Malori ya mafuta yanaswa na lita 66,048 za kemikali bashirifu
Mapipa yenye kemikali bashirifu zilizoingizwa nchini na kusafirishwa kinyume cha taratibu. Uchepushwaji wa kemikali hizo huusishwa na utengenezaji wa dawa za kulevya.
Muktasari:
- Kemikali zilizokamatwa ni lita 16,048 za cyclohexanone pamoja na lita 50,000 za Extra Neutral Alcohol (ENA), huku magari hayo mawili yakihusika katika usafirishaji huo.
Dar es Salaam. Malori mawili yaliyopaswa kusafirisha mafuta ya petroli yamekamatwa jijini Dar es Salaam yakiwa yamebeba shehena ya kemikali bashirifu zinazodaiwa kuingizwa nchini na kusafirishwa kinyume cha sheria.
Malori hayo yalikamatwa katika operesheni maalumu iliyofanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambapo jumla ya lita 66,048 za kemikali bashirifu zilizokuwa zikisafirishwa katika mazingira ya kutatanisha.
Kemikali zilizokamatwa ni lita 16,048 za cyclohexanone pamoja na lita 50,000 za Extra Neutral Alcohol (ENA), huku magari mawili yaliyohusika katika usafirishaji huo yakishikiliwa pamoja na watuhumiwa wawili waliokamatwa.
Mojawapo ya lori la mafuta lililokamatwa likiwa limebeba kemikali bashirifu zinazotumika kutengeneza dawa za kulevya.
Kamishna Jenerali DCEA, Aretas Lyimo amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa kemikali hizo zilikuwa zikisafirishwa kwa kutumia magari ya kubeba mafuta ya petroli aina ya Scania huku vibali vya kughushi vikidaiwa kutumika kufanikisha usafirishaji huo.
Amesema matumizi ya magari ya mafuta kusafirisha kemikali zinazotumika kwa matumizi ya binadamu yanaweka maisha ya wananchi hatarini kutokana na uwezekano wa uchafuzi wa kemikali na madhara makubwa kiafya.
Mbali na ukiukwaji wa sheria za usafirishaji wa kemikali, Lyimo amesema mazingira ya ukamataji huo yanaashiria uwepo wa mtandao wa kihalifu wenye nia ya kuzichepusha kemikali hizo kwenda katika utengenezaji wa dawa za kulevya kwenye maabara bubu.
Amesema kemikali aina ya cyclohexanone ni miongoni mwa zinazotumika kutengeneza dawa za kulevya aina ya Phencyclidine (PCP), maarufu kwa kusababisha madhara makubwa ya akili na tabia kwa watumiaji.
“Matumizi ya PCP yanaweza kusababisha mtu kupoteza fahamu, kuchanganyikiwa, kuwa mkali kupita kiasi, kupata degedege, matatizo ya akili ya kudumu na hata kifo kutokana na matumizi ya muda mrefu au kiwango kikubwa,” amesema.
Lyimo amebainisha kuwa lita 16,048 za cyclohexanone zilizokamatwa zingeweza kuzalisha tani 11.4 za dawa hizo za kulevya, kiwango ambacho kingeweza kusambaa katika maeneo mbalimbali nchini na kuathiri maelfu ya vijana.
“Kwa kuwa kilo moja ya kemikali hizi huweza kuzalisha takribani gramu 750 za dawa za kulevya aina ya PCP, kiwango kilichokamatwa kingekuwa hatari kwa jamii endapo kingefanikiwa kuingia sokoni,” amesema.
Aidha, amesema uchunguzi umebaini kuwa kemikali za cyclohexanone ziliingizwa nchini na kampuni ya Kinglion Investment LTD bila kufuata matakwa ya sheria ikiwemo kupata vibali kutoka mamlaka husika.
Kwa upande wa kemikali aina ya Extra Neutral Alcohol (ENA), amesema zilikuwa zikitoka katika kampuni ya Maranile Group Limited iliyopo Kibaha mkoani Pwani kabla ya kukamatwa zikiwa safarini.
Katika operesheni hiyo, mamlaka ilimkamata Bakira Abel Zacharia (44), mkazi wa Dar es Salaam, aliyekuwa dereva wa gari lenye tela lililokuwa limebeba lita 30,000 za kemikali hizo.
Pia, Vicent Stephen Rashid (26), mkazi wa Mbeya, alikamatwa akiwa dereva wa gari lenye tela lililokuwa limebeba lita 20,000 za kemikali hizo.
Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani Sura ya 182, usafirishaji wa kemikali unahitaji vibali maalumu vya kuingiza na kusafirisha, huku matumizi ya vibali vya kughushi au kutoa taarifa za uongo kuhusu matumizi ya kemikali hizo yakitajwa kuwa kosa la jinai.
Sambamba na operesheni hiyo, mamlaka pia imefanya misako katika mikoa ya Dodoma, Mtwara, Njombe, Ruvuma, Kilimanjaro, Arusha, Dar es Salaam, Morogoro na Mwanza ambapo tani 5.733 za bangi, tani 1.67 za mirungi, gramu 48.23 za heroini na gramu 113.35 za kokeini zimekamatwa.
Operesheni hizo pia zimehusisha uteketezaji wa ekari 38.5 za mashamba ya bangi pamoja na kukamatwa kwa magari manne na pikipiki 14 zilizokuwa zikihusishwa na biashara hiyo haramu, ambapo pia watuhumiwa 84 wakikamatwa kuhusiana na matukio hayo.
Aonya vijana kukosa ajira
Katika hatua nyingine Kamishna Jenerali Lyimo amewaonya vijana hususani wanafunzi wa vyuo vikuu kuachana na matumizi ya dawa za kulevya kutokana na hatari ya kukosa ajira, hasa katika vyombo vya dola ambako Serikali imeanza kuwafanyia vipimo waombaji wote kabla ya kuajiriwa.
Lyimo amebainisha kuwa baadhi ya vijana wanaingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya kutokana na ushawishi wa makundi na mitindo ya maisha inayowapotosha, hali inayoweza kuathiri mustakabali wao wa ajira na maisha kwa ujumla.
Amesema mkakati unaendelea ndani ya vyombo vya dola kwa kupima afya za waombaji kazi kabla ya kuajiriwa ili kubaini wanaotumia dawa za kulevya.
“Tunapobaini mtu anatumia dawa za kulevya maana yake ajira yake imeishia hapo. Ndiyo maana tunatoa wito kwa vijana, hasa wa vyuo vikuu, waachane na matumizi ya dawa hizo,” amesema.
Kuhusu ambao tayari wako kazini amesema, “Tumebaini hata baadhi ya watumishi wa Serikali wanatumia dawa za kulevya. Tumeanzisha mpango kabambe wa kuhakikisha yeyote anayebainika anachukuliwa hatua za kisheria na za kiutumishi zinafuatwa,” amesema.
Mojawapo ya lori la mafuta lililokamatwa likiwa limebeba kemikali bashirifu zinazotumika kutengeneza dawa za kulevya.
Lyimo amesema Serikali inalenga kujenga jamii yenye nguvu kazi imara, inayofanya kazi kwa bidii na kuchangia ukuaji wa uchumi bila kuathiriwa na matumizi ya dawa za kulevya.
“Matumizi ya dawa hizo yamekuwa changamoto kubwa inayoharibu nguvu kazi ya taifa na tayari mamlaka imeanza operesheni katika miji mikubwa nchini kwa lengo la kuvunja vijiwe vinavyojihusisha na utumiaji wa dawa hizo,” amesema Lyimo.