Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makete kuongeza tija uzalishaji wa viazi mviringo

Shamba la viazi mviringo likionyesha kunawiri kutokana na kufuata njia bora za kilimo cha zao hilo.

Muktasari:

  • Wilaya ya Makete ni moja ya wilaya zilizobarikiwa kuwa na ardhi yenye uwezo mkubwa wa kuzalisha viazi mviringo lakini changamoto ya maji imeendelea kuathiri uzalishaji licha ya jitihada za halmashauri hiyo kuboresha kilimo hicho.

Njombe. Halmashauri ya Wilaya ya Makete mkoani Njombe imejipanga kuongeza tija katika uzalishaji wa kilimo cha viazi mviringo kwa kuweka mkazo kwenye mifumo ya umwagiliaji, ili kukabiliana na changamoto ya ukame inayowakumba wakulima wengi.

Hayo yamebainishwa leo Novemba 18, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Jerry Daimon wakati akizungumza na waandishi wa habari wilayani humo.

Amesema Wilaya ya Makete ni moja ya wilaya zilizobarikiwa kuwa na ardhi yenye uwezo mkubwa wa kuzalisha viazi mviringo lakini changamoto ya maji imeendelea kuathiri uzalishaji, licha ya jitihada za halmashauri hiyo kuboresha kilimo hicho.

Amesema halmashauri hiyo ina mpango wa kuboresha miundombinu ya umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji wa viazi mviringo na kufanya hivyo kutasaidia kuondoa changamoto kwa wakulima wilayani humo.

“Mfano, sasa hivi tunazungumzia hali ya mvua ambayo haieleweki lakini tukishakuwa na miradi ya umwagiliaji, tutakuwa tumempa uhakika yule mwananchi wa lini alime na kuwa na uhakika wa kuchagua,” amesema Daimon.

Amesema mwaka jana halmashauri ya Wilaya ya Makete ililima hekta 18,000 za viazi mviringo na kufanikiwa kuzalisha zaidi ya tani 390 za zao hilo.

Mjiorojia kutoka Bodi ya Maji, Hamisi Sangoda ambaye ni moja ya wataalamu kutoka Bonde la Maji la Ziwa Nyasa, amesema wamefanya utafiti katika vijiji vya Malembuli na Ibaga, kata ya Mang'oto ili kubaini maeneo sahihi ya kuchimba visima vitakavyowezesha kilimo cha umwagiliaji kuendelea kwa mwaka mzima.

“Kazi inayoendelea hapa ni utafiti wa maji chini ya ardhi kwa ajili ya uchimbaji wa visima vya umwagiliaji,” amesema Sangoda.

Naye Mhandisi wa Umwagiliaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete, Ahamad Kichumbaki amesema endapo miradi ya maji iliyopendekezwa itatekelezwa kikamilifu ndani ya wilaya hiyo, wakulima watafanya uzalishaji wa misimu miwili na kuongeza mapato ya kaya pamoja na halmashauri hiyo.

“Vilevile, tutakuwa na chanzo kimoja cha maji ya mto, nacho kitasaidia katika kumwagilia mashamba kwenye eneo hili,” amesema Kichumbaki.

Mkulima wa viazi kutoka Kijiji cha Malembuli, Japhet Sanga amesema hadi kufikia mwaka 2024/2025, zaidi ya Sh1.9 bilioni zimekusanywa kupitia ushuru wa viazi, lakini sehemu ya wakulima wameshindwa kunufaika kutokana na uhaba wa maji kwenye maeneo ya uzalishaji.

“Watu wanategemea mvua, kwa hiyo tukipanda mazao yetu kwa mwaka mvua inanyesha kwa baadhi ya maeneo, hivyo inatupa changamoto kutegemea mvua katika uzalishaji,” amesema Sanga.