Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Matumizi sahihi ya dawa yanapaswa kuwa hivi

Mfamasia Mwandamizi wa Baraza la Famasia (PC), Amour Iddi (kushoto), akitoa elimu kwa wadau wa afya waliojitokeza kwenye maonesho ya wiki ya famasia jijini Dar es Salaam, ambayo yaliambatana na utoaji wa elimu kwa umma. Picha na Said Powa

Muktasari:

  • Baraza la Famasi limesema matumizi holela ya dawa, kutomaliza dozi na kugawana dawa ni matumizi yasiyo sahihi ya dawa ambayo huchoea magonjwa mwilini.

Dar es Salaam. Mratibu wa Kanda ya Mashariki wa Baraza la Famasi, Tumaini Makole ametaja mambo matatu anayopaswa kuzingatia mgonjwa ili atumie dawa kwa usahihi, ikiwemo kufanyiwa vipimo kubaini tatizo linalomsumbua.

Makole amesema endapo mgonjwa ataanza kutumia dawa bila kufahamu chanzo cha tatizo lake, hutengeneza usugu wa vimelea dhidi ya dawa mwilini.

Mtaalamu huyo wa famasi ametoa kauli hiyo leo Juni 12, 2026 wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Famasi yaliyofanyika Dar es Salaam.

Maadhimisho hayo yalianza Juni 10 na yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 16, yakiwa na kaulimbiu ya “Famasi Kufungua Maono 2050 katika Sekta ya Afya.”

Hatua nyingine muhimu aliyoitaja Makole, baada ya mgonjwa kuonana na wataalamu wa afya, anapaswa kufanyiwa vipimo, kuandikiwa dawa sahihi na kuzitumia kwa usahihi kama alivyoelekezwa.

“Unaandikiwa dawa uitumie kwa siku tano, unywe baada ya kila saa nane, halafu ukaanza kutumia na kuacha baada ya siku tatu. Hayo ndiyo tunaita matumizi yasiyo sahihi ya dawa,” amesema.

Amesema mtu anapoandikiwa dawa aitumie kwa siku tano au wiki moja, lazima azingatie maelekezo hayo na hashauriwi kumpatia mtu mwingine dawa hiyo.

Amesema kumeibuka tabia ya mtu anapopata nafuu kukatisha matumizi ya dawa, hali ambayo ameieleza kuwa ni hatari kwa mgonjwa.

Makole amesisitiza kuwa matumizi sahihi ya dawa ni muhimu kuzingatiwa na mtu hapaswi kuacha dawa ili kumhifadhia ndugu yake ambaye anaumwa.

“Tunawasisitiza wananchi kuhusu matumizi sahihi ya dawa. Ukipewa dawa hupaswi kuitumia pamoja na mtu mwingine. Huyo anayeumwa aende kwa wataalamu apate ushauri,” amesema.

Akizungumzia Wiki ya Famasi yenye kaulimbiu ya ‘Famasi Kufungua Maono 2050 katika Sekta ya Afya’, Makole amesema Dira ya Maendeleo ya Taifa inawalenga wataalamu wa famasi kutokana na kuhusika kwenye mnyororo mzima wa dawa.

Mnyororo huo ni kuanzia uzalishaji hadi kusimamia matumizi ya mwisho kwa mwananchi.

“Tunaposema famasi ni ufunguo wa Maono 2050 katika sekta ya afya, tunamweka mfamasia katikati katika kutekeleza malengo ya dira,” amesema.

Makole amesema wataalamu wa famasi wanahusika na usimamizi wa matumizi sahihi ya dawa kwa watumiaji wa mwisho.

Kwa upande wake, Justin Shaban, mkazi wa Mbezi ambaye alihudhuria maonesho hayo, ameliomba Baraza la Famasi kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya dawa.

“Bado elimu ya matumizi sahihi ya dawa katika jamii ni changamoto. Tunaliomba Baraza la Famasi kuendelea kuwatumia wataalamu wake kutoa elimu kwa wananchi.

“Wapo watu hawamalizi dawa wanazopatiwa na wataalamu na baada ya muda ugonjwa unarudi kwa kasi, wanalalamika na wengine hupoteza maisha,” amesema.


Wizara inasemaje

Kwa mujibu wa Hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Afya ya mwaka 2026/27, Baraza la Famasi lina majukumu ya kusimamia taaluma na wataalamu wa dawa, utendaji wao pamoja na usajili na utoaji wa vibali maeneo yanayotoa huduma za dawa na kuelimisha jamii kuhusu matumizi sahihi ya dawa.

Kwa mujibu wa hotuba hiyo, Baraza hilo lina wataalamu 15,943 wanaotambuliwa hadi sasa. Kati yao, wafamasia ni 4,256, mafundi sanifu dawa ni 10,512 na mafundi dawa wasaidizi ni 1,175.

Kwa upande wa majengo ya biashara ya famasi, tayari 487 yamesajiliwa kutoa huduma za dawa nchini, hivyo kufanya jumla ya majengo hayo kufikia 3,718.

“Katika kipindi hiki, wafamasia 3,159, mafundi sanifu dawa 5,305 na mafundi dawa wasaidizi 324 wamefanya mafunzo endelevu, na moduli 17 za mafunzo hayo zimeidhinishwa,” taarifa hiyo imeeleza.