Marobota 50 ya vitenge yanaswa Mtwara

Sunday January 27 2019
nanyumbu pic

Dar es Salaam. Kamati ya ulinzi na wsalama ya wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara imefanikiwa kukamata marobota 50 ya nguo aina ya vitenge yaliyoingizwa nchini kinyume cha sheria yakitokea Msumbiji.

 

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Moses Machali amesema leo Jumapili Januari 27, 2019 kuwa marobota hayo yalikamatwa jana saa 12 jioni baada ya gari aina ya fuso iliyokuwa imepakia kufanyiwa ukaguzi.

 

“Taarifa nilizonazo gari lilikamatwa mchana eneo Daraja Umoja Mtambaswala na shughuli ya kulikagua ilifanyika jioni. Wahusika wa lile gari waliweka maroboto yale chini kisha kuyafunika na turubai huku juu wakiweka vyuma chakavu ili kuwazuga maofisa wa forodha,” amesema Machali ambaye pia nduiye mkuu wa wilaya hiyo.

 

Advertisement

Ofisa tarafa wa Nanyumbu, Livinus Nchimbi amesema gari hilo lilikuwa linatokea Msumbiji kupitia kitongoji cha Mtambaswala kilichopo kijiji cha Lukula wilayani humo.

 

Kwa mujibu wa Nchimbi, marobota hayo yana kilo zaidi 130 kwa kila moja na thamani yake ni zaidia ya Sh19.57 milioni.

 

“Mzigo huu ungeingia bila kukamatwa tungepoteza fedha hizi. Naviomba vyombo vya ulinzi na usalama vya mpakani viendelee kuimarisha ulinzi na kudhibiti uingizwaji wa bidhaa zinatoka na kuingia nchini bila kufuata utaratibu,” amesema Nchimbi.

Advertisement