Majaliwa atoa maagizo kwa MaDC, RC kuhusu sherehe za muungano

Muktasari:

  • Wakati sherehe za miaka 58 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar  zikitarajiwa kufanyika kitaifa mjini Dodoma Aprili 26, 2022, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kote nchini siku hiyo kuandaa shughuli za kufanya kwenye maeneo yao.


Unguja. Wakati sherehe za miaka 58 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar  zikitarajiwa kufanyika kitaifa mjini Dodoma Aprili 26, 2022, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kote nchini siku hiyo kuandaa shughuli za kufanya kwenye maeneo yao.

Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Aprili 24, 2022 wakati akifungua maonyesho ya maadhimisho hayo katika viwanja vya Maisara mjini Unguja, Zanzibar.

“Sherehe za mwaka huu zitakuwa tofauti, badala ya kwenda kufanya michezo uwanjani,  tutasherehekea kwa makongamano yanayotoa elimu kuhusu muungano, historia yake tulipotoka na tunapokwenda ili vijana waweze kuujua muungano kwenye nchi yetu.”

“Kwa hiyo tumeagiza wakuu wa mikoa na wilaya waandae shughuli za kufanya inaweza kuwa ya usafi masokoni, hospitali, shuleni na shughuli nyingine yoyote. Kila mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya wakusanye kwa pamoja wananchi waliopo kwenye maeneo yao kwa shughuli hiyo,” amesema.

Majaliwa amebainisha kuwa ipo kila sababu ya kujivunia na kusherehekea muungano huo ambao waasisi wake ni mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume.

Amesema katika ushirika wowote kwenye  maisha ya mwanadamu haukosi kuwa na changamoto na kwamba changamoto hizo huwa ni chachu ya kudumisha uhusiano.

“Katika muungano kumekuwa na hoja zinazolalamikiwa na pande zote mbili lakini  viongozi wetu wameendelea kusimama imara  kuhakikisha hoja hizo zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa maslahi mapana ya muungano wetu,” amesema.

Naye makamu wa pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla amesema viongozi wana kila sababu ya kuwaeleza Watanzania mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya muungano huo.

“Wazanzibari tunaendelea kunufaika na muungano kwa kiasi kikubwa, tutaendelea kuuenzi, kuheshimu, kuujali na kuzungumza vizuri kiuhalisia kwa maslahi ya Taifa letu,” amesema Abdulla.

Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo.