Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbinu zabainishwa kuboresha tafiti, bunifu zinazofanyika Tanzania

Muktasari:

  • Serikali imedhamiria kuhakikisha utafiti na ubunifu vinakuwa nyenzo muhimu katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii sambamba na kujenga Taifa linaloongozwa na maarifa

Dar es Salaam. Ongezeko la rasilimali fedha, uboreshaji wa miundombinu na ujuzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kwa vijana, pamoja na ushirikiano kati ya vyuo vikuu, sekta binafsi na wadau mbalimbali wa maendeleo yametajwa kama baadhi ya mambo yatakayosaidia uboreshaji wa tafiti na bunifu zinazofanyika nchi.

Pia wabunifu, watafiti pamoja na jamii kunufaika na tafiti na bunifu zinazofanyika nchini.

Hayo yamebainishwa leo Jumatau Juni 9, 2025 na wadau mbalimbali walioshiriki katika maadhimisho ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye amebainisha upungufu wa rasilimali fedha, uhusiano hafifu na sekta ya viwanda vimekuwa vikisababisha mkwamo katika ubiasharishaji wa utafiti na bunifu mbalimbali zinazofanyika nchini.

Profesa Anangisye amesema ubiasharishaji wa tafiti na bunifu ni mchakato mpana unaohitaji mazingira bora, ufadhili wa kutosha, ushauri wa kimkakati na ushiriki wa sekta binafsi.

"Pengo kati ya tafiti za vyuo na utekelezaji wake kwenye sekta ya viwanda na biashara ni changamoto inayohitaji ushirikiano wa dhati kati ya taasisi za elimu ya juu, sekta binafsi, Serikali na wawekezaji," amesema.

Anasema lengo ni kuhakikisha bidhaa za ubunifu zinaingia sokoni, zinatengeneza ajira, zinaboresha maisha ya Watanzania na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya Taifa.

Ameongeza ili kufikia malengo hayo amewasihi wadau wa sekta binafsi na wawekezaji kuendelea kushirikiana na watafiti, kutoa ushauri na mitaji itakayosaidia kugeuza mawazo ya kibunifu kuwa biashara na huduma zenye tija kwa jamii.

Kwa upande wake, Mhadhiri kutoka UDSM, Profesa Lilian Kaale amesema ni ngumu kufikia mafanikio hayo bila kuzingatia umuhimu wa kuwepo kwa mifumo madhubuti ya fedha endelevu na usimamizi wa miliki bunifu.

Hivyo, ameshauri kupitia vitengo vya tafiti na ubunifu kuelimisha na kuhamasisha wabunifu na watafiti juu ya masuala ya haki miliki ili kulinda matokeo ya tafiti na bunifu zao.

“Elimu hiyo ni muhimu kuwasaidi kulinda bunifu zao pamoja na tafiti hivyo ni muhimu kuwa na uwelewa wa kutosha ya namna gani wanaweza liziwekea ulinzi kazi zao,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Peter Ulanga amesisitiza uwekezaji zaidi katika teknolojia ili kufikia mapinduzi makubwa katika masuala ya tafiti na bunifu nchini.

Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesisitiza ushirikiano kati ya taasisi za elimu na sekta binafsi ili kusaidia kuzalishwa kwa tafiti na bunifu zitakazoleta suluhu ya changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.

Kitila amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha utafiti na ubunifu vinakuwa nyenzo muhimu katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii sambamba na kujenga Taifa linaloongozwa na maarifa.

"Tafiti na bunifu zinayofanyika nchini hazitakiwi kubaki kwenye makaratasi au majarida ya kitaaluma pekee, bali inapaswa kuwa na mchango wa moja kwa moja katika maisha ya Watanzania," amesisitiza.

Ameongeza Serikali imeweka fedha katika kuhakikisha bunifu na tafiti zinakuwa na matokeo chanya hivyo ni wakati wa kuangalia namna zinavyoweza kwenda sokoni.