Prime
Maswali kibao tukio la 'utekaji' wa Tarimo
Dar es Salaam. Wakati Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi wa tukio la kutaka ‘kutekwa’ kwa mfanyabiashara, Deogratius Tarimo, mijadala imeibuka juu ya hali ilivyokuwa na kuibua maswali kibao.
Tukio hilo lililotokea Jumatatu ya Novemba 11, 2024 eneo la Kiluvya jijini Dar es Salaam, limetonesha matukio ya aina hiyo ya watu ‘kutekwa’ ama kupotea katika mazingira ya kutatanisha.
Baadhi ambayo wamekuwa wakikumbwa na kadhia hiyo, wamekuwa wakionekana ama wakiwa na majeraha, wengine wameuawa na wengine wakiendelea kutafutwa kwa kutokuonekaa kwao.
Video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii inayowaonyesha watu wawili wakijaribu kumkamata na kumwingiza kwa nguvu ndani ya gari Tarimo, maarufu Deo Bonge imeibua mjadala maeneo mbalimbali nchini.
Katika video hiyo, inaonyesha jinsi Deo Bonge alivyokabiliana na watu hao ambao inadaiwa ni askari polisi. Purukushani za hapa na pale zilifanyika kwenye mwanga na zinaonesha jinsi watu hao walivyomchania nguo ya juu na kumwanga tumbo wazi.
Simulizi za mashuhuda wa tukio hilo akiwemo muhudumu wa hoteli hiyo wanaeleza tukio lilivyokuwa na jinsi watu hao walivyofika eneo hilo akidai walijitambulisha ni askari polisi wa kituo cha Gogoni wakimtaka apande kwenye gari aina ya Raumu waliyokwenda nayo.
Video hiyo ya sekunde 49 inasikika sauti ya Deo Bonge akiomba msaada kutoka kwa majirani ‘mnaniua, aiiii, iiiii, naomba msaada, nisaidieni jamani.” Huku watu hao nao wanasikika wakisema twende Gogoni.
Miongoni mwa maswali yanayoibuka juu ya tukio hilo ni je, watu hao walitumwa na nani, walikuwa na lengo gani dhidi ya mfanyabiashara huyo, kwa nini hawakutaka kujitambulisha kwa kutoa vitambulisho.
Mbona hawakwenda na gari la polisi au hata askari mwenye sare, kwa nini walipomuona askari wa usalama barabarani aliyekuwa amevaa sare wakaambiana waondoke, kwa nini wananchi hawakumsaidia au kuwashurutisha watu hao kumwachia?
Kama ni mhalifu kwa nini waliamua kumwacha na moja ya dhana zao za kazi ambayo ni pingu waliyokuwa wamemfunga mkono mmoja wa kushoto?
Mmoja wa askari polisi mstaafu mwandamizi akizungumzia tukio hilo amesema,”kwa uzoefu wangu, haikuwa sahihi kwa watu wale kama kweli ni askari kumwachia mtuhumiwa akiwa na pingu, kwa sababu pingu ni moja ya silaha za polisi.
Kama kweli alikuwa ni polisi halafu walipaswa kumdhibiti mtu yule na kumfunga pingu na kwa sababu video ile inaonyesha walikuwa zaidi ya watatu, walikuwa na uwezo huo.”
Askari huyo aliyeomba hifadhi ya jina lake amesema,”ila ukiitazama video ile, inaonyesha wakamataji walikuwa na hofu na ndio maana walishindwa kumdhibiti mtu yule. Hiyo inaashiria, huenda wale sio polisi bali ni wahalifu tu, au inawezekana ni polisi halali, lakini wanafanya kazi ambayo hawakutumwa na kwa masilahi yao binafsi.”
Wakili Jebra Kambole kwenye ukurasa wake wa kijamii wa X (zamani Twitter) ameandika maswali matano yakielekeza mtu hapaswa kukamatwa na mtu, kavaa kiraia, gari halina namba au namba za kiraia.
Watu ambao hawajatoa vitambulisho, watu wasiokwambia kosa lako na kwamba uko chini ya ulinzi na mwisho watu wasio na hati ya ukamataji, “pambana kama Big Tarimo!!”
Taarifa ya Polisi
Mapema leo Jumatatu, Novemba 13, 2024, Jeshi la Polisi kupitia kwa Msemaji wake, David Misime limetoa taarifa kwa umma likieleza kufuatilia tukio hilo lililotokea Hoteli ya Rovenpic, Kiluvya Novemba 11, 2024 na kuahidi kuwakamata watu hao.
“Jeshi la Polisi linachunguza picha mjongeo inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha watu wanaojaribu kumkamata na kumwingiza kwa nguvu ndani ya gari, Deogratius Tarimo. Tukio hili liliripotiwa na yeye mwenyewe katika kituo cha Polisi Gogoni Jijini Dar es Salaam Novemba 11, 2024,” imesema taarifa hiyo.
Baadaye jioni, Mwananchi lilimtafuta tena Misime kujua kinachoendelea hususan watu hao wakidaiwa kuwa ni askari kutokana na baadhi kuonekana nyuso zao na watu kuwatambua. Hata hivyo, hakupatikana.
Simulizi za mashuhuda
Mwananchi limefika eneo hilo la tukio na kuzungumza na mashuhuda wa tukio hilo akiwemo mmoja wa wahudumu wa hoteli hiyo, iliyopo maeneo ya Kiluvya madukani ambaye hakutaka jina lake kutajwa, akisema mfanyabiashara huyo ni mteja wao na amekuwa na kawaida ya kwenda sehemu hiyo mara kwa mara.
"Huyu mfanyabiashara ni mgeni wetu na huwa anakuja hapa mara kwa mara kunywa na kulala baada ya kufanya shughuli zake ingawa hatujui anaishi wapi," amesema.
Amesema ni mteja wao wa muda mrefu amekuwa akiwaungisha na akiwa hapo muda mwingi walikuwa wanachangamana naye vizuri na hakuwahi kuonyesha jambo lolote la tofauti.
Amesimulia hata siku hiyo ya tukio linatokea mchana hivi, alikaa kidogo ndipo vijana hao watatu walikuja kimuonekano ilionekana walikuwa wamekubaliana kufanya mazungumzo hayo.
"Alikuwa amekaa hapa kaunta akinywa kinywaji baridi hatukuwa tunahisi chochote, baada ya muda vijana wawili waliingia na kwenda kukaa pembeni yake wakawa wanasalimiana kama wanajuana," amesema.
Amesimulia mazungumzo hayo hayakudumu sana kwakuwa watu hao walionekana wenye haraka muda mwingi wakimtaka kwenda nje ya hoteli hiyo.
"Baadaye tulianza kuona wanaanza kusigana na vijana hao ambao awali walikuwa wanajitambulisha Polisi wa Kituo cha Gogoni na kumtaka akapande kwenye gari waende naye kituoni hapo " amedai.
Amesimulia katika mvutano huo, mfanyabiashara huyo alikuwa anawagomea akiweka msimamo wake kutaka wamuonyeshe kitambulisho kwanza ajiridhishe kama kweli ni askari Polisi.
"Baada ya kubishana kwa muda mrefu ndipo walianza kumvuta kwa nguvu wakimpeleka nje walikosimamisha gari kutokana na nguvu alizokuwa nazo Deo walionekana kama wanazidiwa," amesema.
Amesema wakati anatolewa eneo la kaunta hiyo vijana hao walikuwa wamejipanga mmoja alimshika upande wa kulia na mwingine kushoto.
"Ilikuwa kila wakitaka kutoa pingu waweze kumfunga Tarimo alikuwa anapangua kwa kuwa naye alionekana mtata wa kutaka kumpeleka wanakotaka," amesimulia.
Amesimulia wakati wakiendelea kumvuta walipofika nje kutokana na kelele alizokuwa anapiga mfanyabiashara huyo, watu wanaoishi jirani na hoteli hiyo walitoka nje kushuhudia tukio hilo.”
"Mvutano ulidumu kwa saa moja hivi, lakini kadri muda ulivyokuwa unasonga watu walikuwa wanaongezeka hadi watoto waliokuwa wanatoka shule wakawa wanakuja kushuhudia," amesema.
Amesema wakati watuhumiwa hao wakiendelea kumsukuma kinguvu mfanyabiashara huyo ili aingie ndani ya gari hiyo, ghafla alijitokeza Polisi wa usalama barabarani aliyekuwa anapita njia.
"Baada ya kumuona askari huyo dereva wa gari hiyo aliyeicha gari ikiunguruma muda wote aliwashitua wenzake akiwataka wamuachie waondoke haraka na ikawa salama yake " amedai.
Mashuhuda wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi baada ya kutembelea eneo hilo, wamesema walikuwa wanashuhudia tukio hilo kama muvi.
"Tulikuwa tunahisi kama mtuhumiwa labda anakamatwa ametenda kosa na tuliokuwepo wengi tulikuwa wanawake na watoto, hatukuwa na ujasiri wa kutaka kuhoji kutokana na aina ya nguvu zilizokuwa zinatumika," amesema, Rahma Juma.
Rahma amesema hoteli hiyo ni eneo ambalo watu wanakwenda kulala, kunywa kula na wakati mwingine kufurahia huku akieleza nyakati za sikukuu huwa panajaa na watoto wanakuwa wengi.
"Ni eneo ambalo watu wamezoea hapa Kiluvya kutokana na kuwa na mandhari nzuri ya kuvutia, kuogelea na tulipoona tukio hili tulistaajabu kwa kuwa si kawaida kusikia mtu akilia anaenda kuuawa," amesema.
Naye, Salum Ali amesema katika tukio hilo kuna mambo mengi nyuma ya pazia ikiwamo aliyekuwa akivutwa kujuana na waliokuwa wakimvuta.
"Kama ni mfanyabiashara inawezekana wamedhulumiana, wanadaiana haiwezekani mtu atoke kusikojulikana aje kuteka, ni nyakati za kuwa makini ni mwishoni mwa mwaka huu matukio ni mengi," amesema.
Amesema kilichomsaidia kuhimili kashikashi za watuhumiwa hao ni umbile lake la unene na ubishi aliokuwa anauonesha vinginevyo watuhumiwa wangefanikiwa.
"Ni tukio lililofanyika kwa muda mrefu kuzozana kulikuwa kwingi, fikiria watu wa tatu wanashindwa kumkamata pamoja na kufanikiwa kumvua shati lakini jamaa alikuwa mbishi," amesema.
Mazingira
Mazingira ya hoteli hiyo imezungukwa na makazi ya watu.
Gari tatu za Jeshi la Polisi ziliwasili eneo hilo saa 4:47 asubuhi zikiwa na askari walioshuka na kuingia hotelini humo.
Baada ya kupita dakika 10 hivi, gari moja ya jeshi hilo iliondoka katika eneo hilo na kuyaacha mawili.