Mawakala wa gesi watakiwa kujiepusha biashara holela

Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Elias Manyaka (katikati) akitoa maelekezo ya namna ya kuzima moto kwa kutumia kizima moto kwa mawakala wa kampuni ya Oryx gas Wanaojihusisha na uuzaji wa gesi za majumbani.

Muktasari:

  • Mawakala wa biashara ya gesi wametakiwa kuwa na mikataba na wasambazaji wakubwa kudhibiti ujazaji holela wa mitungi ya bidhaa hiyo.

Moshi. Mawakala wa uuzaji wa gesi za majumbani mkoani Kilimanjaro wametakiwa kuwa na mikataba na wasambazaji wakubwa wa bidhaa hiyo ili kukabiliana na changamoto ya uuzaji wa gesi zilizo na ujazo pungufu.

Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) Kanda ya Kaskazini, Lorivic Longi'du, ameeleza hayo leo Oktoba 30, 2022 katika mafunzo kwa mawakala wa kampuni ya Oryx wanaojihusisha na uuzaji wa gesi za nyumbani mkoani hapa.

Long'idu amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwakumbusha mawakala wa gesi wajibu, sheria na kanuni zinazotumika katika kudhibiti nishati hiyo ambayo ni muhimu na kuepusha madhara yanayoweza kutokea kutokana na kuuza bidhaa hiyo bila kufuata taratibu.

"Mawakala wa gesi wanapaswa kuwa na mikataba na wasambazaji wakubwa ili kudhibiti ubora wa gesi, kama itatokea mitungi iliyopungua ujazo haitaingia sokoni na pia biashara ya ujazaji holela wa mitungi ya gesi itakoma," amesema Long'idu.

Amesema mpaka sasa katika mkoa wa Kilimanjaro kuna kesi zaidi ya mbili zinazohusisha ujazaji holela wa mitungi ya gesi ambazo zipo mahakamani.

"Wafanya biashara hao wamekua wakichukua mitungi mikubwa na wakati mwingine huvizia gesi inayosafirishwa kwenda nje ya nchi ambapo kwa kiasi kikubwa inapitia katika mkoa wa Kilimajaro na Arusha na hivyo kuchukua gesi hiyo na kujaza kwenye mitungi isivyo halali," amesema Long'idu.

Kwa upande wake Ofisa Masoko wa Oryx, Alex Wambi amesema mafunzo hayo yametolewa kwa mawakala 100 wanaouza gesi za nyumbani na yamelenga kuwaelimisha juu ya matumizi sahihi ya gesi pamoja na namna wanaweza kuuza gesi katika hali ya usalama. 

Akizungumza mara baada ya mafunzo hayo, Alice Shirima anayefanya biashara hiyo amesema licha ya kuuza gesi kwa muda mrefu hakuwa na ufahamu juu ya kuwa na mkataba na wale wasambazaji wa kubwa, hivyo mafunzo hayo yamewajenga katika kuendesha biashara zao kwa faida zaidi.

"Kwenye semina ya leo kuna suala la kuwa na mikataba na wale wasambazaji wakubwa ambao ndio wanatusambazia gesi, hii itakuwa na faida kwetu kwani wakati mwingine unaweza kupata shida ukashindwa kujua ni nani atakusaidia," amesema Shirima.