Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbowe anusuru nyumba yake kuuzwa, akataliwa kulipwa fidia

Muktasari:

  • Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mary Mrio, ameamuru kuachiliwa kwa nyumba ya Mbowe iliyokamatwa isivyo halali.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi imetupilia mbali maombi ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe la kutaka kulipwa gharama za kesi aliyofungua kuwapinga wanahabari waliokuwa wamekamata nyumba yake isivyo halali ili waipige mnada.

Uamuzi huo umetolewa leo, Machi 13, 2024 na Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Mary Mrio, aliyesikiliza shauri hilo baada ya kukubaliana na hoja ya wanahabari hao, Maregesi Paul na wenzake tisa, kuwa Mbowe hana haki ya kulipwa gharama kwa shauri la aina hiyo.

Akitoa uamuzi huo  Mrio ameamuru kuachiliwa kwa nyumba hiyo, lakini akamkatalia Mbowe maombi yake ya kulipwa gharama kwa kile alichokuwa akidai kuwa wanahabari hao walikamata nyumba yake hiyo isivyo halali.

Mrio amesema kwa mujibu wa kanuni ya 51 (1) ya Kanuni za Mahakama ya Kazi, Tangazo la Serikali (GN) namba 106 la mwaka 2007, Mbowe hastahili kulipwa gharama katika shauri hilo.

Amesema  kanuni hiyo inaeleza kwamba hakuna gharama itakayotolewa kwa upande wowote kwenye shauri la aina hiyo (mgogoro wa kikazi) isipokuwa tu kama kuna shauri lililofunguliwa linakuwa halina maana bali la usumbufu tu.

“Kwa kusema hayo Mahakama hii imeona hakuna haja ya kutoa gharama za kesi, hivyo kila upande utabeba gharama zake,” amesema Mrio.

Baada ya uamuzi huo, wakili wa Mbowe, John Mallya alifanya mawasiliano kwa njia ya simu na Mbowe kisha akawaeleza wanahabari hao kuwa mteja wake huyo yuko safarini lakini ameomba wakutane Jumatano kwa majadiliano kuhusu madai ya mishahara yao ili kumalizana nje ya Mahakama.

Mbowe alifungua shauri hilo baada ya wanahabari hao kukamata nyumba yake ili ipigwe mnada kutokana na deni la malimbikizo ya mishahara yao wanayomdai mkurugenzi wa gazeti la Tanzania Daima walilokuwa wakifanyia kazi, Dadley Mbowe ambaye ni mtoto wa Mbowe.

Wanahabari hao walikamata nyumba hiyo ya ghorofa moja iliyoko katika kiwanja namba 9, Mtaa wa Feza, Mikocheni B, Februari 28, 2024 kupitia kwa dalali wa Mahakama, Kampuni ya Udalali ya MM Auctioneer & Debt Collectors, kwa amri ya Mahakama hiyo.

Mahakama hiyo iliamuru kukamatwa na kupigwa mnada nyumba hiyo Machi 14, 2024, kufuatia maombi ya wanahabari hao katika shauri lao la maombi ya utekelezaji wa tuzo iliyotolewa kwao na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA).

Paul na wenzake walifungua shauri hilo la utekelezaji wa tuzo ya CMA mahakamani hapo dhidi ya Dudley baada ya kushindwa kutekeleza tuzo hiyo ya CMA, kuwalipa deni la malimbikizo ya mishahara yao kiasi cha Sh62.7 milioni.

Baada ya mdaiwa huyo, kushindwa kufika mahakamani mara tatu, katika shauri hilo la maombi ya utekelezaji ndipo wanahabari hao waliiomba Mahakama hiyo kuamuru wakakamata nyumba ili ipigwe mnada walipwe deni.

Hata hivyo, Mbowe naye alifungua shauri la maombi mahakamani hapo dhidi ya wanahabari hao, mkurugenzi huyo wa gazeti la Tanzania Daima (mwanaye Dudley) na dalali huyo wa Mahakama akipinga kukamatwa na kupigwa mnada kwa nyumba hiyo.

Katika shauri hilo, alikuwa akipinga nyumba yake hiyo kukamatwa, akidai kuwa wanahabari hao waliikamata isivyo halali.

Katika hati yake ya kiapo na wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo kupitia kwa wakili wake, John Mallya, alidai kuwa si mali ya mdaiwa wao bali yeye ndiyo mmiliki wa hiyo nyumba.

Pia, alidai kuwa yeye si sehemu ya shauri hilo la maombi ya utekelezi lililofunguliwa na wanahabari hao na wala hawana madai yoyote dhidi yake.

Hivyo, alikuwa aliiomba Mahakama hiyo ifanye uchunguzi wa usahihi wa kukamatwa kwa nyumba hiyo, kisha itoe ukamatwaji huo si halali na ni batili na itoe amri ya kuachiliwa.

Sambamba na amri hiyo ya kuachiwa nyumba hiyo, pia Mbowe aliomba mahakama iamuru wajibu maombi hao (wanahabari) walipe gharama halisi alizozitumia mpaka tarehe ya kuachiliwa kwa nyumba hiyo na nafuu nyingine kadri Mahakama itakavyoona inafaa.