Mbowe atoa angalizo mkataba wa bandari

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akizungumza katika moja ya tukio la chama hicho. Picha na Mtandao.

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amekosoa hatua ya Serikali kuingia makubaliano na Serikali ya Dubai katika ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari nchini, akiitaka Serikali kufikiria upya.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amekosoa hatua ya Serikali kuingia makubaliano na Serikali ya Dubai katika ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari nchini, akiitaka Serikali kufikiria upya.

Uchambuzi huo wa Mbowe unaakisi mjadala unaoendelea nchini kuhusu mkataba uliosainiwa Oktoba 25, mwaka jana kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kwa ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari (IGA).

Mkataba huo unafanyika baada ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kusaini hati ya hakubaliano (MoU) na kampuni ya kimataifa ya huduma za bandari Dubai Port World (DPW) kutoka Dubai.

Makubaliano hayo yalibainisha maeneo mahsusi ya ushirikiano ili kuendeleza na kuboresha uendeshaji wa miundombinu ya kimkakati ya bandari za bahari na maziwa makuu, maeneo maalum ya kiuchumi, maeneo ya maegesho na utunzaji mizigo na maeneo ya kanda za kibiashara.

Akitoa tamko la chama hicho leo Juni 7 kupitia mtandao wa Club House akiwa nchini Ujerumani, Mbowe ameonyesha wasiwasi wa kutoa dhamana hiyo ya kuendesha bandari zote katika bahari na maziwa kwa mwekezaji mmoja.

“Hatujajifunza kutokana nay ale yaliyotokea baada ya kubinafsisha Tanesco, Shirika la Reli (TRL), ATCL na mashirika mengine na hasara kubwa tuliipata kama Taifa,”alisema Mbowe.

Pili, amehoji hatari iliyopo baada ya mkataba kuanza kutumika kabla ya kuridhiwa na Bunge, ikiwamo shughuli za upembuzi yakinifu hivyo Bunge kuridhia mkataba bila kuwa na mamlaka ya kubadilisha chochote kilichopitishwa katika mkataba huo.

Tatu ni hoja ya usuluhishi wa mgogoro kufikishwa kwenye Baraza la Usuluhishi, chini ya Sheria za Usuluhishi za Kamisheni ya Umoja wa Mataifa juu ya Sheria zinazohusika na Biashara za Kimataifa.

Amesema hatua hiyo ni kinyume na maelekezo ya kifungu cha 11 cha Sheria ya mamlaka ya nchi kuhusiana na umiliki wa rasilimali na maliasili za Tanzania ya mwaka 2017, kinachoelekeza migogoro yote ya aina hiyo itatatuliwa katika vyombo vya sheria vya Tanzania.

Nne, ni kuhusu wasiwasi wake katika kifungu kinachonyima pande mbili mamlaka na haki za kusitisha mkataba huo. Kwa mujibu wa mkataba huo, ridhaa au idhini ya kuvunja mkataba haitazuliwa na upande mmoja bila kutoa sababu za msingi.

Aidha, amesema kwa hatua hiyo Serikali husika hazitakuwa na haki ya kuvunja mkataba, kujitoa, kuahirisha au kusitisha mkataba katika mazingira yoyote yale.

“Jambo hili ni hatari na linaondoa uhuru wa nchi yetu yaani sovereignty, inawezekanaje kuingia mkataba ambao hata upande wa pili unapokiuka kwa makusudi huwezi kujitoa au kuvunja mkataba husika,”alihoji Mbowe.

Tano, ni wasiwasi kuhusu kukosekana muda wa ukomo wa mkataba huo. Kwa mujibu wa mkataba huo, ukomo wa mkataba huo ni mpaka hapo shughuli za mradi huo zitakapokuwa zimekamilika. Serikali iombwe kutoa ufafanuzi kuhusu jambo hili la ukomo wa mkataba.

 “Kwa hiyo Serikali haitakuwa na haki ya kuanzisha au kuendeleza bandari zake kwa kipindi ambacho hakijulikani.

“Tunawezaje kuweka mipango ya kuendeleza bandari zetu kama hatujui mkataba unamalizika vipi? Pia Serikali haitabadilisha sheria zake katika uendeshaji bandari kwa muda usiojulikana,” amehoji.