Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Majaliwa aagiza ujenzi mji wa Serikali kukamilika Oktoba 2023

Muktasari:

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza ifikapo Oktoba, 2023 mradi wa majengo ya wizara mbalimbali unaoendelea katika mji wa Serikali uwe umekamilika.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza ifikapo Oktoba, 2023 mradi wa majengo ya wizara mbalimbali unaoendelea katika mji wa Serikali uwe umekamilika.

Majaliwa ameongeza kuwa kukamilika kwake ikiwa ni pamoja na kuwekwa samani ili azma ya Serikali watumishi wahamie katika majengo hayo ifika Januari Mosi mwaka 2024 itimie.

Taarifa iliyotolewa ofisi ya Waziri Mkuu kwa vyombo vya habari, imeeleza kuwa Majaliwa ametoa maagizo hayo leo Jumatatu Julai 3, 2023, baada ya kukagua ujenzi wa Mji wa Serikali na Uwanja wa Mashujaa, Mtumba jijini Dodoma.

Kiongozi huyo amewataka wanaotekeleza mradi huo, kuhakikisha wananunua bidhaa zinazozalishwa na viwanda vilivyopo nchini, ili kuokoa fedha za kigeni pamoja na kuongeza tija katika uwekezaji.

“Tafuteni mbinu za kiufundi za kukamilisha majengo haya kwa wakati bila kuathiri viwango ikiwa ni pamoja na kusimamia ujenzi huu usiku na mchana. Tunataka tumalize majengo haya, Watanzania wanataka kuona yakikamilika na kuanza kutumika.

“Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuhusu uwekezaji na amekuwa akialika wawekezaji wa nje na wa ndani kujenga viwanda vya bidhaa mbalimbali ikiwemo marumaru (tiles). Tutumie bidhaa zao badala ya kuziagiza nje ya nchi,” amesema Majaliwa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama amesema mbali na ujenzi wa majengo ya wizara, mradi mwingine wa uwanja wa Mashujaa unaendelea katika eneo hilo.

Mhagama amesema ujenzi wa uwanja wa Mashujaa na mnara utakaoongoza kwa urefu barani Afrika. Amefafanua kuwa mnara huo utakuwa na urefu wa mita 110.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Dk Jim Yonazi amesema watahakikisha wanasimamia kikamilifu ujenzi wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.