Mbunge ataka sheria mahususi ya ukatili wa kijinsia
Muktasari:
- Imeelezwa kuwa, Sheria ya Kanuni ya Adhabu; Sheria ya Ndoa, Sheria ya Mtoto, Sheria ya Makosa ya Mtandao na Sheria ya Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu zinavifungu vinavyozuia makosa ya ukatili wa kijinsia
Dodoma. Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na wizara nyingine na asasi za kiraia zinafanya tathmini ili kubaini iwapo kuna haja ya kuwa na sheria mahususi ya ukatili wa kijinsia au kuboresha sheria zilizopo.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini amesema hayo leo Jumanne Juni 11, 2024 wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalumu, Tamima Haji Abbas.
Mbunge huyo amehoji ni lini Serikali itatunga sheria mahsusi kwa makosa ya ukatili wa kijinsia.
Amesema Sheria ya Kanuni ya Adhabu; Sheria ya Ndoa, Sheria ya Mtoto, Sheria ya Makosa ya Mtandao na Sheria ya Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu zinavifungu vinavyozuia makosa ya ukatili wa kijinsia na vifungu vinavyohusika na makosa ya ukatili wa kijinsia.
“Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na wizara nyingine na asasi za kiraia inafanya tathmini ili kubaini iwapo ipo haja ya kuwa na sheria mahususi ya ukatili wa kijinsia au tuboreshe sheria zilizopo,” amesema Sagini.
Amesema tathmini hiyo ikikamilika, itasaidia Serikali kufanya uamuzi sahihi kuhusu suala la kutunga sheria mahsusi kwa makosa ya ukatili wa kijinsia au kuboresha sheria zilizopo.
Akiuliza swali la nyongeza, Tamima amehoji ni kigezo gani cha kubainisha haja ya kutunga sheria mahususi ya makosa ya ukatili wa kijinsia.
“Kwa kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia vinazidi kushamiri nchini wakati sheria ipo je Serikali inatuambia ni nini kuhusiana na hali hiyo,” amehoji.
Akijibu swali hilo, Sagini amesema vigezo vinavyofaa kutengeneza sheria, ni tathimini ya uzito ama ukengeufu unaosababishwa na mtawanyiko wa sheria hizo, hususani zikishafanyika na Tume ya Marekebisho ya Sheria huishauri Serikali.
Amemtaka mbunge huyo kuipa nafasi Serikali kupitia Tume ya Marekebisho ya Sheria, inayohusisha wadau mbalimbali wakiwamo wabunge na kuwa watapata msimamo wa pamoja wa namna ya kuliendea jambo hilo.
Kuhusu kushamiri matukio ya ukatili wa kijinsia, Sagini ameiasa jamii kuzingatia maadili ya jamii kwa kuwa karibu Tanzania ambayo ina mila, desturi na dini ambazo zote hakuna hata moja inayoruhusu vitendo hivyo vinafanyika.
“Lakini maadamu yanafanyika katika jamii zetu niase pale inapotokea wahusika watoe taarifa katika vyombo vyetu ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani wahusika,”amesema.
Mbunge wa viti maalumu, Mwantum Dau Haji ametaka Serikali kutunga sheria haraka ili wabakaji waache ukatili wa kijinsia.
Akijibu swali hilo, Sagini amesema zipo sheria mbalimbali nchini ambazo zinaweza kuwathibiti watu wanaofanya matukio mbalimbali ya ukatili wa kijinsia.
“Ikiwa mambo yamefanyika katika mitandao, tutatumia sheria ya mitandao, ikiwa amefanyiwa mtoto zipo sheria za mtoto,”amesema.