Mbowe: Hatukuwa na wagombea sahihi

What you need to know:

  • Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe amekiri kuwa walikuwa na baadhi ya wagombea ambao hawakuwa wakikubalika kwenye maeneo waliyogombea nafasi mbalimbali ikiwemo ubunge na madiwani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Mwanza. Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe amekiri kuwa walikuwa na baadhi ya wagombea ambao hawakuwa wakikubalika kwenye maeneo waliyogombea nafasi mbalimbali ikiwemo ubunge na madiwani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Pia, amesema kwa sasa falsafa zake za kisiasa zinakwenda sawa na zile za aliyekuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi Marekani, Thomas "Tip" O'Neil Jr.

Amesema O'Neil kupitia kitabu chake cha 'All Politics is Local' amesema siri za ushindi za chama cha siasa ambazo ndizo anazutimia kuongoza mapambano ya kushika dola nchini.

Amezitaja falsafa hizo kuwa ni chama kupata mgombea sahihi na nayekubalika kwa wapiga kura.

"Nikiri kuna maeneo mengi tulikuwa na wagombea sahihi, lakini kuna maeneo kadhaa tulikuwa na wagombea dhaifu, huo ni ukweli na haupingiki kwa sababu waswahili wanasema wali wa kushiba unaonekana kwenye sahani," amesema Mbowe.

Ametaja jambo la pili kuwa ni chama kuwa na ajenda ya kuwashawishi wanachi kukichagua, ambapo kwa upande wa Chadema, Mbowe amesema hakijawahi kukosa ajenda ya kushindana na Chama tawala-CCM.

"Ilani yetu ya uchaguzi ilikuwa bora kwa sababu imefanyiwa utafiti," amesema.

Mambo mengine ambayo Mbowe ameyataja ni kuwa na uongozi imara na rasilimali fedha ambapo kwa sasa chama kinatengeneza miundombinu rafiki ikiwemo kuwekeza kwa vijana na kukuza teknolojia kutoka analojia kwenda dijitali.

"Sasa hivi wanachama wa Chadema ni ambao hawazidi umri wa miaka 45 hii ni dalili nzuri kwamba, upinzani utakuwa imara zaidi lakin pia tunapambana kuhakikisha kila kitu tunachokifanya kinafanyika kidijitali," amesema Mbowe.

Kiongozi huyo amesema kikao cha Kamati ya Utendaji ya Chadema Kanda ya Victoria kimeafiki kuwa kila Jumamosi kuwa siku ya kuvaa sare ya Chama hicho kwa wanachama wake.

"Tunatambua kuwa wana Chadema walikuwa wameshaanza kusahau hadi kuvaa sare, lakini sasa wanachama wa Chadema watavaa sare kila Jumamosi ili kuongeza motisha na idadi ya wafuasi wetu," amesisitiza.

This page might use cookies if your analytics vendor requires them.