Mbowe, Mnyika na Sugu watua Mwanza kukiwasha

Baadhi ya madereva bodaboda, bajaji na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiwa eneo la dampo Buhongwa jijini Mwanza tayari kwa uzinduzi wa mkutano wa chama hicho unaofanyia leo Januari 21, 2023. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

  • Mikutano ya kisiasa imerejea baada ya kuzuia kwa takribani miaka saba tangu mwaka 2016 kwa amri ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli kwa madai ya kutoa fursa kwa Serikali na Watanzania kufanya kazi kujenga uchumi; ni wabunge na madiwani ndio waliruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo yao ya uchaguzi.

Mwanza. Viongozi wa kitaifa wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, John Mnyika na wajumbe wa Kamati Kuu wakiwemo wabunge wa zamani Joseph Mbilinyi maarufu  Sugu na Mchungaji Peter Msigwa tayari wametua jijini Mwanza kwa ajili ya mkutano wa hadhara unaofanyika jijini humo leo.

 Viongozi na makada wengine wa Chadema waliotua Mwanza ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa chama hicho (Bawacha), Sharifa Suleiman, katibu wake, Catherine Ruge, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee (Bazecha), Hashim Issa Juma na wabunge wa zamani Suzan Kiwanga na Suzan Lyimo.

Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zakaria Obadi amewataja makada wengine ambao tayari wako Mwanza ni Meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob, John Heche na John Pambalu ambao pia ni wenyeji wa mkutano huo wa hadhara unaofanyika katika viwanja vya Furahisha jijini Mwanza leo Jumamosi Januari 21.

Bila kutaka kuingia kwa undani suala hilo, Obadi amesema viongozi hao wako sehemu maalum kwa ajili ya mapumziko kabla ya mapokezi rasmi yanayotarajiwa kufanyika eneo la Buhongwa, nje kidogo ya jiji la Mwanza.

“Kutoka Buhongwa, viongozi hao na msafara wao wataenda moja kwa moja hadi uwanja wa Furahisha ambako mkytano wetu unafanyika,” amesema Obadi

Akizungumzia mkutano huo unaofanyikia Uwanja wa Furahisha leo Jumamamosi, Januari 21, 2023, Heche ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema amesema licha ya kufanyika jijini Mwanza, mkutao huo utahudhuriwa na makada wa chama hicho kikuu cha upinzani kutoka mikoa jirani ya Shinyanga, Geita, Mara na Simiyu.

Chadema yakiwasha Mwanza, Mbowe achukizwa 'kulamba asali'

 “Wana Chadema na Watanzania kwa ujumla wamekosa hamasa ya mikutano ya kisiasa kwa takribani miaka saba; kuna hamasa kubwa na tangazo la mikutano yetu ya Mwanza na Mara imepata mapokezi chanya kutoka kwa umma. Tunatarajia kuwa mikutano mikubwa ya kihistoria kote nchini,” amesema Heche

Agnes Mabula, mkazi wa mtaa wa Nyabulogoya eneo la Nyegezi jijini Mwanza ameendeleza pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusahihisha makosa ya mtangulizi wake, Hayati John Magufuli kwa kuruhusu mikutano na shughuli za kisiasa kufanyika kwa mujibu wa sheria na katiba.

“Rais Samia ameonyesha ukomavu siyo tu wa kiuongozi, bali pia kisiasa kwa sababu naamini wapo wana CCM ambao wangependa kuona vyama vya upinzani vikinyimwa fursa ya kufanya siasa kama ilivyokuwa wakati wa mtangulizi wake John Magufuli; kwa hili Rais Samia anastahili pongezi,” amesema Agnes