Mbunge, DC wa zamani afa ajalini

Mkuu wa wilaya ya Misungwi, Juma Sweda
Muktasari:
Makanga aliyekuwa katibu wa uenezi CCM mkoani Simiyu, alifariki dunia jana katika ajali iliyosababishwa na bodaboda kugongana na bajaj wilayani Misungwi.
Mwanza. Aliyewahi kuwa mbunge wa Bariadi Magharibi na mkuu wa wilaya za Same, Kwimba na Kibondo, Danhi Makanga amefariki dunia katika ajali.
Makanga aliyekuwa katibu wa uenezi CCM mkoani Simiyu, alifariki dunia jana katika ajali iliyosababishwa na bodaboda kugongana na bajaj wilayani Misungwi.
Mkuu wa wilaya ya Misungwi, Juma Sweda alisema ajali hiyo ilitokea jana eneo la Nyashishi na Makanga alikuwa amepakiwa kwenye bodaboda.
Bila kueleza chanzo cha ajali hiyo, Sweda alisema Makanga na dereva wake waligongana na bajaj hiyo hivyo kusababisha vifo vya wote wawili huku dereva wa bajaj akijeruhiwa.
Akizungumzia ajali hiyo, mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Misungwi, Daud Gambandu alisema amepokea kwa mshtuko na kwa simanzi kubwa taarifa hizo kwa kuwa anamfahamu kiongozi huyo aliyewahi kutumikia wananchi katika awamu ya nne ya uongozi ya Rais Jakaya Kikwete.