Majanga tena, jengo laporomoka laua watano

Muonekano wa Mabaki ya jengo ghorofa lililoanguka katika Kijiji cha Sembeti, kata ya Marangu mashariki Wilaya ya Moshi Mkoa wa Kilimanjaro, nakusababisha Vifo vya vibaruwa 5 waliokuwa wakifanya kazi ya ujenzi wa jengo hilo. Picha na Dionis Nyato

Muktasari:

  • Ghorofa mbili zapanda kwa wiki tatu

Mosh. Ni majanga tena, ndivyo unavyoweza kuelezea tukio la kuporomoka kwa jengo la ghorofa ambalo ujenzi wake ulikuwa ukiendelea katika kijiji cha Sembeti Marangu Wilaya ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro na kusababisha vifo vya mafundi watano.

Taarifa za awali zinaeleza chanzo cha kuporomoka kwa jengo hilo la ghorofa mbili lilisababisha majeruhi tisa na mafundi wengine 16 wakiokolewa bila madhara ni ujenzi usiozingatiwa viwango na kujengwa kwa muda mfupi.

Mtaalamu wa majanga nchini, Mhandisi James Mbatia alisema hakuna lugha nzuri ya kuelezea tukio hilo zaidi ya uzembe katika mifumo ya ujenzi kuanzia mmiliki wa jengo, wahandisi na wasimamizi wa ujenzi wa jengo hilo.

“Ni uzembe kwa sababu mpaka ghorofa liporomoke ni lazima kuna kitu hakikufuatwa, iwe ni ubora wa nondo na uchanganyaji wa vifusi na kama kutoka ghorofa ya kwanza kwenda ya pili kulikuwa na muda wa kutosha.

“Mwaka 2006 kuna jengo liliporomoka kule Chang’ombe, Dar es Salaam na kuua watu wanne na Waziri Mkuu wakati huo akiwa Lowassa (Edward) alitoa maagizo watu wawajibishwe na kulitulia tulia kidogo, lakini tumerudi kule kule,” alieleza.

Mwaka 2013, jengo lingine liliporomoka katika mtaa wa Indira Gandhi, Dar es Salaam na kuua takribani watu 36 na kuporomoka kwa majengo hayo kulielezwa kulitokana na ujenzi usiozingatia utaalamu kama tukio jipya la Moshi lilivyo.


Tukio la Moshi lilivyokuwa

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi alisema uchunguzi wa awali unaonyesha jengo lilijegwa kwa muda mfupi na kulikuwa na mafundi 30 ambapo watano wamefariki dunia na tisa wamejeruhiwa.

Alisema jengo hilo lilikuwa likijengwa mchana na usiku, liliporomoka juzi usiku wakati kazi ya ujenzi ikiendelea na uchunguzi wa awali unaonyesha chanzo ni kutofuatwa kwa taratibu za ujenzi.

“Tulifanikiwa kupata miili minne ambayo ilipelekwa hospitali, lakini pia tuliokoa majeruhi tisa waliopelekwa hospitali kwa matibabu zaidi, hivyo mpaka asubuhi ya leo (jana) tuliokoa mwili mwingine na kufikia watano.

“Majeruhi tuliowakoa jana tumepata taarifa wanaendelea vizuri. Kazi inayoendelea sasa ni kukata zile nondo ambazo zilianguka na kile kifusi na kutoa matofali,” alisema na kuongeza:

“Kazi hii itatusaidia kujua kama kuna majeruhi wengine ama miili ambayo labda mtu aliingia bila kujulisha wasimamizi wa eneo hili ambao walikuwa wakisimamia ujenzi uliokuwa,” alisema Mkomagi.

Alisema taarifa za awali zinaonyesha jengo limejengwa kwa kipindi kifupi, kwamba ndani ya wiki tatu ghorofa mbili zilikuwa zimepanda, jambo ambalo kitaalamu lina shida.

“Naweza kusema ndani ya wiki tatu floor (ghorofa) mbili zimepanda na wakati wanatoa ile mirunda iliyokuwa inashikilia slab ile ya kwanza ili watengeneze slab ya pili ndio slab zote zikaporomoka,” alieleza ofisa huyo wa zimamoto.

Maelezo hayo yao yaliungwa mkono na Mhandisi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Lameck Benard aliyesema tayari wamechukua sampuli kwa ajili ya kufanya vipimo vya kimaabara.

“Sisi tunaangalia masuala ya utaalamu zaidi na masuala ya ujenzi huwezi ukayatolea taarifa kabla hujafanya vipimo. Kwa hiyo tumechukua sampuli za nondo, za kokoto na ule mchanganyiko zege, ili tukauangalie maabara.

“Lakini kwa hatua za awali hapa inaonyesha jengo limejengwa kwa muda mfupi. Baada ya vipimo tutakuwa na la kusema,” alisema Benard.


Manusura waeleza kilichotokea

Mmoja wa mahuhuda, Andrea Tarimo alisema jengo hilo liliporomoka saa 4 usiku wakati ujenzi ukiendelea na wananchi walifika haraka kuanza kuokoa watu na baadaye Zimamoto na Uokoaji nao walifika.

“Ilikuwa saa 4 usiku wakati kazi ya kumimina zege inaendelea, mimi nilitoka kidogo nilienda nyumbani kutafuta chakula nikiwa huko ndio nikasikia kishindo kikubwa, nikarudi mbio na mke wangu,” alisema Tarimo.

“Watu wakaanza kupiga mayowe ndio tukaona ghorofa limedondoka. Hatukukuta mtu juu watu wote walikuwa chini wamekandamizwa na kifisi kwa hiyo wananchi wakaanza kufanya jitihada za kuwaokoa watu walio hai na waliokufa.”

Kwa upande wake, fundi aliyenusurika, Valence Mrina alisema aliambiwa kuna kazi ya kumimina zege akaenda na walikuwa wakilipwa Sh20,000 kila mtu kwa siku.

“Kazi ya kumimina zege ilianza saa 5 asubuhi na mpaka saa 12 jioni kazi ilikuwa bado inaendelea. Tatizo lilitokea kwenye saa 4 usiku nilikuwa hapa chini nakoroga zege nikasikia kishindo, nikakimbia kutoka hapa ndio nikawa nasikia watu wanasema niokoeni niokoeni.

“Tuliokoa baadhi na wengine waliokolewa na Zimamoto ambao walikuja na kulikuwa na jirani alikuwa na greda alikuwa anapambana kuokoa watu tukishirikiana wote na wananchi wa jirani na vijiji pia jirani,”alieleza Mrina.

Jovin Mmbando, alieleza ilipofika saa nne kasoro usiku yalitokea mabishano, kwani walitaka walipwe fedha zao waondoke lakini walitakiwa kumaliza kazi kwanza ya kumimina zege.

“Kulitokea ubishani wa kupandisha zege, watu wakawa wanasema wamechoka na ni usiku tukapumzika dakika kadhaa na ilipofika saa nne watu wakakubali kurudi kuendelea kumalizia kazi.

“Ghafla tukasikia mlio kama mbao imevunjika, kila mtu akawa anajitetea na mimi nilihisi ngazi imedondoka, wakati nakimbia kifusi kikaniangukia na nikashindwa kutoka hadi nilipookolewa na sasa napata matibabu hospitali,” alisema.

Manusura mwingine, Mathias Kyara alieleza wakati wakimalizia kazi ili wapewe fedha zao ghafla walisikia kitu kimeanguka na waliokuwa pembeni walikimbia na kuokokewa, lakini waliokuwa katikati ndio walifukiwa na kufariki dunia.

Imeandikwa na Daniel Mjema, Janet Joseph na Florah Temba