Mama amuua mtoto wake kwa kumkata na shoka

Wednesday September 15 2021
auwawapic
By Seif Jumanne

Njombe. Jeshi la polisi mkoani Njombe, linamshikilia Vaileth Chaula (30) mkazi wa kijiji cha Mkongomi kata ya Kidugala wilayani Wanging'ombe kwa kosa la kumuua mtoto wake kwa kumkatakata na shoka kichwani.

Kamanda wa polisi mkoa wa Njombe Hamisi Issah amesema kwa mujibu wa maelezo ya wanandugu mwanamke huyo alikuwa na matatizo ya akili.

Amesema miezi michache iliyopita mwanamke huyo akiwa Makambako alipokuwa ameolewa  alipatwa na matatizo ya akili na kurudishwa nyumbani kwao kwa wazazi wake ili apatiwe matibabu.

Amesema akiwa na mtoto huyo ambaye alionekana kumdekea mama yake huyo aliona kuwa anasumbuliwa hivyo alichukua shoka na kumkatakata mtoto huyo.

"Huo ni ukatili ingawa huyu mama ni mgonjwa lakini sasa sheria haisemi namna hiyo" amesema Issah.

Amesema mwanamke huyo anashikiliwa na jeshi la polisi wakisubiri kukamilika kwa baadhi ya mambo ili wamfikishe mahakamani.

Advertisement

Katika hatua nyingine mwanafunzi wa kidato cha sita shule ya sekondari Mwakavuta iliyopo wilayani Makete Ndenja Ng'wale amejinyonga kwa kutumia kamba za manila katika mtaa wa Sido Njombe mjini.

Amesema mwanafunzi huyo alirudi nyumbani kwa ruhusa kutoka shule aliyokuwa anasoma kutokana na kuumwa jino na alikwenda kwa shangazi yake kupata matibabu lakini baadae alianza kuumwa na tumbo na kutapika.

"Hatujui kama marehemu alikuwa na msongo wa mawazo au alipatwa na kitu gani kwakuwa alichukua sturi na kamba ya manira na kujinyonga kwenye kenchi ya nyumba hiyo hadi kufa" amesema Issah.

Kamanda Issah amesema matukio ya kujinyonga hadi kufa yanazidi kushamiri hivyo ni vema familia zikawaangalia watu wao na kuwapa ushauri nasaha ili wasifanye vitendo hivyo.

Advertisement