Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mara yapanga bajeti ya Sh488.9 bilioni

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi akizungumza kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa huo. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

  • Kiasi hicho cha fedha kinatarajiwa kutumika kwa ajili ya mishahara, matumizi mengineyo na miradi ya maendeleo katika ngazi ya sekretarieti ya mkoa na zile za serikali za mitaa mkoani humo.

Musoma. Sekretarieti ya Mkoa wa Mara pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa mkoani humo zinatarajia kutumia zaidi ya Sh488.9 bilioni katika mwaka wa fedha 2026/27 kwa ajili ya kutekeleza shughuli za sekretarieti ya mkoa na mamlaka za serikali za mitaa.

Kiasi hicho cha fedha kinatarajiwa kutumika kwa ajili ya mishahara, matumizi mengineyo na miradi ya maendeleo katika ngazi ya sekretarieti ya mkoa na zile za serikali za mitaa mkoani humo.

Taarifa hiyo imetolewa mjini Musoma leo Jumanne Machi 3,2026 na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Mipango na Uratibu Mkoa wa Mara, Emmanuel Mazengo kwenye kikao cha kamati ya ushauri mkoa wa Mara (RCC).

Mazengo amesema kiasi hicho cha fedha kimeongezeka kutoka Sh400.1 bilioni kiasi ambacho mkoa huo uliidhinishiwa kwa ajili ya kutekeleza shughuli za sekretarieti ya mkoa na mamlaka za serikali za mitaa kwa mwaka wa fedha 2025/26.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amesema bado hajaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya jamii, hivyo kuwataka watendaji wa Serikali kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo sambamba na usimamizi.

Amesema kwa mwaka wa fedha 2024/25 mkoa huo ulivuka na bakaa ya Sh26.9 bilioni fedha ambazo zilipangwa kutumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali lakini hazikutumika.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa miradi mingi ya mwaka 2025/26 bado uko nyuma huku miradi mingine ikiwa bado ipo katika hatua za awali za utekelezaji wake, ambapo ameagiza miradi yote ikamilike kabla ya Juni 2026.

Baadhi ya wajumbe wa kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa (RCC) mkoani Mara wakiwa kwenye kikao mjini Musoma.  Picha na Beldina Nyakeke



Kanali Mtambi pia ameziagiza halmashauri zote mkoani humo kuanza mara moja maandalizi ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa mwaka 2028,  kwa maelezo kuwa kwa mwaka huo wanafunzi hao watakuwa mara mbili ya kawaida kutokana na kuanza kwa utekelezaji wa sera ya mpya ya elimu.

"Anzeni kutenga bajeti kutokana na fedha za ndani kwani mwaka 2028 tutakuwa na wanafunzi wa kidato cha kwanza waliomaliza darasa la saba na wale watakaoishia darasa la sita, hii ina maana mahitaji yatakuwa makubwa hivyo ni wajibu wetu kuanza maandalizi kuanzia sasa," amesema

Wakichangia hoja katika kikao hicho baadhi ya wajumbe wametaka kuwepo kwa uwajibikaji wa watendaji wa Serikali ili kuboresha huduma za jamii kwa wakazi wa mkoa huo.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mara, Agnes Marwa amesema kutokana na kuwa na chanzo cha uhakika wa maji hakuna sababu ya baadhi ya vijiji vya mkoa huo kukosa huduma hiyo.

"Hakuna sababu ya vijiji vya mkoa wa Mara kukosa maji wakati tuna chanzo kikubwa sana cha maji ambacho kimetumika kupeleka maji katika mikoa kama Shinyanga na Singida,viongozi hakikisheni Mkoa wa Mara upatikanaji unakuwa wa uhakika pamoja na maeneo ya vijijini," amesema Agnes.

Christina Joseph amewataka watendaji wa Serikali kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ubora na wakati ili wananchi waweze kunufaika.