtu kufungwa kuna haki zake zinapaswa kuzingatiwa lakini kusema kweli hili suala la mitondoo linapingana sana haki za abinadamu kwahiyo Zanzibar tunapaswa tubadilike mtu anatakiwa apate haja yake akiwa faragha,” amesema

Naye Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar, Khamis Ramadhan Abdallah amesema imani yake ni kwamba majaji na mahakimu hao wakimaliza mafunzo hayo wataongeza ufanisi katika utendaji kazi wao na kuleta mabadiliko katika usikilizawaji na maamuzi mbalimbali ya kesi hivyo kuwataka wawe makini wakati wa mafunzo hayo.

Mafunzo hayo ya siku mbili yameza leo na yanatarajiwa kukamilika kesho Jumapili Novemba 28, 2021.