Makada Chadema washinda rufaa Mahakama Kuu

Ng'hulime Ilanga (kushoto) na mwenzake Katala Kikaja (kulia) wakiwa katika moja ya picha waliyopigwa wakiwa chini ya ulinzi huku wamefungwa pingu mkononi. Mpiga Picha Maalum.

Muktasari:

  • Makada hao walifungwa jela maisha kesi iliyotokana uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020.

Mwanza. Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga imewachiwa huru makada wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Katala Kikaja na Ng'hulima Lilanga waliohukumiwa kifungo cha maisha jela kwa makosa ya wizi, unyang'anyi wa kutumia silaha na ubakaji.


Uamuzi huo umetolewa leo Jumatano Novemba 16, 2022 na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Athuman Matuma baada ya kuridhika na hoja za warufani kuwa ushahidi uliowatia hatiani Aprili 12, mwaka huu, ulikuwa dhaifu, unaotia mashaka na usiokubalika mbele ya macho ya sheria.


Wana Chadema walitiwa hatiani kwa makosa mawili ya wizi, ubakaji, kuharibu mali na unyang’anyi wa kutumia silaha baada ya kukamatwa wakiwa kituo cha kupigia kura Kata ya Dutwa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu walikokuwa mawakala wa wagombea wa chama hicho kikuu cha upinzani katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020.


Pamoja na wizi wa Sh300, 000, warufani hao kwa pamoja walidaiwa kumbaka msadizi wa kituo cha kupigia kura ambaye jina lake lilihifadhiwa kulinda utu na heshima yake mbele ya jamii.


Tangu walipokamatwa siku ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020, kufikishwa mahakamani na kuhukumiwa kifungo Aprili 12, mwaka huu, warufani hao wamekaa mahabusu na gerezani kwa takribani miaka miliwi na miezi mitatu kutokana na shitaka la unyang’anyi wa kutumia silaha ambayo ni moja ya mashtaka yaliyokuwa yanawakabili kutokuwa na dhamana.


Hadi kuachiwa huru leo, warufani hao wametumikia takribani miezi saba ya adhabu yao katika magezeza ya Bariadi, Shinyanga na Butimba jijini Mwanza.

 Fuatilia mitandao yetu ya kijamii na gazeti la Mwananchi kesho kwa habari zaidi