Majeruhi wa Lucky Vicent waanza matibabu Marekani

Muktasari:

Wakati wanafunzi hao wakiwasili juzi usiku, shule hiyo, iliyokuwa imefungwa kwa wiki moja, jana ilifunguliwa huku wanafunzi wakifanyiwa utaratibu wa kusaidiwa na wanasaikolojia.

Dar/Arusha. Hatimaye wanafunzi watatu wa Shule ya Msingi ya Lucky Vicent waliojeruhiwa katika ajali ya gari iliyoua wenzao 32, walimu wawili na dereva, wamewasili nchini Marekani na sasa wamelazwa Hospitali ya Mercy Medical kwa matibabu zaidi.

Wakati wanafunzi hao wakiwasili juzi usiku, shule hiyo, iliyokuwa imefungwa kwa wiki moja, jana ilifunguliwa huku wanafunzi wakifanyiwa utaratibu wa kusaidiwa na wanasaikolojia.

“Ndege iliyowabeba watoto watatu na wazazi wao iliwasili Charlotte jioni ya Siku ya Mama (Duniani),” inasema taarifa ya Samaritan Purse iliyotumwa katika tovuti yao jana.

“Samaritan’s Purse imewaleta watoto watatu wa Kitanzania waliojeruhiwa vibaya, manusura pekee katika ajali ya basi iliyoua watu 35 na ambao hivi karibuni ilikuwa habari kubwa duniani na kwa Marekani. Watakuwa wakipata huduma maalumu katika hospitali ya mjini Sioux City, Iowa.

“Watoto wanapumzika vizuri katika kituo cha afya cha Carolinas na wanatarajiwa kuhamishiwa kituo cha Mercy pia cha mjini Sioux leo (jana).”

Makamu wa Rais anayeshughulikia mawasiliano ya Hospitali ya Mercy Medical, Dave Smetter jana alisema matibabu ya watoto hao ni bure.

Akiwa katika mahojiano na vituo mbalimbali vya televisheni nchini Marekani, Smetter alisema mara baada ya ndege iliyowachukua wanafunzi hao kuondoka nchini Tanzania na kufika Marekani, watoto hao watapata huduma maalumu kulingana na majeraha yao.

Smetter alikiambia kituo cha televisheni cha 4News (KTIV) kuwa watoto hao watakuwa huko kwa wiki mbili na zaidi kwa ajili ya matibabu.

Alisema watapata madaktari bora wa mifupa na kuhakikisha wanarudi katika hali ya kawaida bila kutozwa hata senti tano.

Alifafanua kuwa mfuko wa Samaritan ndiyo umegharamia safari ya watoto hao watatu, wazazi wao pamoja na madaktari kwenda na kurudi kwa ndege maalumu ya kubebea wagonjwa.

“Watapata matibabu ya kina ya majeraha waliyonayo na kwa kawaida majeraha na madhara waliyoyapata kwenye ajali hiyo matibabu yake kwa Tanzania humuacha muhusika akiwa hana baadhi ya viungo vilivyoathirika kwa kuvikata, ” alisema Smetter.

Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu ambaye amesaidia kupatikana kwa msaada huo alisema “hospitali kuu ya Mercy imekubali kuwapokea na kuwatibu hawa watoto wote bure. Kwa maneno mengine watatoa dawa, watatoa madaktari bingwa wa aina zote ikiwamo wa mifupa kwa kila mtoto.”

Shule yafunguliwa

Jijini Arusha, shule yao ya Lucky Vicent ya hapa imefunguliwa baada ya mapumziko ya wiki moja, ambayo wanafunzi walipewa baada ya ajali hiyo.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Ephraim Jackson alisema mwitikio umekuwa mkubwa kwa madarasa yote na wanafunzi wa darasa la saba wamefika 50 kati ya 71.

“Tumefungua leo (jana) na masomo yanaendelea kama kawaida. Walimu na wafanyakazi wasio walimu wanashirikiana kikamilifu. Pia ari ya kimasomo iko juu kwa sababu wanafunzi wanataka kufanya vizuri katika masomo yao,” alisema Jackson.

Katika hatua nyingine shule hiyo inapokea wataalamu wa Saikolojia ambao wapo tayari kuwasaidia ushauri nasaha wafanyakazi na wanafunzi.

Mwalimu mkuu msaidizi, Longino Nkana alisema watatoa nafasi kwa watalaamu hao kutoa ushauri utakaowawezesha wenye hofu kuwa kawaida na kuendelea na maisha kama awali.

Alisema kwa kuwa hawana chumba kikubwa ambacho kinaweza kuwahudumia wanafunzi wote, watakuwa wakipewa ushauri kwa makundi.