Mapenzi yanavyoteketeza maisha ya wapendanao

Saturday June 25 2022
mapenzipic
By Aurea Simtowe
By Hamida Shariff

Dar/Moro. Mauaji yenye viashiria vya wivu wa kimapenzi yanazidi kushika kasi.

Tukio la hivi karibuni la Leonia Ziota kufariki dunia katika nyumba ya kulala wageni na baa ya Lavi Park, sehemu ambayo inasadikika alikuwa na mwenzake wa kiume, linaongeza orodha ya matukio ya vifo vya wenza, yanayodaiwa kusababishwa na wivu wa mapenzi.

Kwa tukio la Leonia, tayari kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, linamshikilia mtu mmoja kwa madai ya kuhusika.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Tegeta kata ya Kunduchi, Mohammed Mawalla, mwili wa dada huyo anayekadiriwa kuwa na miaka 30 hadi 40, uligundulika Juni 17 saa sita mchana.

Uligundulika baada ya wahudumu wa nyumba hiyo ya wageni kubisha hodi kwa ajili ya kufanya usafi, lakini juhudi zao zikashindwa kuzaa matunda.

“Kila asubuhi huwa wanafanya usafi vyumbani lakini chumba kile kwa mujibu wa walichokisema kila walipogonga ili waweze kufanya usafi hakikufunguliwa, jambo ambalo liliwafanya kutafuta mbinu ya ziada ili waweze kufungua mlango.

Advertisement

“Baada ya kufungua walikuta mazingira yaliyoashiria kuwepo kwa tatizo, hivyo walitoa taarifa kwangu na kituo cha polisi kilichopo jirani,” alisema.

Alisema kwa mujibu wa wahudumu wa eneo hilo, wenza hao wawili walichukua chumba Alhamisi Juni 16, kujipumzisha huku aliyeandikisha akiwa mwanaume.

“Inaonekana kulikuwa na purukushani, maana mwili ulikuwa na majeraha,” alisema.

Meneja wa eneo hilo ambaye hakufahamika jina aligoma kuzungumza, huku akisema kuwa kila kitu kipo mikononi mwa polisi wanaoendelea na uchunguzi hivi sasa.

Mmoja wa wanaofanya shughuli katika eneo hilo, alilieleza Mwananchi kuwa mwili huo ulipatikana baada ya dada wa usafi kugonga mlango bila mafanikio.

“Ikifika saa nne asubuhi huwa ni muda wa usafi, sasa yule dada aligonga bila mafanikio kila akienda akirudi akigonga kimya ikabidi awashirikishe wengine, walipofanya maarifa ya kufungua mlango walimkuta huyo dada akiwa ameshakufa,” alisema dada huyo ambaye hakutaka kutaja jina.

Kwa mujibu wa mashahidi na watu wanaomfahamu marehemu, walisema alikuwa akimiliki saluni ya kike katika eneo la Sinza karibu na baa mpya ya Kitambaa Cheupe, zamani Meeda.

Geodfrey Mande ambaye ni kaka wa mrehemu alipohojiwa alisema siku moja kabla ya kupata taarifa ya kifo cha ndugu yao, walikuwa wakimpigia simu bila mafanikio, jambo ambalo liliwafanya kuanza kufuatilia kujua alipo.

Alisema baada ya kufuatilia waliambiwa kuwa alienda Tegeta na tangu hapo hawakupata taarifa zake hadi waliposikia kuna mwili wa mtu umepatikana katika eneo la Tegeta, hivyo ilibidi wafuatilie na walipoonyeshwa picha waligundua kuwa ni yeye.

“Baada ya kwenda hadi hospitali tuliambiwa twende polisi, tulifuata taratibu na waliahidi kuwa watamfuatilia mtu ambaye amefanya tukio hilo na walisema anafahamika kwa sababu sehemu waliyokuwapo kuna taa za usalama,” alisema.

Kupitia taarifa ya jeshi la Polisi iliyotolewa na kamanda wa Polisi kanda Maalumu ya Dar es Salaam ilithibitisha kutokea kwa tukio hilo katika nyumba ya kulala wageni ya Lavi Park iliyopo Tegeta kwa Ndevu jijini hapa.

“Chanzo halisi cha tukio kinachunguzwa na kwa kutumia mbinu za upelelezi wa kisayansi mtuhumiwa huyo aliyetoroka mara baada ya tukio hilo amekamatwa Juni 21, 2022 maeneo ya Manzese, Kinondoni jijini hapa,” alisema Muliro.


Mauaji Morogoro

Mbali na tukio hilo, juzi mwanaume mmoja aliyetambulika kwa jina la Kibwana Musa mkazi wa kijiji cha Kiziwa A mkoani Morogoro, anadaiwa kuuawa kwa kukatwa mapanga na mtu aliyedaiwa kuwa na uhusiano na mwanamke aliyekwenda kuishi kwake.

Akisimulia mkasa huo, Mwenyekiti wa kijiji cha Kiziwa A wilayani Morogoro, Mbena Loki alisema kuwa tukio hilo la mauaji lilitokea juzi majira ya alfajiri wakati marehemu akiwa amelala nyumbani kwa mwanamke huyo aliyefahamika kwa jina la Farida Ally, ambapo mtuhumiwa aliweza kuingia ndani baada ya mwanamke kufungua mlango kwa lengo la kwenda chooni kujisaidia.

“Huyu mtuhumiwa zamani alikuwa na uhusiano na huyu mwanamke na baadaye waliachana kila mmoja akaendelea na maisha yake. Hivi karibuni huyu mwanamke alianzisha uhusiano wa kimapenzi na marehemu, hata hivyo bado huyu mtuhumiwa aliendelea kumsumbua na kumfuatilia mwanamke mpaka jana ndipo alipoamua kufanya tukio hilo la mauaji,” alidai Loki.

Mwenyekiti huyo alisema taarifa za kuuawa kwa mwanamume huyo zilianza kusambaa majira ya asubuhi ambapo uongozi wa kijiji ulifika eneo la tukio na kumchukua mwanamke huyo kwa kumpeleka kituo kidogo cha polisi Mkuyuni kwa ajili ya usalama wake.

Alisema kuwa baada ya kufanya tukio hilo mtuhumiwa huyo alikimbia kusikojulikana na polisi wanaendelea na jitihada za kumsaka, huku wananchi wengine wenye hasira wakiamua kuchoma moto nyumba ya mtuhumiwa.

Kwa upande wake kaka wa marehemu Juma Kibwana, alisema kuwa alipata taarifa za kuuawa kwa mdogo wake majira ya asubuhi kutoka kwa mpwa wake, hivyo alifika eneo la tukio na kukuta mwili wake ukiwa na majeraha na kutokwa na damu nyingi.

Kaka huyo wa marehemu alisema kuwa kabla ya umauti marehemu hakuwahi kumweleza chochote kuhusu uhusiano wake na mwanamke huyo, hivyo tukio hilo limemshangaza na kumsikitisha kwani pamoja na kuwa la kikatili, lakini pia marehemu ameacha pengo kwa familia yake ambayo ni mke na mtoto mmoja.

“Mimi ninachofahamu marehemu mdogo wangu alikuwa na mke mmoja ambaye kwa sasa ni mjamzito pamoja mtoto mmoja, hata hivyo huyo mke wake kwa sasa yupo kwao mkoani Kigoma alikokwenda kujifungua,” alisema Juma.

Naye kiongozi wa familia ya marehemu, Msafiri Ally aliliomba Jeshi la Polisi kuendesha msako mkali ili kufanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo ambaye amekimbia baada ya kufanya mauaji hayo.

Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Fotunatus Musilimu alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa kimapenzi, kwani mtuhumiwa alikuwa na chuki na marehemu ambaye alikuwa na uhusiano na mwanamke huyo ambaye alishamwacha.


Advertisement