Mapadri wapya watakiwa kutokuwa na kigugumizi kutenda mema
Muktasari:
- Askofu wa Jimbo katoliki la Moshi, Askofu Ludovick Minde amewataka mapadri wapya kutokuwa na kigugumizi na wasiwasi wowote katika kutenda yaliyo haki na mema.
Moshi. Askofu wa Jimbo katoliki la Moshi, Askofu Ludovick Minde amewataka mapadri wapya kutokuwa na kigugumizi na wasiwasi wowote katika kutenda yaliyo haki na mema.
Askofu Minde ameyasema hayo leo Alhamisi Agosti 12, 2021 katika misa takatifu ya upadirisho wa mapadri 13 iliyofanyika katika Parokia ya Kristu Mfalme iliyopo manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Amewataka waumini wa kanisa hilo kuwaombea mapadri hao ili waweze kudumu katika nafasi zao za kitume na kuwa waaminifu katika kutimiza mipango mitakatifu iliyowekwa na kanisa.
"Mkawe na uaminifu kamili kama kristu alivyokuwa mwaminifu katika kutimiza mipango mitakatifu ya Mungu hivyo na nyinyi mkawe watakatifu na kutenda yaliyo mema katika maeneo yote yanayozunguka utume wenu."
Mashemasi 13 wa jimbo katoliki la moshi wakiwa wamelala kifudifudi wakati wa kila kiapo cha daraja la upadre kama ishara ya kujitolea maisha yao kwa Mungu. Ibada ya upadirisho imeongozwa na Askofu wa jimbo katoliki la Moshi, Askofu Ludovick Minde akiongozana na mapadre wa Jimbo hilo. Picha na Janeth Joseph.
"Tuwaombee wakae katika utume wao wa upadri ,mtu asiwe na wasiwasi wowote na kigugumizi katika kutenda yaliyo haki ili kila mtu aone kweli nyie ni makuhani na wahudumu wa Mungu wetu, tuwaombee ili wafanye mambo ya maendeleo katika suala la utakatifu."
"Mkafanye maendeleo na mpige hatua pamoja na waumini wenu katika suala la utakatifu ,minong'ono na kigugumizi iishe na iondolewe,"amesema Askofu Minde.