Makamba ataka wabunge wampe muda, katika katika ya umeme
Waziri wa Nishati, January Makamba akizungumza bungeni jijini Dodoma alipokuwa akichangia taarifa ya shughuli ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini toka Januari 2021 hadi Februari 2022. Picha na Edwin Mjwahuzi
Muktasari:
Waziri wa Nishati, January Makamba amewataka wabunge kumpa muda ili kutatua changamoto za kukatika mara kwa mara kwa umeme nchini.
Dodoma. Waziri wa Nishati, January Makamba amewataka wabunge kumpa muda ili kutatua changamoto za kukatika mara kwa mara kwa umeme nchini.
Makamba ameyasema hayo wakati akijibu hoja zilizotolewa na wabunge wakati taarifa ya shughuli za Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kwa kipindi cha Januari 2021 hadi Februari 2022 ilivyowasilishwa bungeni.
Makamba amesema kimataifa inapaswa kutengwa asilimia 10 hadi 12 ya pato ghafi ya shirika kama hilo kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu.
Amesema mwaka jana Tanesco ilipata mapato ya Sh1.8 trilioni maana yake fedha ya ukarabati zilikuwa zinatakiwa ziwe ni Sh180 bilioni.
Akawauliza wabunge kama wanafahamu ni kiasi gani kilichotengwa kwa muda wa miaka 10 iliyopita kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya shirika hilo.
Amesema jitihada mbalimbali zinafanywa kukabiliana na changamoto hiyo ikiwemo kutengeneza mradi mkubwa wa dola bilioni 1.9 wakuimarisha vituo vya umeme (up grade sub station) ili kuhakikisha kuwa umeme uko sawa (stable) kwenye gridi ya Taifa.
“Hatutaki kusema haya maneno sana, sisi tunaomba mtupe muda. Mheshimiwa Waziri aliyenitangulia (Dk Medard Kalemani) alikaa miaka minne alifanya kazi nzuri, mimi nina miezi minne na tuombe na mimi nipate miaka minne,”amesema.
Amesema Rais John Magufuli pia alikaa katika nafasi ya urais kwa miaka na Rais Samia Suluhu Hassan ndio kwanza ana mwaka mmoja tangu aingie madarakani.
Makamba aliwaomba wabunge wamwombee kwa Mungu Rais Samia naye aipate miaka hiyo ya uongozi na kwamba kwa miaka hiyo hawatakuja kuzungumza changamoto hiyo.
“Kwa hiyo tuvumiliane, tupeane muda, maneno ya kushambuliana binafsi yanasikitisha kwamba waziri kapanda helkopta kaweka hivi na hivi. Hii siyo sifa ya mbunge, hatuko hapa kutupiana mawe.
Hii ni meli yetu wote nikifeli mimi imefeli nchi, akifeli Rais imefeli nchi. Kama una matatizo na ya mheshimiwa Rais ama mimi kuwa waziri tutafute jambo jingine sio mambo ya nchi,”amesema.
Akizungumzia mradi wa kufua umeme wa maji wa Mwalimu Julius Nyerere, Makamba amesema alipoingia wizarani aliomba taarifa ya mradi ambapo aliambiwa kuwa mradi huo umechelewa kwa siku 177.
“Nikawauliza mbona mtaani hatujui, wabunge wanajua, Watanzania wanajua wakajibu kuwa hawajui. Kwa hiyo kazi yangu ya kwanza nilikwenda katika kamati (Nishati na Madini) kueleza kwa nini umechelewa. Sasa leo linatupwa kama zigo langu,”amesema.
Amesema changamoto za uchelewaji wa mradi huo zinatokana na kubadilishwa kwa mfumo wa mradi ambapo hivi sasa unasimamiwa kwa ukaribu kuliko ambavyo umewahi kusimamiwa.
“Siku zote jukumu letu ni kuhakikisha kuwa mradi huu unaisha ukiwa salama na ukiwa imara na ndicho tunafanya,”amesema.
Mwisho