Prime
Makali ya dola yang’ata tena kwenye mafuta
Dar/Mikoani. Unaweza kusema changamoto ya Dola ya Marekani imeng’ata tena baada ya bei ya mafuta kuongezeka kwa kiwango kilichoacha kilio kwa wananchi.
Uhaba wa dola katika mzunguko wa uchumi duniani umesababisha kupanda kwa thamani ya sarafu hiyo inayotumika katika miamala ya kimataifa kwa zaidi ya asilimia 85.
Thamani ya dola dhidi ya sarafu nyingi ambayo imekuwa ikipanda kwa siku za hivi karibuni, imetoka wastani wa Sh2,332 Agosti mwaka jana, lakini jana ilikuwa ikibadilishwa kwa Sh2,455.
Kwa kipindi cha mwaka mmoja ulioishia Mei, 2023 Tanzania ilitumia Dola 3.46 bilioni za Marekani (Sh8.34 trilioni) kuagiza bidhaa za mafuta na vilainishi nje ya nchi.
Miongoni mwa athari za dola ambazo tayari zimeonekana hapa nchini ni kuchelewa kwa malipo ya wakulima wa tumbaku ambao hulipwa kwa dola, lakini pia thamani ya sarafu ya nchi nyingi za Afrika imeshuka kutokana na utegemezi wao wa kununua bidhaa kutoka nje ya nchi.
Kumekuwa na ongezeko la bei ya bidhaa zinazonunuliwa kutoka nje ya nchi kwa kuwa zinahitaji dola na kwa jumla kumeibuka ugumu wa kufadhili na kufanya manunuzi ya bidhaa ambazo zinanunulia kwa dola.
Juzi, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) ilitangaza mabadiliko ya bei kikomo za mafuta ya petroli itakuwa Sh3,199 mwezi huu ikilinganishwa na Sh2,736 ya mwezi uliopita wa Julai.
Bei ya rejareja ya dizeli imeongezeka kwa Sh391, huku mafuta ya taa yakipungua kwa Sh161.
“Mabadiliko ya bei hizo yanatokana na changamoto za upatikanaji wa dola ya Marekani, mabadiliko ya sera za kikodi, kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola hiyo, ongezeko la gharama za mafuta katika soko la dunia na gharama za uagizaji wa mafuta,” ilieleza taarifa hiyo ya Ewura.
Bei hizo za rejareja kwa Mkoa wa Arusha zitauzwa Sh3,283, Kibaha (Sh3,204), Dodoma (Sh3,258), Geita (Sh3,364), Iringa (Sh3,263), Kagera (Sh3,415), Katavi (Sh3,357) na Kilimanjaro (Sh3,273).
Ramadhani Juma, dereva wa huduma za usafiri wa mtandaoni alisema mafuta yanapopanda ni changamoto kwenye mzunguko wa biashara, hivyo ongezeko la bei ndilo linaweza kuleta nafuu kwa madereva.
Mkazi wa Kikuyu, Asha Ndwata alisema katika kipindi kifupi kumekuwa na ongezeko la nauli, sasa kupanda huku tena kwa mafuta huenda kukaongeza tena gharama za usafiri.
“Tunamuomba Rais Samia Suluhu Hassan atusaidie, maisha yamekuwa magumu sana huku mtaani. Sasa tena bei ya mafuta imeongezeka hii ni shida kubwa,” alisema.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa), Priscus Joseph alisema kupanda bei ya mafuta ya petroli na dizeli kutaathiri gharama za maisha kutokana na usafirishaji wa bidhaa muhimu, ikiwamo mazao.
Alisema kwa basi linalofanya safari za mkoani ongezeko hilo la bei litasababisha kupoteza Sh100,000 hadi 250,000 na kuishauri Serikali na mamlaka kuangalia namna ya kupitia upya viwango vya nauli.
“Ongezeko la Sh400 kwa lita ni kubwa sana, Serikali na mamlaka zinazohusika liiangalie upya, lakini pia Rais ikiwezekana arudishe ilie ruzuku ya kila mwezi aliyokuwa anaitoa,” alisema Priscus.
Akizungumzia suala la kupanda kwa nauli, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), Salum Pazzy alisema, suala hilo lina vigezo vingi.
Alibainisha kuwa kiwango cha nauli kinachopangwa kinazingatia mambo mengi, ikiwemo bei ya vipuri, ununuzi wa magari pamoja hali usafirishaji.
“Kama wanahitaji mabadiliko ya nauli zipo taratibu za kufuata, mfano ukiangalia nauli ya daladala ilikaa kwa miaka tisa kutoka Sh400 hadi Sh500, hivyo tunapopanga bei mpya tunaangalia mambo mengi,” alisema Pazzy.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa), Elias Lukumay alisema kuongezeka kwa bei ya mafuta husababisha wasiwasi miongoni mwa Serikali nyingi kwa kuwa ni nishati inayoendesha uchumi.
“Pindi mafuta yanapopanda bei, gharama zetu za uendeshaji zinapanda na hata gharama za vitu vingine nazo zinapanda,” alisema Lukumay.
Pia, alisisitiza umuhimu wa mafuta katika usafiri na usafirishaji.
Alisema dizeli ni mafuta muhimu kwa usafirishaji wa bidhaa na petroli ni muhimu kwa usafirishaji wa watu.
Kutokana na ongezeko hilo la bei ya mafuta, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Usimamizi na Maendeleo ya Ujasiriamali, Dk Donath Olomi alisema kuna uwezekano mkubwa wa ongezeko hilo kuongeza mfumuko wa bei.
“Ongezeko la Sh463 kwa lita moja ya petroli na Sh391 kwa lita moja ya dizeli ni kubwa sana,” alisema Dk Olomi, ambaye ni mtaalamu wa uchumi na mbobezi wa biashara.
Alisema ongezeko la bei ya mafuta litaongeza bei ya usafirishaji, hivyo gharama za maisha zitakuwa juu, huku akishauri Serikali kuweka ruzuku kama ilivyofanya siku za nyuma.
Hata hivyo, alishauri nchi kuweka nguvu zaidi katika mabadiliko ya utegemezi wa nishati ya mafuta na sasa kuanza kukumbatia matumizi ya gesi asilia inayopatikana hapa nchini.
“Tunahitaji uwekezaji mkubwa katika gesi asilia kwa matumizi mbalimbali, kwa kuwa yenyewe ni nafuu kuliko mafuta na inapatikana hapa,” alisema Dk Olomi.
Wengine walificha
Kabla ya kutangazwa kwa bei mpya ya mafuta juzi, baadhi ya vituo vya mafuta katika maeneo tofauti vilikuwa vimeyaficha vikivizia mabadiliko ya bei ili viweze kupata faida kubwa zaidi.
Katika baadhi ya maeneo ya nchi kulikuwa na minong’ono na malalamiko ya wananchi kukosa mafuta, licha ya Ewura kudai kuwa kiwango cha mafuta kilichoingizwa nchini kilikuwa kinatosheleza mahitaji.
Hata hivyo, baadhi ya vituo vilikuwa haviuzi vikidai hayapo na wengi walikuwa wakiuza bei kubwa kinyemela.
Mkoani Tabora jana ilitangazwa kuwa lita 106,000 za mafuta aina ya dizeli zimekamatwa na maofisa wa Ewura katika kituo kimoja cha mafuta.
Meneja wa Ewura Kanda ya Magharibi, Walter Christopher alisema mafuta hayo yalikuwa kwenye kituo hicho kwa zaidi ya saa 24 pasipo sababu za msingi na wahusika kushindwa kutoa sababu zinazoeleweka.
“Katika kufuatilia madai ya upungufu wa mafuta tumebaini kuna ujanja unafanyika kama huu wa kuchelewesha magari yenye mafuta,” alisema Christopher kuhusu mafuta hayo yaliyokamatwa saa chache kabla ya mabadiliko ya bei.
(Imeandikwa na Kelvin Matandiko, Sharon Sauwa, Robert Kakwesi, Hawa Mathias, Fortune Francis na Fina Lyimo)