Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Makosa ya jinai yashuka, uhalifu wa mtandao wapaa

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mwaka wa fedha 2026/2027 Bungeni jijini Dodoma. Picha na Said Khamis.

Muktasari:

  • Amesema kupungua kwa makosa ya jinai kunatokana na kuongezeka kwa uelewa na ushirikiano wa jamii katika kubaini na kuzuia uhalifu. Kati ya makosa hayo, 9,603 ni makosa dhidi ya binadamu, 13,986 ni makosa dhidi ya maadili ya jamii, 14,794 ni makosa dhidi ya mali, huku makosa 644 yakiwa ya uhalifu wa kifedha.

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi amesema jumla ya makosa makubwa ya jinai 39,027 yaliripotiwa katika vituo vya polisi nchini kati ya Julai 2025 hadi Aprili 2026.

Katambi amesema hayo leo Jumatatu, Mei 25, 2026 wakati akiwasilisha bungeni jijini Dodoma bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2026/27.

Amesema idadi hiyo imepungua ikilinganishwa na makosa 40,022 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2024/25.

Amesema kupungua kwa makosa hayo kunatokana na kuongezeka kwa uelewa na ushirikiano wa jamii katika kubaini na kuzuia uhalifu.

Kati ya makosa hayo, 9,603 ni makosa dhidi ya binadamu, 13,986 ni makosa dhidi ya maadili ya jamii, 14,794 ni makosa dhidi ya mali, huku makosa 644 yakiwa ya uhalifu wa kifedha.


Uhalifu wa kimtandao

Katambi amesema katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026, makosa ya uhalifu wa kimtandao yaliyoripotiwa katika vituo vya polisi yaliongezeka kutoka 748 mwaka 2024/25 hadi 1,323 mwaka 2025/26.

Amesema ongezeko hilo limetokana na matumizi ya vifaa vya kisasa vya uchunguzi, kuongezeka kwa operesheni na doria mtandaoni pamoja na mwitikio mzuri wa wananchi katika kutoa taarifa kuhusu uhalifu wa mtandao.

Kwa mujibu wa Katambi, katika mwaka wa fedha 2026/27, Wizara kupitia Jeshi la Polisi itaendelea kudhibiti uhalifu wa kimtandao, ikiwemo matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na udukuzi wa taarifa, kwa kuanzisha ofisi za kanda za upelelezi wa makosa hayo katika Jiji la Dodoma na Zanzibar.

Amesema wizara itaweka mifumo ya ufuatiliaji wa mashambulizi ya kimtandao, kuimarisha kikosi maalumu cha kudhibiti taarifa potofu na uchochezi mtandaoni, kutoa elimu kwa umma kuhusu athari za kusambaza taarifa za uongo pamoja na kufuatilia na kudhibiti akaunti hatarishi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Katambi amesema Jeshi la Polisi limeendelea kutekeleza programu maalumu za mafunzo kwa maofisa, wakaguzi na askari ili kuwawezesha kukabiliana na aina mpya za uhalifu, ikiwemo uhalifu wa mtandaoni.

Amesema hadi Aprili 2026, jumla ya maofisa, wakaguzi na askari 157 walikuwa wamepata mafunzo ya uchunguzi wa makosa ya kimtandao, sayansi ya uchunguzi wa alama za vidole na uchunguzi wa hati zenye mashaka.

Pia walipata mafunzo ya uchambuzi wa tabia za wahalifu, uchunguzi wa kisayansi wa vifaa vya kielektroniki, usimamizi wa masuala ya kiusalama wakati wa majanga, kupambana na ugaidi wa kimataifa pamoja na mbinu za uchunguzi wa kisayansi. Mafunzo hayo yalitolewa katika nchi za Brazil, India, Uturuki, Korea Kusini, Misri na Urusi.


Operesheni za kudhibiti

Katambi amesema katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026, Jeshi la Polisi lilifanya operesheni mbalimbali za kudhibiti uhalifu nchini na kufanikiwa kukamata silaha 187 pamoja na risasi 196.

"Silaha zilizokamatwa ni pamoja na shotgun 45, bastola sita, rifle 10, Mark IV nne na magobole 122. Jumla ya watuhumiwa 169 walikamatwa na kufikishwa mahakamani, huku kesi zao zikiendelea kusikilizwa," amesema.

Ameongeza kupitia operesheni hizo, nyara za Serikali 3,618 zenye uzito wa kilogramu 99,642 na gramu 94 zilikamatwa. Watuhumiwa 1,175 walifikishwa mahakamani na kesi zao zipo katika hatua mbalimbali.


Usalama Barabarani

Katambi amesema jumla ya madereva 3,051,541 waliokiuka sheria za usalama barabarani walikamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kupewa onyo, kutozwa faini, kufikishwa mahakamani na kufungiwa leseni.

Amesema Jeshi la Polisi limeendelea kushirikiana na wadau wa usalama barabarani kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya barabara kupitia vyombo vya habari, shule za msingi na sekondari, vituo vya maegesho ya pikipiki na bajaji pamoja na vituo vya mabasi.

Hata hivyo, amesema takwimu zinaonyesha matukio ya ajali za barabarani yaliyoripotiwa katika vituo vya polisi yamepungua kutoka 1,322 katika kipindi cha Julai 2024 hadi Aprili 2025 na kufikia matukio 1,233 katika kipindi kama hicho mwaka 2025/26.

"Katika ajali hizo, watu 1,066 walipoteza maisha ikilinganishwa na watu 1,275 waliokufa katika kipindi kama hicho mwaka 2024/25, sawa na upungufu wa asilimia 16.4. Aidha, watu 1,869 walijeruhiwa ikilinganishwa na 2,278 waliojeruhiwa mwaka uliopita, ikiwa ni upungufu wa asilimia 18," amesema.

Katambi amesema katika mwaka wa fedha 2026/27, Wizara kupitia Jeshi la Polisi itaendelea kuimarisha usimamizi wa sheria za usalama barabarani kwa kufanya doria na kuchukua hatua dhidi ya wanaokiuka sheria hizo.

Amesema wizara itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuhusu matumizi sahihi ya barabara kwa mujibu wa sheria, hatua ambazo zinalenga kuimarisha usalama barabarani nchini.