Mbaroni wakituhumiwa kuua swala 28

Nyara na vielelezo vya wanyamapori vilivyokamatwa katika familia ya Masunga Madede katika kijiji cha Mwasilimbi kata ya Ihusi wilayani Bariadi. Picha na Samira Yusuph.

Muktasari:

Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kuua swala 28 wanaokadiriwa kuwa na thamani ya Sh38 milioni katika pori la akiba la Maswa mkoani humo.

Bariadi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kuua swala 28 wanaokadiriwa kuwa na thamani ya Sh38 milioni katika pori la akiba la Maswa mkoani humo.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo Agosti 18, 2023 Kamanda wa Polisi mkoani humo, Edith Swebe amesema watuhumiwa hao walikutwa na nyama ya swala hao katika makazi yao.

Amewataja watuhumiwa hao ni Masunga Madede (58), Mussa Masunga (28) na Yunis Makwaya (45) ambao walitiwa mbaroni kufuatia oparesheni ya pamoja iliyofanyika kijiji cha Mwasilimbi wilayani Bariadi wakiwa na pikipiki iliyokuwa inatumika kusafirishia nyara za Serikali.

“Watuhumiwa hawa walikutwa na nyara za Serikali ambazo ni wanyamapori aina ya swala 28 wakiwa wamewaua, watuhumiwa pamoja na vielelezo watafikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria,”amesema Swebe

Akieleza mikakati ya kulinda wanyamapori katika pori la akiba Maswa, Ofisa Mhifadhi wa pori hilo, Lawrence Okode amesema oparesheni zinazotokana na taarifa fiche zimekuwa na mafanikio.

“Wanyama hao wanathamani  ya Sh38 milioni na hao wamewaua kwa matakwa yao binafsi hivyo tunaendelea kuwatahadharisha wananchi wanaoishi maeneo yanayopakana na mapori yetu ya akiba kujiepusha na uwindaji usio wa kisheria,”amesema