Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Majaliwa atoa maagizo kwa Ma-RC, DC 

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa wakati akizungumza na Kamati za Usalama za mikoa na wilaya pamoja na viongozi wa CCM wa mikoa kwenye kikao kazi alichokiendesha kwa njia ya mitandao (video conference) leo Jumatatu, Julai 22, 2024.

Muktasari:

  • Ameagiza miradi ikamilishwe kwa asilimia 90 ifikapo Desemba 2024 na kuhakikisha uzalishaji wa chakula unatosha.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Mikoa (RC) na Wilaya (DC) wasimamie miradi yote ya maendeleo kwenye maeneo yao kuhakikisha inakamilishwa ili ianze kutoa huduma kwa wananchi.

Majaliwa ametoa maagizo hayo leo Jumatatu, Julai 22, 2024, wakati akizungumza na Kamati za Usalama za mikoa na wilaya pamoja na viongozi wa CCM wa mikoa kwenye kikao kazi alichokiendesha kwa njia ya mitandao (video conference) kutokea ofisi ndogo ya Waziri Mkuu iliyoko Magogoni, jijini Dar es Salaam.

“Kwenye eneo la usimamizi wa miradi, wakuu wa mikoa hakikisheni mna taarifa za utekelezaji wa miradi hiyo, hii ni fursa yenu ya kujua benki tuliyonayo ya utekelezaji wa miradi yote ya tangu mwaka 2021.

“Angalieni ni miradi gani imepata fedha na mjiridhishe kama imekamilika au la, na kama bado haijakamilika, fuatilieni ni kwa nini haijakamilika,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu amesema miradi inayojengwa kwa fedha za Serikali kwenye halmashauri na manispaa ni mingi, hivyo amesisitiza ikamilishwe kwa asilimia 90 ifikapo Desemba, 2024 ili ianze kutumika mapema.

“Matumizi ya miradi hii, ndiyo faraja kwa wananchi na ndiyo matamanio yao,” amesisitiza.

Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwahimiza viongozi hao wafuatilie uzalishaji wa chakula, ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na ziada ya kutosha.

“Tanzania tumezalisha chakula kingi na tuna ziada, wakuu wa mikoa na wilaya ni jukumu lenu kusimamia kilimo na uzalishaji uwe umefikia malengo na wenye ziada. Pia fanyeni sensa ya kujua mazao ya kwenye maghala, uhifadhi wake ni mzuri na je kinatosha? Tuwe na takwimu za kutosha juu ya chakula tulichonacho kwenye hifahi yetu,” amesisitiza.

Wakati huohuo, Majaliwa amesisitiza makusanyo yote ya fedha kwenye halmashauri na manispaa ni lazima yaingizwe benki ndipo yapangiwe matumizi.

“Hata kama zi fedha za msaada kutoka kwenye taasisi au asasi zisiso za kiserikali, ni lazima DC ajue ili atoe taarifa kwa RC. Ma-RC wasimamie mtiririko wa fedha kwenye halmashauri.

“Suala la usimamizi wa mapato ya Serikali iwe ajenda ya kudumu. Tusipofanya hivyo, tutashindwa kutekeleza mipango yetu. Mmemsikia Rais wetu, Suluhu Hassan akisisitiza kuhusu ukusanyaji wa mapato, mapato ambayo baadaye yanaletwa kwenye maeneo yenu, ili kutekeleza miradi.”

Maeneo mengine aliyoyawekea msisitizo kwenye kikao hicho ni pamoja na utatuzi wa kero za wananchi, udhibiti na uhifadhi wa mazingira, nishati safi ya kupikia, ulinzi na usalama, kilimo cha umwagiliaji, magonjwa yasiyoambukiza, maandalizi ya AFCON 2027 na ushirikiano baina ya viongozi wa Serikali na wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kikao kazi hicho kilihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa.