Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makonda ampa Mavunde saa 24 kufika Geita

Muktasari:

  • Waziri wa Madini, Anthony Mavunde atakiwa kufika Geita kesho kutatua changamoto ya mgogoro wa mipaka ya vijiji nane, mwenyewe asema leo usiku atafika katika mkoa huo.

Geita. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda amesema akiondoka mkoani Geita kesho apishane na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde atakayekwenda kutatua mgogoro wa mpaka kati ya wananchi wa vijiji nane na mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM).

 Hata hivyo, Mavunde amemueleza Makonda kwa simu kwamba leo Jumamosi usiku atatua mkoani Geita kushughulikia mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu, huku akisema maelekezo ya chama hicho tawala lazima yatekelezwe.

Makonda ameeleza hayo leo Jumamosi Novemba 11, wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Nyankumbu katika mwendelezo wa ziara yake ndani ya Geita akitokea Kagera.

Kiongozi huyo amesema huwezi kwenda Mkoa wa Geita ukaacha kuzungumzia masuala madini kwa sababu ndio yanayogusa uchumi wa wananchi na mkoa huo sambamba na mgogoro wa mipaka wa wananchi wa vijiji nane.

"Utajiri Geita Mungu aliuweka katika dhahabu iliyopo chini ya ardhi hapa na wakazi wa mkoa huu ni wanufaika," amesema Makonda.

Baada ya maelezo hayo, Makonda alimpigia simu Mavunde kumweleza kuwa leo wakati akipata chakula cha mchana alifuatwa na mmoja wa wazee akimuomba kuingilia kati suala la mgogoro wa mpaka baina yao na GGM uliohudumu kwa miaka zaidi ya 20.

"Sasa maelekezo ya chama kesho (Jumapili) naondoka Geita, nipishane na wewe ukiwa unaingia Geita," amesema Makonda akizungumza na Mavunde kwa simu huku wananchi wakimsikiliza.

Baada ya maelezo yao Mavunde amemjibu mwenezi huyo akisema anautambua mgogoro huo na Rais Samia alitoa maelekezo ya kupatiwa ufumbuzi wa suala hilo. Amesema mwezi uliopita alikuwa mkoani Geita kuzungumza na wananchi wa vijiji vyote.

"Niliwaahidi kuwa ndani ya mwezi mmoja nitarudi kuwapa mrejesho kesho nitafanya kikao. Niseme kwa maelekezo yako leo nitakuwa Geita," amesema Mavunde.

Katika hatua nyingine, Makonda amewaambia wananchi wa Geita kuwa yeyote anayempinga Rais Samia Suluhu Hassan basi atakuwa anampinga hayati John Magufuli ambaye alimwamini na kuwa makamu wake wa Rais.

"Naomba kutoa tangazo rasmi kama mtoto wa kanda ya ziwa Rais Samia ni dada yenu, shangazi yetu, mama yetu na bibi yetu na tuna jukumu kanda ya ziwa kumshika mkono na kumuunga mkono," amesema Makonda.


Atinga na baiskeli

Kama iliyo kawaida yake kutinga na usafiri tofauti katika mikutano yake ya hadhara, ambapo leo hii ametinga na baiskeli aliyokuwa akiendesha na wananchi wa Geita alioambatana nao kwenda Uwanja wa Nyankumbu. Juzi akiwa Kagera alitumia bajaji, jana farasi leo baiskeli.