Mapya yaibuka kifo cha Mengi
Ndugu jamaa na marafiki wakiwa nyumbani alikozaliwa marehemu Reginald Mengi, Nkuu Sinde Machame kwa ajili ya kutoa pole. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Mwandishi wa habari Jackline Masinde, mwenyekiti mstaafu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda pamoja na wabunge wa Chadema, Upendo Peneza (viti maalumu) na Saed Kubenea wa Ubungo ni miongoni mwa wanaoukumbuka mchango wa mfanyabiashara huyo.
Dar/Dodoma. Baadhi ya watu ambao kwa namna moja au nyingine maisha yao yaliguswa na Mengi wameeleza jinsi walivyonufaika na mchango wake.
Watu hao, kila mmoja ana simulizi ya kusisimua kumhusu mfanyabiashara huyo aliyezaliwa Mei 29, 1942.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti jana, walieleza alivyowasaidia baada ya kumfuata au yeye kuwafuata pale alipoguswa na kazi au matatizo yao.
Mwandishi wa habari Jackline Masinde, mwenyekiti mstaafu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda pamoja na wabunge wa Chadema, Upendo Peneza (viti maalumu) na Saed Kubenea wa Ubungo ni miongoni mwa wanaoukumbuka mchango wa mfanyabiashara huyo.
Masinde na ujumbe mzito
Masinde ambaye alikuwa mwandishi wa Mwananchi hadi siku chache zilizopita anasema alifahamiana na Mengi mwaka jana, baada ya habari yake ya uchunguzi kuhusu watu wenye ulemavu kutumika kuwatajirisha wengine jijini Dar es Salaam.
Alisema habari hiyo iliangazia jinsi watu wanavyokwenda kuwachukua wenye ulemavu mikoani na kuwapeleka Dar es Salaam, kisha kuwatumia kama ombaomba na fedha zinazopatikana kuzichukua wao.
Masinde alisema baada ya habari hiyo iliyochapishwa mfululizo kumalizika, Mengi alimuita ofisini kwake na kuzungumza naye ikiwamo kumweleza jinsi habari hiyo alivyoifanya ambapo mfanyabiashara huyo alimzawadia fedha, kujitolea kumsomesha pamoja na kitabu alichomwandikia ujumbe wa kumtia moyo.
“Alinipokea, kwanza alishangaa kwani alidhani ningekuwa mkubwa kiumbo na kiumri, nami nilishangaa kwani sikuamini kama nimekutana naye kwani nilizoea kumuona kwenye televisheni tu,” alisema Masinde.
“Alinikumbatia, akaniwayo na kuni-kiss katika paji la uso na kuniambia your are great girl kisha tukakaa ofisini kwake pembeni kwa mazungumzo yaliyolenga kumwelezea undani wa habari hiyo ya ombaomba.”
Masinde alisema baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa zaidi ya saa mbili ndipo Mengi alimpatia zawadi.
“Alipotaka kunipa zawadi, akanyanyuka katika kiti alipokuwa amekaa na kwenda kukaa katika kiti chake cha ofisini na kuniita,” alisema mwandishi huyo.
“Nilipofika nikakaa mbele yake, akatoa fedha katika droo yake na kunipatia na akaniambia atahakikisha ananisaidia nafika pale ambapo nataka kufika kwani ameona kitu cha kipekee kwangu.”
Masinde alisema alimweleza Mengi anahitaji kwenda kusoma - ombi ambalo alikubaliwa na kuanza mchakato uliomwezesha kupata chuo nchini India ambacho ilikuwa aende Agosti, mwaka jana.
Hata hivyo, alisema ilishindikana kwani mfanyabiashara huyo alisafiri kwenda nje ya nchi hali iliyokwamisha kwenda chuoni na kuombwa tena na Mengi atafute chuo kingine alichopata huko Mauritius.
Alisema Mengi alimuunganisha na mkurugenzi wa Taasisi ya Reginald Mengi ambaye alimweleza awe anawasiliana naye kwa mambo mengine kama itakuwa vigumu kumpata yeye (Mengi).
“Tayari Mengi amekwisha kunilipia gharama zote za chuo kwa mwaka mmoja, kilichobaki ni kupewa fedha za gharama za matumizi madogo ya chuo lakini kila kitu kiko tayari kwa ajili ya safari mwezi huu.
“Kilichokuwa kimebaki ni kwenda kumuaga na mimi niliandaa zawadi kwa ajili ya kumshukuru kwa zawadi hii ya kunisomesha,” alisema Masinde ambaye amesisitiza kutekeleza yote aliyomwachia kama wasia.
“Katika kitabu alichonipa aliniandikia ujumbe kwa lugha ya Kiingereza akimaanisha kutokana na moyo nilionao, ujasiri wa kufanya stori za hatari, akanitabiria nitakuja kuwa mwandishi bora duniani kama nitaamini katika slogan ya I Can, I Must, I Will.”
Mbunge Peneza
Mbunge Peneza alisema atamkumbuka Mengi kwa kumtia moyo wa kusonga mbele ili kutimiza ndoto zake za kuwa kiongozi.
Akizungumza na Mwananchi jana katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma, alisema mwaka 2014 akiwa anazungumza katika kipindi cha ITV kuelekea uchaguzi wa ndani ya Chadema kwa Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha), Mengi alimuona na kuandika ujumbe mfupi katika akaunti yake ya Twitter akionyesha furaha yake kwa namna alivyokuwa akijieleza kama mgombea uenyekiti.
“Aka-twiti, akasema namuangalia Upendo Peneza ni kijana ambaye kutokana na jinsi anavyojieleza namuona ni shujaa wangu mdogo,” alisema mbunge huyo.
Alisema baadaye Mengi alimpigia simu ya kumtia moyo afike hadi ambapo anataka kufika, jambo ambalo lilimsaidia katika kampeni zake za kuwania nafasi hiyo.
“Natambua juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa na Mzee Mengi za kuwasaidia watu mbalimbali,” alisema Peneza ambaye katika uchaguzi huo alishika nafasi ya pili na Patrobas Katambi akaibuka mshindi wa uenyekiti.
Hata hivyo, Katambi alijiuzulu nafasi hiyo na kutimkia CCM ambapo Rais John Magufuli alimteua kuwa mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini.
Kibanda, Kubenea
Kwa upande wake, mwandishi mkongwe nchini, Kibanda, akiwa mhariri mtendaji mkuu wa Kampuni ya New Habari 2006, alijeruhiwa jicho na watu wasiojulikana, lakini Mengi alikuwa mmoja wa waliochangia matibabu yake nje ya nchi.
“Hata nilipoumia mwaka 2013 alikuwa ni miongoni mwa marafiki wa Kibanda waliochangia matibabu yangu kule Afrika Kusini kama rafiki, mzazi, mlezi na kiongozi,” alisema Kibanda.
“Nilipata ujasiri wa kuongoza Jukwaa (la Wahariri Tanzania-TEF) kwa sababu ya msaada wa mawazo na fedha, kuna wakati alikuwa anakodi kumbi kwa ajili ya (wahariri) kufanyia mikutano.”
Alisema pamoja na yote hayo hakuwahi kuingilia uamuzi wa TEF, licha ya mara kadhaa kuwa na mitizamo iliyotofautiana akiwa ni mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari (Moat).
“Alikuwa anatuelewa (wahariri), anatumia muda mwingi kutuelimisha na kutuambia mawazo yake akihimiza weledi na maadili ya kitaaluma ya vyombo vya habari,” alisema Kibanda.
Mbunge Kubenea ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya Halihalisi Publishers, alisema Mengi kwake alikuwa rafiki, mzazi, mlezi na kiongozi.
Alisema hatua aliyofikia hadi sasa, kwa asilimia 80 kuna mchango wa mfanyabiashara huyo ikiwamo uandishi wa habari, umiliki wa chombo cha habari na hata ubunge.
Alisema alipomwagiwa tindikali mwaka 2008, Mengi alikwenda moja kwa moja Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) akitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam.
Alisema wakati huo hakukuwa na mitandao mingi ya kijamii, na kwamba kwa mujibu wa Mengi alimwambia kuwa alisikia tukio hilo kupitia taarifa ya habari ya ITV akiwa uwanjani hapo akitokea Moshi saa nne usiku.
“Akaniuliza kuna mpango gani wa matibabu, nikamweleza madaktari wamenishauri nikatibiwe nje ya nchi kwa sababu wao hawana uwezo wa kunitibu zaidi ya kupunguza machungu na wingi wa tindikali kwa kuweka maji kwenye bomba la sindano na kuniwekea machoni,” alisema.
“Wameniambia nisipopata matibabu sahihi ndani ya saa 48 ninaweza kuwa kipofu kabisa.”
Alisema Mengi alimwambia, kama shida ni matibabu gharama zote atatoa yeye (Mengi) na siku iliyofuata alikutana na wadau wa habari, ikiwamo wamiliki wa vyombo vya habari kwenye ukumbi wa Habari (Maelezo) kujadili suala hilo.
Alisema baadaye Mengi alimwambia amezungumza na Rais Jakaya Kikwete (wakati huu) na amesema Serikali itagharamia matibabu, lakini kwa sababu mambo ya kiserikali yanachukua muda kushughulikiwa ataanza yeye.
“Alinipa dola 5,000 nikaenda India, Hospitali ya Apollo wakati huo balozi alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa sasa John Kijazi, alinipokea na kuniambia hajapata taarifa kutoka serikalini za matibabu yangu,” alisema Kubenea.
“Nikamwambia nimekuja na fedha yangu, hivyo akanipa mtu aliyekuwa anaitwa Kiondo anipeleke hospitali, nikaanza tiba.”
Alisema kabla ya kuwa mbunge alikwenda kutibiwa India zaidi ya mara 10, huku karibu mara sabu au nane gharama zote zikilipwa na Mengi, ikiwamo London nchini Uingereza na Uholanzi.
“Siyo mimi tu, bali hata marafiki zangu wa karibu wanapopata shida nilikuwa nikimuomba msaada anasaidia hapohapo, hata alipoumizwa Absalom Kibanda nilizungumza naye na akasema yupo tayari kuuza kiatu chake kumtibia,” alisema mbunge huyo.
Habari hizi zimeandikwa na Fortune Francis, Kalunde Jamal, Elias Msuya (Dar es Salaam), Florah Temba, Janeth Joseph (Kilimanjaro) na Sharon Sauwa (Dodoma)