Mambo kumi yaliyotikisa msiba wa Rais Magufuli

Muktasari:
- Siku mbili baada ya maziko ya Rais wa Tano, John Magufuli yaliyofanyika wilayani Chato Mkoa wa Geita, kuna mambo 10 yaliyotokea tangu siku aliyoaga dunia hadi alipohifadhiwa katika nyumba yake ya milele, mengine yakibaki kuwa historia na simulizi kila kona.
Dar es Salaam. Siku mbili baada ya maziko ya Rais wa Tano, John Magufuli yaliyofanyika wilayani Chato Mkoa wa Geita, kuna mambo 10 yaliyotokea tangu siku aliyoaga dunia hadi alipohifadhiwa katika nyumba yake ya milele, mengine yakibaki kuwa historia na simulizi kila kona.
Kiongozi huyo alifikwa na umauti akiwa madarakani Machi 17 mwaka huu na mazishi yake yalifanyika Machi 26.
Siku mbili baada ya kifo aliyekuwa makamu wake, Samia Suluhu Hassan aliapishwa na kuwa kiongozi mkuu wa nchi.
Wengi wamuaga, wafa
Machi 20 na 21, wananchi wa Dar es Salaam walipata fursa ya kutoa heshima za mwisho kwa Magufuli ukiwa ndio mkoa wa kwanza. Maelfu ya wananchi walifurika katika Uwanja wa Uhuru, hali iliyosababisha mkanyagano miongoni mwao.
Ingawa bado Serikali haijatoa idadi ya waliofariki dunia wala majeruhi katika harakati za kupata fursa ya kuaga, lakini kuna watu watano kutoka familia moja walipoteza maisha pamoja na dada yao wa kazi katika tukio hilo.
Ndugu hao wa familia ya Daudi Mtuwa ni Susan Mtuwa na watoto wake wawili Nathan (6) na Natalia (5) pamoja na watoto wengine wawili Cris (11) na Michelle (8) wa shemeji zake Susan pamoja na dada wa kazi, Anitha Mfikwa.
Kuzungushwa uwanjani, mtaani
Machi 22, 2021 ilikuwa ni zamu ya wakazi wa Dodoma katika Uwanja wa Jamhuri na siku hiyohiyo ndiyo ilikuwa siku ya kuaga kitaifa, huku viongozi wengi wakubwa wa kimataifa wakihudhuria, wakiwamo baadhi ya marais kutoka Bara la Afrika.
Pengine kutokana na uzoefu walioupata Dar es Salaam, Dodoma watu wachache ndio walipata nafasi ya kuaga kwa kupita karibu na jeneza la Magufuli.
Viongozi ndio waliruhusiwa kwenda kuaga na baadaye gari lilizungushwa mara tano katika Uwanja Jamhuri na wananchi walikuwa wakipunga mkono.
Siku iliyofuata mwili wake ulipelekwa visiwani Zanzibar, kule watu walipata fursa ya kuaga na baadaye ulikwenda kulazwa katika Ikulu ya Zanzibar.
Kesho yake mwili ulielekea Mwanza ambako watu wachache walipata nafasi ya kuaga, kisha ukazungushwa katika uwanja mara tano na kupitishwa katika baadhi ya mitaa.
Marais tisa washiriki
Marais tisa kutoka barani Afrika walishiriki katika mazishi ya kitaifa ya Magufuli yaliyofanyika jijini Dodoma, huku wakimmwagia sifa kwa kusema alikuwa kiongozi mahiri.
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alitaka kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ ya Magufuli iendelezwe kwa kuwa itawafanya Watanzania kuwa na moyo wa ushujaa na kusonga mbele.
Rais wa Afrika Kusini, Matamela Cyril Ramaphosa alimtaja Magufuli kwa kuwa na uzalendo kwa Taifa lake, kusimamia maadili, vita dhidi ya rushwa na kukuza Kiswahili.
Taratibu za mazishi
Safari ya mwisho ya Magufuli ilihitimishwa nyumbani kwake wilayani Chato.
Siku moja kabla ya mazishi wananchi wa wilaya hiyo na maeneo ya jirani walipata fursa ya kumuaga.
Mazishi yake yaliyohudhuriwa na maelfu ya watu wakiongozwa na Rais Samia pamoja na viongozi wakuu wa kitaifa, yalifanyika kwa taratibu za Kanisa Katoliki pamoja na za kijeshi, kwa kuwa Magufuli alikuwa Amiri Jeshi Mkuu.
Baada ya ibada wanajeshi waliendelea na shughuli zao na wakati wote suala la ubebaji wa mwili lilikuwa lao.
Baada ya mwili wa Magufuli kuwekwa kaburini, familia yake ilikuwa ya kwanza kuweka udogo kisha Rais Samia na wengine wakafuata.
Baada ya taratibu za kanisa wanajeshi walipiga mizinga 21 ya heshima wakati wakihitimisha maziko ya aliyekuwa kiongozi wao huku ndege za kivita zikikatiza angani kutoa heshima.
Baada ya shughuli hiyo, jeshi lilimkabidhi mama Janeth Magufuli bendera ya Taifa kama ishara ya kuthamini mchango wa mume wake.
Alichosema Kikwete
Katika hotuba yake msibani Chato, Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alisema Magufuli alikuwa ndio chaguo lake la kwanza katika orodha ya watu 38 waliojitokeza kuomba uteuzi wa kuwa wagombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Hotuba ya Kikwete iliibua mjadala miongoni mwa watu kwasababu alisema si kweli kuwa alimchukia mrithi wa nafasi yake kama walivyokuwa wakisema wale aliowaita waganga njaa, hivyo alisisitiza walikuwa marafiki muda wote.
“Ooh! JK anamchukia Magufuli, labda sio mimi. Unamchukiaje mtu ambaye umemkabidhi ilani ya uchaguzi na akaitekeleza kwa kiwango cha juu sana, utamchukia kwa sababu ipi. Lakini nikasema duniani waganga njaa wengi, wengine wanapata mradi wao kwa kuongopa, nikasema hawajui walitendalo niwasamehe,” alisema Kikwete.
Mwinyi aibua kicheko msibani
Katika mwendelezo ule wa viongozi wakuu wa Serikali na wastaafu kutoa neno katika msiba huo, ilifikia zamu ya Rais wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassani Mwinyi ambaye aliwachekesha waombolezaji kutokana na maneno yake na hali ya kusahau mambo.
Mwinyi alianza kwa kuomba radhi kutokana na kile alichokisema tatizo lake la sasa kusahau sahau na kwa msisitizo alisema kuna wakati huwa anawasahau hata watoto wake wa kuwazaa mpaka mke wake, Siti Mwinyi amkumbushe. Mwinyi alichekesha zaidi alipomuuliza msaidizi wake walipo, ambaye alimwambia Chato.
Mara kadhaa alikuwa akiwauliza wasaidizi wake neno la kumalizia katikati mwa sentensi.
Alichokisema Niwemugizi
Akiongoza ibada ya mazishi, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge Ngara, Severine Niwemugizi alisema aliyekuwa Rais wa Tanzania, hayati Magufuli aliagiza arejeshewe hati yake ya kusafiria na alimtamkia mara mbili kuwa kiongozi huyo wa kiroho ndiye atakayemzika.
Mzee wa Chato aomba mkoa
Wakati Niwemugizi akisema hayo, mzee wa Wilaya ya Chato mkoani Geita, Samwel Bigambo alimuomba Rais Samia kumalizia mchakato wa Chato kuwa mkoa.
“Siku moja aliwahi (Magufuli) kutuambia hii Chato tunataka tuifanye iwe mkoa, sasa je, hiyo ahadi ife? Haiwezi kufa kwa sababu wewe (Rais Samia) ulikuwepo,” alisema Bigambo.
Akijibu hoja hiyo, Rais Samia aliwahakikishia wakazi wa Chato kuwa ahadi iliyotolewa na Magufuli inafanyiwa kazi.
Ujumbe wa mwisho wa JPM
Akitoa salamu za shukrani kwa waombolezaji, Ngusa Samike ambaye ni msemaji wa familia alisema kabla ya mauti kumfika, Magufuli aliwataka Watanzania wasitetereke bali wamtegemee Mungu.
Pia, alisema kwa mara ya mwisho Magufuli alipomtembelea mama yake ambaye ni mgonjwa alimfanyia sala ikiwa ni utaratibu aliouzoea.
Habari hii imeandikwa na Ephrahim Bahemu, Tatu Mohamed na Aurea Semtowe.