Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mawakili wa Serikali watakiwa kujiandaa na AI, mikataba ya kimkakati

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari,akizungumza katika mafunzo ya tatu ua Mawakili wa Serikali kutoka Wizara,Idara za Serikali zinazojitegemea,Wakala za Serikali na Mamlaka za Serikali za Mitaa (RS & LGAs) nchi nzima,yaliyoanza leo Jumatano Julai 15, 2026 jijini Arusha.

Muktasari:

  • Maendeleo ya teknolojia, hususan matumizi ya akili unde, yameleta changamoto mpya zinazohitaji wataalamu wa sheria kuwa na uelewa mpana ili kuweza kuzisimamia ipasavyo.

Arusha.  Mawakili wa Serikali nchini wametakiwa kujijengea uwezo zaidi katika usimamizi wa mikataba ya kimkakati na kukabiliana na changamoto mpya za teknolojia, ikiwamo matumizi ya akili unde (AI), ili kulinda maslahi ya taifa na wawekezaji katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Wito huo umetolewa leo Jumatano, Julai 15, 2026 na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari wakati akifungua mafunzo ya tatu ya Mawakili wa Serikali yanayowakutanisha mawakili kutoka wizara, idara za Serikali zinazojitegemea, wakala za Serikali na Mamlaka za Serikali za Mitaa (RS & LGAs) kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo mawakili hao, kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao na kuwawezesha kukabiliana na changamoto mpya katika sekta ya sheria.

Johari amesema maendeleo ya teknolojia, hususan matumizi ya akili unde, yameleta changamoto mpya zinazohitaji wataalamu wa sheria kuwa na uelewa mpana ili kuweza kuzisimamia ipasavyo.

Ametaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni upotoshaji wa taarifa, uhalifu wa mtandaoni na masuala ya usalama wa taarifa, akisema mawakili wa Serikali wanapaswa kuhakikisha mifumo ya sheria inaendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia.

Aidha, amesema Serikali imeanza rasmi utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 tangu Julai Mosi mwaka huu, hivyo mawakili wa Serikali wana jukumu la kuhakikisha sheria, sera na mifumo ya kisheria vinaunga mkono malengo ya kujenga Tanzania yenye uchumi wa kati wa juu, shindani, jumuishi na endelevu.

"Hatutaki mawakili wa Serikali wawe watazamaji wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Tunataka muwe vinara wa mabadiliko na daraja la kufanikisha malengo ya taifa kupitia sheria bora, ushauri wa kisheria wenye weledi na usimamizi madhubuti wa mikataba," amesema Johari.

Amesema sheria na mikataba bora ni msingi muhimu wa maendeleo ya wananchi na ukuaji wa uchumi, hivyo mawakili wanapaswa kuendelea kuongeza ujuzi unaozingatia mabadiliko ya uchumi wa dunia, biashara za kimataifa, teknolojia na siasa za kimataifa.

Johari amesema karibu asilimia 70 ya rasilimali zinazotarajiwa kugharamia utekelezaji wa Dira hiyo zinatarajiwa kutoka sekta binafsi, jambo linalofanya ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP) kuwa eneo muhimu linalohitaji wataalamu wa sheria wenye uwezo wa kusimamia mikataba mikubwa kwa kuzingatia maslahi ya taifa na wawekezaji.

Amesema mafunzo hayo yanahusisha pia mada mbalimbali ikiwemo siasa za kimataifa, usalama wa mtandao na usuluhishi wa migogoro, kwa lengo la kuwawezesha mawakili kutoa ushauri wa kisheria unaolinda maslahi ya nchi.

Kwa upande wake, Mwandishi Mkuu wa Sheria, Onorious Njole amesema mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuendelea kuwajengea uwezo mawakili na maafisa sheria ili waweze kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika mazingira ya sasa ya utendaji kazi.

Amesema mafunzo hayo yamewashirikisha zaidi ya mawakili wa Serikali 350, ambao wanatarajiwa kuongeza uwezo wao wa kitaaluma na kuwa chachu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Naye Mkurugenzi wa Uratibu na Huduma za Ushauri wa Sheria, Wakili Neema Ringo amesema mawakili wa Serikali wana nafasi ya kipekee katika kufanikisha dira hiyo kwa kuwa wanasimamia tafsiri na utekelezaji wa sheria zinazoweka msingi wa miradi ya maendeleo na kulinda maslahi ya taifa.

"Mawakili wa Serikali mna nafasi ya kipekee katika kufanikisha Dira. Ninyi ndiyo mnaoweka msingi wa kisheria unaowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kulinda maslahi ya taifa. Mafunzo haya yanawalenga kuwaongezea uwezo ili kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi zaidi," amesema Ringo.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo mawakili katika maeneo ya uongozi wa kimkakati wa sheria, usimamizi wa mikataba, utatuzi wa migogoro, usimamizi wa hatari za kisheria katika uwekezaji na matumizi ya teknolojia katika sekta ya sheria.