Majaliwa awataka ma-RC kutuma taarifa maadhimisho siku ya Ukimwi
Muktasari:
Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewapa siku 30 wakuu wa mikoa nchini kutuma taarifa za maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani kwa tume ya kudhibiti Ukimwi (Tacaids) sambamba na mafanikio yaliyopatikana.
Moshi. Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewapa siku 30 wakuu wa mikoa nchini kutuma taarifa za maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani kwa tume ya kudhibiti Ukimwi (Tacaids) sambamba na mafanikio yaliyopatikana.
Majaliwa ameeleza hayo leo Jumanne Desemba mosi, 2020 katika maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani ambayo kitaifa yamefanyika katika viwanja vya shule ya msingi Mandela manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
"Nitoe agizo kila Mkoa utoe taarifa yake ya mafanikio waliyoyapata katika maadhimisho haya kwa tume ya kudhibiti ukimwi ndani ya mwezi mmoja kuanzia sasa, na ifikapo Desemba 30 kila Mkoa utoe taarifa ikilenga maadhimisho haya na mafanikio yaliyopatikana,” amesema Majaliwa.
Katika maadhimisho hayo yenye kauli mbiu, ‘mshikamano wa kimataifa tuwajibike pamoja’, Majaliwa amesema, “serikali inathamini yale yote yanayofanywa katika kupambana na virusi vya Ukimwi hapa nchini, tunatambua mchango unaotolewa na wadau na marafiki ambao kila mmoja anajihusisha katika kutoa elimu juu ya maambukizi ya Ukimwi.”
“Maadhimisho ya siku ya ukimwi leo hapa Kilimanjaro ni sehemu ya utaratibu ambao tumejiwekea kila mwaka ,niendelee kusisitiza kwa wasimamizi wa maonyesho haya kuhakikisha kwamba yatafanyika kote nchini kwa ngazi za mikoa kila mwaka.”
"Halmashauri na hata vijiji navyo viendelee kuadhimisha na kwa kuwa kila agizo tulishalitoa kwa kila mkoa kuendelea kuadhimisha naomba nitoe agizo kila Mkoa utoe taarifa yake ya maadhimisho na mafanikio yaliyopatikana katika maadhimisho haya.”
Akizungumza kwenye maadhimisho hayo mratibu mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa Tanzania (UN), Zlatan Millisic amesema wataendelea kushirikiana na Tanzania kupambana na kuzuia maambukizi mapya, unyanyapaa pamoja na vifo vitokanavyo na Ukimwi.