Mbunge ‘Jah People’ avuta jiko

Mbunge wa Makambako mkoani Njombe, Deo Sanga maarufu ‘Jah People’ (wa tatu mbele) na mkewe Suzana Kapasi (wa pili kushoto) baada ya kufunga ndoa.

Muktasari:

Mbunge wa Makambako mkoani Njombe, Deo Sanga maarufu ‘Jah People’ amefunga ndoa na mkewe Suzana Kapasi.

Dar es Salaam. Mbunge wa Makambako mkoani Njombe, Deo Sanga maarufu ‘Jah People’ amefunga ndoa na mkewe Suzana Kapasi.

Ndoa hiyo imefungwa leo Jumatano Septemba 14, 2022 mchana katika kanisa Katoliki la Ilangamoto katika Mji wa Makambako mkoani humo.

Baada ya ndoa hiyo, hivi sasa sherehe zinaendelea katika uwanja wa mpira wa miguu wa Amani.

Viongozi mbalimbali wamehudhuria akiwemo Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, Waziri wa Maliasili na Utali, Dk Pindi Chana.

 Wengine ni wabunge mbalimbali akiwemo William Lukuvi (Isimani-Iringa), Festo Sanga (Makete) na Joseph Kamonga (Ludewa) pamoja na wananchi wa Mji wa Makambako.

Wakila kiapo cha ndoa kanisani, Sanga na Suzana walikubali kuishi pamoja na katika maisha yake yote ya ndoa iwe shida na raha.

Padri Ladislaus Mgaya wa Jimbo la Katoliki Njombe ndiye aliyewafungisha ndoa hiyo.

“Iwe ishara ya upendo na uaminifu wangu kwako,” amesema Sanga mwenye umri wa miaka 66 wakati akimvisha pete mkewe kanisani.

“Kupitia pete hii iwe ishara kwangu ya upendo na uaminifu kwako,” amesema Suzana.